METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, April 17, 2023

VIONGOZI WA DINI IKUNGI WATAKIWA KUKEMEA VIKALI KUHUSU MAPENZI YA JINSIA MOJA








Na Mathias Canal – Ikungi, Singida

VIONGOZI wa Dini Mkoani Singida wametakiwa kuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vya mmomonyoko wa Maadili ambavyo ni kinyume na mila na desturi na kwamba watumie nafasi yao  kuibadilisha mitazamo  juu ya utamaduni huo.

Kauli hiyo imetolewa April 16, 2023 na Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Mhe. Miraji Mtaturu wakati akizungumza na viongozi wa dini ya Kiislamu katika msikiti wa mji wa Makyungu Wilayani Ikungi ambapo amesema Viongozi wa Dini wana nafasi kubwa ya kuiusia jamii kufuata Maadili yanaelezwa kwenye vitabu vitukufu.

Mhe. Mtaturu alisisitiza kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakitumia kivuli cha haki na usawa jambo linalosababisha kukithiri kwa vitendo vinavyokiuka maadili ya Tanzania ikiwemo Mapenzi ya Jinsia moja.

“Viongozi wa Dini Mnanguvu ya ushawishi kwa waumini (Wananchi), kuna hili suala ya Haki na usawa ambalo baadhi ya watu wamekuwa wakitumia kivuli hicho kukiuka maadili yetu, niwaombe Viongozi wangu wa Dini mlikemee na kulipinga vikali hili”Alisema Mhe. Mtaturu.

Katika Hatua nyingine Mhe. Mtaturu aliongeza kwa kuwataka viongozi wa Msikiti huo kubuni Miradi ya maendeleo badala ya kutegemea wafadhili jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya Waislaamu wa eneo hilo.

Aliongeza kuwa hivi karibuni ataletwa mtaalamu wa michoro kwaajili ya kulipangilia eneo la Msikiti Makyungu ili kuongezea thamani kwa kujenga Vibanda vya kukodisha wafanyabishara pamoja na Ukumbi wa Mikutano utakaowaingizia kipato waumini hao.

Kuhusu Miradi Mhe. Mtaturu alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kutekeleza miradi hiyo ikiwemo Sekta ya nishati, Miundombinu ya Barabara na Mawasiliano, Maji, Shule na Afya kwenye wilaya hiyo na kuwahakikishia kuendelea kuwasemea wananchi wa Jimbo la Singida Mashariki kwa ujumla.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com