Na Saida Issa, Dodoma
MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa mazingira Mjini Dodoma(Duwasa) imeeleza kuwa uzalishaji wa maji katika jiji la Dodoma umeongezeka kutoka lita Milioni 61.5 na kufika 67.1 kwa siku.
Hayo aliyaeleza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (Duwasa), Mhandisi Aron Joseph jana jijini hapa wakati akizungumzia mafanikio ya miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan madarakani na mipango ya kuboresha huduma ya maji.
Alisema katika wilaya ya Chamwino upatikanaji wa maji umeongezeka kutoka asilimia 42 mpaka 87, Kongwa umeongezeka kutoka asilimia 44 hadi 88 na Bahi asilimia 37 hadi 95.
"Kuhusu maji taka alisema serikali imetenga kiasi cha sh Bilioni 4.9 kwa ajili ya kukarabati mtandao wa majitaka eneo la Area D na C ambapo chemba 1,005 zitajengwa na kubadili kilomita 19 za mtandao chakavu,
Serikali imetenga kiasi cha sh Bilioni 23.8 ili kupunguza adha ya maji kwa kuchimba visima maeneo ya Nzuguni, Bihawana na Zuzu,"alisema.
Aidha alisema katika eneo la Nzuguni kiasi cha sh Bilioni 5.8 kimetengwa kwa ajili ya kuongeza uzalishaji kwa asilimia 11.3, Zuzu-Nala sh Bilioni 7.8 zimetengwa ili kuongeza uzalishaji kwa asilimia 10.
"Bihawana sh Bilioni 10.2 zimetengwa kuongeza uzalishaji kwa asilimia 15.2, Kongwa sh Milioni 68 ili kuongeza uwezo wa chemchem na Chamwino mradi wa miji 28,
Kuhusu miradi wa ujenzi wa uboreshaji wa huduma za majitaka jijini Dodoma, alisema utagharimu Dola Milioni 70, utajenga mabwawa mapya 16 na utaratibu majitaka lita Milioni 20 kwa siku,"alisema.
Pia, kutakuwa na mtandao wa mabomba kilomita 250, kuunganisha wateja wapya 6,000 na kwamba tathimini ya kumpata Mhandisi mshauri imekamilika Oktoba mwaka jana na imetumwa Korea kwa ajili ya kibali.
Alifafanua kuwa kwa sasa jiji la Dodoma lina wakazi 765,179 kwa mujibu wa sensa yam waka 2022 ambao takribani asilimia 91 wanapata huduma ya majisafi na salama kwa mgao na asilimia 20 huduma ya uondoshaji majitaja.
Alieleza mahitaji maji kwa sasa ni lita 133,400,000 kwa siku na yataongezeka hadi lita 417,308,000 kwa siku ifikapo mwaka 2051.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Resemary Senyamule alisema uzalishaji maji katika kipindi cha miaka miwili ya Rais Samia upotevu wa maji umepungua kutoka asilimia 39.1 hadi asilimia 83.
Aidha, alisema maduhuli yameongezeka kutoka kiasi cha sh Bilioni 1.6 hadi sh Bilioni 2.3 huku upatikanaji wa maji ukiongezeka kutoka asilimia 61.5 hadi asilimia 67.8.
0 comments:
Post a Comment