METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, March 16, 2023

KAMPUNI YA MBOLEA YA MINJINGU YATOA UFAFANUZI KUHUSU TUHUMA ZA KUHIFADHIWA MCHANGA KWENYE MIFUKO YA MBOLEA NJOMBE

  


TAARIFA  KWA UMMA

Uongozi wa Kampuni ya  uzalishaji, usambazaji na uuzaji  wa mbolea Minjingu Mines and Fertiliser Limited (MMFL) unapenda kutoa ufafanuzi wa tuhuma zilizoelekezwa kwenye Kampuni katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii. Tuhuma hizo zilihusu upatikanaji wa mifuko 776 ya mchanga kwenye ghala letu lilloko mjini Njombe. Maelezo yetu ni kama haya yafuatayo:

Kwamba: kampuni ya MMFL ambayo ni kampuni ya uzalishaji wa mbolea aina mbali mbali ni ya Kitanzania iliyojijengea heshima ya uzalishaji na usambazaji wa mbolea ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha miaka 22. Tunautaarifu umma kwamba hatujawahi kuhujumu wakulima au wadau wa kilimo kwa kuzalisha na au kufungasha mchanga/udongo katika mifuko yake kama mbadala wa mbolea. Aidha kampuni imeendelea kuwa na ushirikiano wa karibu na Serikali katika kuhakikisha kwamba wakulima wanapata mbolea ya ruzuku kwa wakati na kwa bei nafuu.

Kwamba: Afisa Mauzo wa MMFL kituo cha Njombe -Bwana Gervas John Mtitu alipatikana na upotevu wa mbolea jambo ambalo alilikiri. Baada ya upotevu huo, Bwana Gervas John Mtitu aliendelea kutoonyesha ushirikiano licha ya jitihada mbali mbali za kumtafuta.

Kwamba: baada ya kutoendelea kupata ushirikiano kutoka kwa Bwana Gervas John Mtitu, tarehe 28/1/2023, Kampuni ilitoa  taarifa Kituo cha Polisi Njombe mjini kuhusiana na upotevu wa mbolea  na kutoonekana kazini ambapo tulipatiwa RB No. NJ/RB/390/2023.

Kwamba: tarehe 20/2/2023, Polisi walifika kwenye ghala  na kumweleza Afisa Masoko wa MMFL kwamba walifika kufanya ukaguzi  baada ya kupata taarifa kwamba kulikuwa na baadhi ya mifuko ambayo haikuwa na mbolea bali bidhaa nyingine. Katika ukaguzi huo, walibaini kwamba kwenye ile mifuko ya zamani (ambayo iliachwa na Bwana Gervas John Mtitu) , kulikuwa na mifuko yenye mchanga. Afisa Masoko wa Kampuni alichukuliwa na Polisi na ghala kufungwa na kuwa chini ya ulinzi wa Polisi.

Kwamba: tarehe 23/2/2023, maafisa wa TFRA kutoka Kanda ya Mbeya walifika  na baada ya hapo, maafisa wa TFRA, Polisi na maafisa kutoka MMFL walifika kwenye ghala na baada ya uchunguzi, walibaini kuwepo na mifuko 776 ya mchanga ikiwa kwenye mifuko ya zamani ya mbolea ya Minjingu. Ili mifuko hiyo ya mchanga kutoonekana kiurahisi, mifuko ya mbolea halisi (ile ya zamani) ilizungushwa pande zote ili ionekane kwamba yote ilikuwa mbolea.

Kwamba: TFRA  waliiandikia MMFL barua  tarehe 24/2/2023 ambapo  maudhui ya barua ilikuwa ni kukutwa na bidhaa ambayo siyo mbolea na Kampuni ilipigwa faini ya shilingi milioni 30. Kampuni ililipa faini hiyo tarehe 25/2/2023.

Kwamba: MMFL imesikitishwa suala hilo (ambalo Mamlaka inayohusika Kisheria ilishalitolea maamuzi) kuletwa tena tarehe 5 Machi 2023 kwenye jamii na kuleta sintofahamu kwa jamii. 

Kwamba: katika jitihada za kuhakikisha wakulima wanapata mbolea kulingana na uhitaji wa virutubisho wa zao, MMFL imekuwa ikishirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) na kutokana na jitihada hizo, Kampuni imeweza kuzalisha mbolea maalum kwa ajili ya mazao ya chai, kahawa, tumbaku, pamba na mazao ya chakula.Tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na Taasisi za Utafiti ili mazao mengi zaidi yaweze kuwa na mbolea zinazokidhi mahitaji ili kuongeza tija.

Kwamba: kutokana na ubora wa mbolea zetu, Kampuni imekuwa ikiuza mbolea zake Kenya, Burundi, Rwanda na Uganda na hakujawahi kuwa na malalamiko yanayohusiana na ubora wa mbolea na mahitaji kwenye nchi hizo yamekuwa yakiongezeka.


Hivyo: 

· Tunawahakikishia wakulima wote wa Tanzania kwamba Kampuni ya MMFL itaendelea kuwapatia             wakulima mbolea zenye ubora.

· Tuko tayari kushirikiana na vyombo vya dola katika kuhakikisha kwamba mtuhumiwa anapatikana             na kupelekwa kwenye vyombo vya sheria.

· Kampuni inaamini kwamba mhusika atakapopatikana, atasaidia kutoa taarifa ambazo zitasaidia kujua         kama haya yaliyojitokeza ni jitihada za yeye peke yake au kuna hujuma ili kuidhoofisha kampuni ya         MMFL.

Tunamhakikishia Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – DKt Suluhu Samia Hassan na Serikali yote kwamba Kampuni ya MMFL itaendelea kuwahudumia wakulima wa Tanzania na wa nchi ambazo wanatumia bidhaa zetu kwa kuwapatia mbolea zilizo na ubora.


Imetolewa na :- 

Kurugenzi ya Mawasiliano

Minjingu Mines & Fertiliser LTD

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com