METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, March 1, 2023

TPHPA IMETOA MAFUNZO KWA WAKULIMA, MAOFISA UGANI NA WAUZAJI WA VIUATILIFU 215 ILI KULINDA AFYA YA WALAJI, WANYAMA NA MAZINGIRA

Na Saida Issa,DODOMA

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viwatilifu Tanzania (TPHPA) imetoa mafunzo kwa wakulima, Maofisa ugani na wauzaji wa viuatilifu 215 ili kulinda afya ya walaji, wanyama na mazingira.

Hayo yalibainishwa jijini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA Profesa. Joseph Ndunguru wakati akizungumza na wandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu wa mamlaka hiyo katika mwaka huu wa fedha.

“Mamlaka imetoa mafunzo kwa wakulima, Maofisa ugani na Wauzaji wa Viuatilifu wapatao 215 kutoka maeneo mbalimbali nchini ili kulinda afya ya walaji, wanyama na mazingira na kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakuwa na ubora unaotakiwa,”amesema

Profesa Ndunguru amesema TPHPA  imeendelea kuwajengea uwezo wakaguzi wa mimea na mazao waliopo katika mipaka ya nchi za  jumuia ya Afrika mashariki kwa njia ya mafunzo.

Amesema  wakaguzi 72 walipatiwa mafunzo ya afya ya mimea kutoka vituo vya Rusumo, Kabanga, Mutukula, Mrusagamba, Kibirizi, Mabamba, Manyovu, Bukoba port, Mwanza Port, Sirari, Holili, Tarakea na Namanga, Tanga port, Horohoro, Dares Salaam port, Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere, Mtwara port, Uwanja wa ndege wa Songwe, Tunduma, Kasumulo na Mtambaswala.

“Ili kudhibiti mlipuko wa viwavijeshi vamizi tumesambaza lita 81,563 za Profenofos  katika halmashauri 57 za mikoa ya Lindi, Pwani, Morogoro, Tanga, Geita, Manyara, Kilimanjaro, Dodoma, Singida, Dar es salaam, Katavi na Arusha kwa ajili ya kudhibiti uharibifu unaotokana na viwavijeshi katika mazao ya nafaka,

Tumesambaza  lita 561 za Chlorpyrifos na Cypermethrin  katika halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro,"amesema.

Katika hatua nyingine amesema katika kubabiliana na viwavijeshi wametoa mafunzo kwa  wakulima 2987 na maofisa ugani 16 katika Kata 16 za halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.

Amesema mafunzo hayo ni ya kuongeza ujuzi kuhusu  mbinu za kudhibiti nzi wa matunda kwa wakulima 849 na maofisa ugani saba  katika Wilaya ya Handeni.

Kuhusu udhibiti wa Nzige Profesa Nduguru amesema warishirikiana  na shirika la kimataifa la kudhibiti nzige wekundu (IRLCO-CSA) kufanya  ufuatiliaji kwenye mazalia ya asili ya nzige wekundu.

Amefafanua kuwa  hekta 195,150 zilifanyiwa ufuatiliaji kwa njia ya anga kwa kutumia helikopita na kubaini hekta 1,000 zilizokuwa na kiwango kikubwa cha nzige

“Unyunyiziaji wa kiuatilifu aina ya fenitrothion kiasi cha lita 450 zilitumika kudhibiti nzige wekundu katika hifadhi ya Katavi ambapo ni mazalia yake ya asili,”amesema.

Profesa Nduguru amesema TPHPA itaendelea kuwajengea uwezo wataalamu wa mamlaka katika kusimamia na kudhibiti milipuko ya visumbufu kwa wakati.

“Tutaendelea kutumia “DNA technology” katika kutambua aina za wadudu na magonjwa ya mazao ili kuwa na udhibiti endelevu,”ameeleza.

mwisho
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com