Kada wa CCM, Ritha Ngowi akionyesha begi lenye fomu za kuomba kugombea kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia chama cha CCM baada ya kukabidhiwa makao makuu ya chama hicho mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
DODOMA
Kada wa CCM, Ritta Ngowi amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama kuwania urais katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba mwaka huu na kusema akifanikiwa ataanzisha kituo kikubwa cha kuwahudumia wastaafu, walemavu, wasiojiweza na vijana.
Kuchukua fomu kwa mwanamama huyo, kunafanya idadi ya wanawake waliojitosa mbio za urais kufikia watano kati ya 39 waliochukua fomu hadi sasa.
Wanawake wengine ni Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa (NIMR), Dk Mwele Malecela, Balozi Amina Salum Alli na Monica Mbega.
Akizungumza jana, Ritta ambaye hakuongozana na wapambe kama ilivyokuwa kwa makada wengine wanaowania nafasi hiyo, alifika saa tatu asubuhi kuchukua fomu hizo.
Ngowi alisema yeye ni mtu anayependa kukaa, kufanya kazi na kusaidia jamii.
“Na katika suala zima la utendaji wangu, nimefanya kazi moja kwa moja na jamii, sijawahi kukaa ofisini,” alisema Ritta.
“Kama nikipata nafasi hii, nitaendeleza mazuri yaliyofanywa na marais waliopita, lakini zaidi nikiweka mkazo kwenye masuala ya elimu na kukuza uchumi,” alisema.
Alisema angependa kuona kila mwananchi anapata elimu na kusiwapo na mtu atakayekaa bila kuwa na shughuli halali ya kufanya.
“Lengo langu ni kuondoa hali ya Watanzania kukaa bila kufanya kazi na vijana wasikae kwenye makundi yasiyo na tija,” alisema Ritta.
Alisema pia ana lengo la kuanzisha kituo kikubwa cha wastaafu, wasiojiweza, walemavu wasio na msaada na vijana wasio na mazingira ya kuajiriwa.“Vijana hawa tutawahifadhi katika kituo kitakachokuwa na maji, hospitali, shule na huduma mbalimbali,” alisisitiza.
Kuhusu elimu, alisema kuna watoto wengi wanashindwa kwenda shule kwa sababu ya kukosa ada hivyo kama atapata ridhaa ya kuongoza, atahakikisha Serikali inabeba jukumu la kuwasomesha.
“Nitaangalia suala la ujenzi wa vivuko katika maeneo yenye foleni kubwa kiasi cha kuathiri uchumi wetu,” alisema.
0 comments:
Post a Comment