Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana akizungumza katika mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya furahisha jijini Mwanza jana.Picha na Michael Jamson.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ameikosoa Serikali ya chama chake kwamba imekuwa siyo sikivu kwa matatizo ya wananchi na kuwa wabunge wa chama hicho wanapitisha sheria ambazo zinakuwa mzigo kwa wananchi.
Akihutubia katika mkutano wa kuhitimisha ziara
yake, jijini Mwanza jana, Kinana alisema atafanya kikao cha kwanza na
wabunge wa CCM baada ya uchaguzi ili kuwaeleza majukumu yao ya msingi
ikiwamo kuiwajibisha Serikali.
Alisema wabunge wa CCM wamekuwa wakiunga mkono
kila jambo linaloletwa bungeni bila kutathmini matokeo ya sheria hizo
kwa wananchi wanaowawakilisha.
Alisema lazima ifike wakati wabunge wa CCM wabadilike na kuwatumikia wananchi wao.
“Nitakutana na wabunge wa CCM na kuwaambia kwamba
sheria walizozipitisha haziwasaidii wananchi… lazima chama kiwe na nguvu
ya kuielekeza au kuiwajibisha Serikali yake,” alisema Kinana huku
akishangiliwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Katibu Mkuu huyo alisema kuna haja ya kubadilisha
mfumo wa utendaji kazi wa chama na mojawapo ni kuchagua mtu mwingine wa
kuongoza wabunge wa CCM bungeni badala ya Waziri Mkuu kama ilivyo sasa.
Alisema Waziri Mkuu ataachwa atekeleze jukumu lake
la kuiongoza Serikali bungeni, lakini kuwe pia na kiongozi wa wabunge
wa CCM bungeni. Alisema mfumo huo utakipa chama nguvu zaidi ya
kuisimamia Serikali yake.
“Wamekaa wabunge tena na kupitisha sheria ya kila
gari kuwa na kizimamoto, nani alisema gari langu lina mpango wa
kuungua?” alihoji kiongozi huku na kusema sheria nyingine zinatakiwa
kufutwa kwa sababu hazimsaidii mwananchi.
Aliishangaa Serikali ya CCM kwa kushindwa kufuta
baadhi ya sheria ambazo zimebainika kuleta usumbufu kwa wananchi na
kusisitiza kuwa lazima ifike wakati Serikali ifanye tathmini ya sheria
zake na kuzifuta ambazo hazifai kwa sasa.
“Nimekuwa waziri na kiongozi serikalini kwa muda
mrefu, lakini sijawahi kuona Serikali ikifuta sheria. Wamekuwa
wakiongeza sheria mpya kila siku. Hivi karibuni Serikali imepeleka
miswada mingine 11 na yote imepitishwa. Kwa namna hiyo tunambebesha
mwananchi mzigo mkubwa,” alisema.
Kinana aliitaka Serikali kuwashirikisha wananchi
wakati wa kutunga sheria ili kuondoa changamoto ambazo zimekuwa
zikijitokeza mara kwa mara.
0 comments:
Post a Comment