Watendaji
mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la umeme Tanzania pamoja na
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania, wakiwa kwenye mafunzo ya kuwajengea
uelewa sawa wa wajumbe wapya wa kamati ya Nishati na Madini na kuwaongezea
uelewa wale waliokuwepo katika kamati hiyo, katika sekta ya Umeme, Mafuta na
Gesi.
Na Godfrey Mwemezi, Dodoma
Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Nishati na Madini imepongeza uongozi wa Shirika la Umeme nchini
(TANESCO) kwa jitihada zake za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme
nchini.
Mwenyekiti wa
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula ametoa
pongezi hizo Jijini Dodoma wakati Kamati hiyo ilipokuwa katika semina ya
kujengewa uwezo katika masuala ya umeme, mafuta na gesi, Machi 25 hadi 26,
2023.
‘’Sisi Kamati ya kudumu ya Bunge ya
Nishati na Madini tunaipongeza Wizara ya Nishati na Shirika la umeme Tanzania
kwa juhudi wanazofanya katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme
nchini, jambo ambalo linaongeza ukuaji wa uchumi wa Taifa letu kwa kasi,” amesema Kitandula.
Akizungumza na
wajumbe wa Kamati hiyo, Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato amesema
kuwa lengo la semina hiyo ilikuwa ni kutoa uelewa sawa kwa wajumbe wapya na
kuwaongezea uelewa wale waliokuwepo katika kamati hiyo.
Amesema semina
hiyo imeandaliwa na Wizara ya Nishati kupitia TANESCO pamoja na Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ili kuendelea kuwaimarisha wajumbe wa
kamati hiyo kwa kuwa ndio wanaoishauri serikali katika sekta ya umeme, mafuta
na gesi.
Wakati akifunga
semina hiyo, Kitandula ameipongeza Wizara na taasisi hizo mbili kwa kuandaa
mafunzo hayo yaliyokuwa na lengo la kuwajengea uelewa wajumbe wa kamati hiyo ya
Bunge.
Baadhi ya
waliohudhuria semina hiyo ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athumani
Selemani Mbuttuka, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Maharage Chande, Mkurugenzi
wa TPDC, Mussa Makame pamoja na watendaji wengine wa Wizara na taasisi hizo.
0 comments:
Post a Comment