METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, February 5, 2024

SERIKALI YATOA KIPAUMBELE KUBORESHA NA KUKAMILISHA MIUNDOMBINU KWENYE MAENEO YA KIUTAWALA


IMEELEZWA kuwa kwa sasa, Serikali imetoa kipaumbele katika kuboresha na kukamilisha miundombinu kwenye maeneo yakiutawala yaliyopo, ili yaweze kutoa huduma kwa ufanisi zaidi na baadae kuendelea na maeneo mengine kwa kufuata taratibu na vigezo vilivyoainishwa. 

Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa TAMISEMI Festo Dugange alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Singida Kaskazini Abeid Ramadhani alipouliza Je, lini Serikali itazigawa Kata za Mtinko, Makuro, Ughandi na Ngimu pamoja na kukifanya Kijiji Kivuli cha Mikulu kuwa Kijiji kamili.

"Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa ABEID IGHONDO RAMADHANI, Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini kama ifuatavyo, 

Mheshimiwa Spika, Uanzishwaji wa maeneo mapya ya utawala katika Mamlaka za Serikali za Mitaa hufanyika kwa kuzingatia mwongozo wa Mwaka 2014 ambapo kusudio hujadiliwa katika vikao vya Ngazi ya Halmashauri, Wilaya na Mkoa kisha kuwasilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI,"alisema.

Kadhalika alisema kuwa maombi ya kugawa Kata za Mtinko, Makuro, Ughandi na Ngimu pamoja na kijiji cha Mikulu yatafanyiwa kazi na Serikali itakapoanza kuanziasha maeneo mapya ya utawala.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com