METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, March 7, 2023

TASAC KUENDELEA KUTEKELEZA MRADI WA KIMATAIFA WA MLVMCT


Na Saida Issa,Dodoma

SERIKALI ya Awamu ya Sita kupitia TASAC inaendelea kukamilisha Mradi wa Kimataifa wa Mawasiliano na Uchukuzi katika Ziwa Victoria (Multi-National Lake Victoria Maritime Communication and Transport  MLVMCT) lengo kukuza uwekezaji katika shughuli za usafiri majini na uvuvi. 

Hayo yameelezwa Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la uwakala wa meli Tanzania (TASAC) Kaimu Abdi Mkenyenge alipokuwa akieleza utekelezaji wa majukumu ya Shirika hilo.

 Alisema kuwa pamoja na mambo mengine ni kujenga vituo vinne (4)  vya uokozi (search and rescue centres-(SARs)) ambavyo vitakuwa kimoja kimoja katika maeneo ya Kanyala  Sengerema, Musoma - Mara, Nansio - Ukerewe na Ilemela  Mwanza Ili  visaidiae katika kushughulikia changamoto za usafiri kwa njia maji, kuimarisha usalama wa vyombo vya usafiri kwa njia maji na kuongeza fursa za kiuchumi kwa jamii zinazoishi kandokando ya Ziwa Victoria. 


"Mradi huu unaotekelezwa na nchi za Tanzania na Uganda umepangwa kugharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 59.23 ambapo upande wa Tanzania gharama za mradi ni Shilingi Bilioni 19.97 zinazojumuisha gharama za kazi za ndani na sehemu ya mchango wa Tanzania katika kugharamia kazi za kikanda zinazofanywa kwa kushirikiana na Uganda,

Mradi huu unatarajiwa kukamilika mnano mwezi Desemba, 2024 na tayari Mshauri Elekezi ameshakabidhiwa maeneo ya kufanyia kazi,"alisema.

Kadhalika alisema kuwa Uendelezaji na Uimarishaji wa Miundombinu ya Mifumo ya TEHAMA ambapo TASAC inatekeleza miongozo inayotolewa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) katika kuhakikisha manunuzi, matumizi bora, sahihi na salama ya vifaa na mifumo yote ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Serikalini. 

"Katika kutekeleza hili, Shirika limeunganisha ofisi zake zote zikiwemo zile za Mikoa, Wilaya na mipaka kwenye Mkongo wa Taifa ambao umerahisisha na kuharakisha mawasiliano ya ndani (Intranet), barua pepe, na mawasiliano na wadau wa nje (Internet),

Uendelezaji miundombinu na mifumo ya TEHAMA ulianza mwaka wa fedha 2018/19 na utakamilika mwaka wa fedha 2025/26,"alieleza. 

Alisema Mbali na Mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho lakini pia kuna fursa mbalimbali katika Sekta ya Usafiri Majini ambazo zinaweza kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi kama vile kuanzisha utaratibu wa kusajili meli kwa masharti nafuu (open registry), kuanzisha maeneo ya ukarabati na ujenzi wa meli katika ukanda wa pwani; kuanzisha maegesho ya boti ndogo katika ukanda wa pwani, kuanzisha viwanda vya utengenezaji malighafi za ujenzi wa boti za plastiki (fibre) pamoja na kujenga bandari rasmi za uvuvi. 

TASAC ilianzishwa chini ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania, Sura 415 na kuanza rasmi kutekeleza majukumu yake tarehe 23 Februari, 2018,Kuundwa kwa TASAC ni hatua ya kisera ya Serikali, kwa upande wa Tanzania Bara, inayokusudia kukuza sekta za usafiri majini, kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma hususan kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa kuinua mchango wa usafiri kwa njia ya maji. 

Hii ni kwa sababu Tanzania ina ukanda mkubwa wa Bahari ya Hindi wenye urefu takriban Kilomita 1,424, Maziwa makubwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa; hivyo kuwepo kwa fursa kubwa ya kukuza uchumi wa nchi yetu hasa wa rasilimali za maji (Blue Economy) kupitia sekta hii ya usafiri majini.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com