METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, April 17, 2021

Waziri Bashungwa Kumaliza Mzozo wa Simba na FCC Jumatatu


Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Serikali imesema vikwazo vilivyoibuka katika mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu ya Simba huenda vikamalizika Jumatatu ijayo wakati Tume ya Ushindani (FCC) itakapokutana kwa mara ya tatu na pande zinazohusika.


Jumanne Aprili 13, 2021 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu ya Simba, Mohammed 'Mo' Dewji kupitia mtandao wake wa kijamii wa Twitter alieleza kusikitishwa kwake na FCC akidai kuwa uongozi wa klabu hiyo na FCC wanafanya vikao na baada ya kumaliza wanaandikiwa barua ya kuwataka waanze upya mchakato.


Leo Ijumaa Aprili 16, 2021 akiwa Bungeni jijini Dodoma Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa alizungumzia suala hilo baada ya mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi kuibua mjadala akitaka kushika shilingi Ofisi ya Waziri Mkuu.


Shangazi (CCM), aliitaka Serikali kumaliza ukiritimba kwenye uwekezaji nchini, akiutolea mfano uwekezaji wa Mo Dewji katika klabu hiyo kongwe nchini akisema wanaicheleweshea Simba kufikia kwenye mafanikio.


Shangazi alisema hakuna sheria maalum inayoongoza uwekezaji katika Sekta ya Michezo, bali sheria inayotumika ni ya Baraza la Michezo (BMT) ambayo alidai ina upungufu akahoji ni lini serikali itawasilisha bungeni sheria hiyo ili kumaliza mvutano.


Waziri wa Nchi, Ofisi nya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Geofrey Mwambe alisema “Kilichotokea ni kwamba, zilikwenda kampuni nne na mwekezaji mmoja, baada ya hapo Tume ya Ushindani (FCC) ilibaini upungufu katika mchakato mzima," amesema Mwambe.


Amesema tume iliagiza Simba ijibu dosari zilizojitokeza, lakini baada ya hapo wakaenda mahakamani baadae wakakubaliana waondoe kesi mahakamani na kurejea meza ya maridhiano, jambo ambalo linaendelea hata sasa.


Waziri amesema Serikali inafuatilia kwa karibu kuona mgogoro huo unakwisha kwa manufaa ya maendeleo ya michezo na uwekezaji nchini.


Hata hivyo Shangaza alisimama na kusema wanachokililia wabunge ni Sera ya Uwekezaji ambayo itaondoa ukiritimba huo.


Ndipo akasisima Waziri Bashungwa, ambaye alisema iko fursa ya uwekezaji katika Sekta ya Michezo na Sheria Na. 18 (a) inabanisha kwamba mtu anaweza kuwekeza kwenye timu ya michezo kwa kiwango kisichozidi asilimia 49 ya hisa na kwamba ndicho kilichozingatiwa katika uwekezaji kwenye Klabu hiyo.


Bashungwa amesema FCC na Simba watakutana kwa mara ya tatu Jumatatu ijayo ambapo Serikali inaamini utakuwa mwisho wa mvutano wa kiuwekezaji ndani ya klabu hiyo.


Spika Ndugai akilizungumzia suala hilo, amesema ni vema jambo hilo limalizwe haraka kwani haiwezekani klabu kubwa inayojiandaa hatua ya nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika kukwamishwa kwa jambo dogo ambalo limechukua miaka mingi.


MWISHO

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com