KATIKA jitihada za kuinua ubora wa elimu ya ufundi nchini, Baraza la
Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) limevifutia usajili vyuo vitatu na
kuvishusha hadhi vyuo kumi na sita.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu
Katibu Mtendaji wa NACTE, Dk Adolf Rutayuga alisema hatua hiyo imefikiwa
baada ya vyuo husika kushindwa kurekebisha kasoro zilizobainishwa na
NACTE.
“Kwa kutumia Sheria ya Bunge Sura Na. 129 na Kanuni za Baraza za
Usajili (2001) na zile za Ithibati na Utambuzi (2001), mnamo tarehe 20
Februari 2015, Baraza lilitoa notisi ya siku 30 kwa taasisi na vyuo
vilivyokiuka taratibu na vyenye mapungufu makubwa ya Usajili na Ithibati
kupitia taarifa yake kwa Umma. Notisi hii ililenga kuzipa taasisi na
vyuo nafasi ya kujitetea na kufanya marekebisho yaliyobainishwa,”
alieleza.
Kaimu Katibu Mtendaji huyo ambaye ni Mkurugenzi wa Ushauri na Malezi
ya Taasisi na Vyuo vya Ufundi NACTE aliwaambia waandishi wa habari kuwa,
Baraza linakiri kuwa taasisi na vyuo vingi vilivyopewa maelekezo ya
kufanya marekebisho vimechukua hatua mbalimbali za kurekebisha mapungufu
yabainishwa.
Hata hivyo alisema hadi kufikia leo tarehe 24 Juni 2015 yaani siku
124 baada ya Notisi ya Baraza, kuna vyuo ambavyo havijachukua hatua
yoyote ya kurekebisha mapungufu yake.
“Baraza limeamua kuchukua hatua kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zake
kwa taasisi na vyuo vyote vilivyoorodheshwa kwa makosa yafuatayo, moja
kumalizika kwa muda wa Usajili wa Awali (Preparatory Registration) na
Usajili wa Muda (Provisional Registration); pili kutoanza mchakato wa
kupata Ithibati baada ya kupata Usajili Kamili; tatu kumalizika kwa muda
wa Ithibati na kutochukuliwa hatua ya kuomba upya Ithibati
(re-affirmation); na nne taasisi na Vyuo kuamua vyenyewe kusitisha kutoa
mafunzo kwa sababu mbali mbali,” alifafanua.
Vyuo vilivyofutiwa usajili ni pamoja na Dar es Salaam College of
Clinical Medicine cha jijini Dar es Salaam kilichokuwa kimepatiwa
usajili wa awali, Ndatele School of Medical Laboratory Sciences cha
Dar-es-Salaam kilichokuwa kimepatiwa usajili wa awali na Institute for
Information Technology cha jijini Dar es Salaam pia chenye namba za
usajili REG/EOS/014.
Taasisi/vyuo vilivyoshushwa hadhi baada ya kushindwa kutimiza
masharti ni pamoja na Sura Technologies – Dar es Salaam, Institute of
Management and Information Technology – Dar es Salaam, Techno Brain -
Dar es Salaam, Ministry of Agriculture Training Institute Igurusi –
Mbeya, Mbozi School of Nursing – Mbeya, KCMC AMO Ophthalmology School –
Moshi, KCMC AMO Anaesthesia School – Moshi, Advanced Pediatrics Nursing
KCMC – Moshi.
Vingine ni, AMO Training Centre Tanga – Tanga, CATC – Songea, CATC –
Sumbawanga, COTC Maswa – Shinyanga, COTC – Musoma, Dental Therapists
Training Centre – Tanga, Ngudu School of Environmental Health Sciences –
Kwimba na KCMC AMO General School – Moshi.
0 comments:
Post a Comment