Na Lucas Raphael,Tabora
Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Mkoani Tabora (WETCU 2018 LTD) wamepitisha mapendekezo ya bajeti ya mapato na matumizi ya sh bil 1.833 kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Akiwasilisha bajeti hiyo kwa niaba ya Meneja Mkuu wa Chama hicho Samwel Jokeya, Meneja Shughuli na Vifaa Lazaro Busagwe alisema mapendekezo hayo yamelenga kuimarisha Ushirika na kuboresha shughuli za wakulima.
Alifafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 wanatarajia kukusanya mapato ya jumla ya sh bil 1.83 kutoka katika vyanzo vyao mbalimbali ikiwemo ushuru wa tumbaku ambao utawaingizia kiasi cha sh mil 697.4.
Vyanzo vingine ni gawio la faida kutokana na uwezekezaji wa WETCU katika benki ya CRDB wa hisa mil 24 ambapo wanatarajia kupata kiasi cha sh mil 864 na gawio la faida kutoka benki ya EXIM kiasi cha sh mil 8.
Aliongeza kuwa watapokea mapato ya sh mil 164.6 yatokanayo na tengo la usimamizi wa pembejeo, sh mil 43 za pango la kiwanja, nyumba, ofisi na maghala na sh mil 56.4 za mizani (digital scale) zilizouzwa kwa vyama wanachama malipo.
Busagwe alibainisha kuwa kati ya fedha hizo sh bil 1.79 zitatumika kwa shughuli mbalimbali, ambapo sh mil 263.3 zitahudumia wanachama (wakulima), mil 393.7 utumishi, mil 975.8 uendeshaji na utawala, mil 124.1 uendeshaji biashara, mil 13, gharama za kibenki na matumizi ya dharura mil 20 huku ziada ikiwa sh mil 30.
Aidha alibainisha kuwa wanatarajia kukusanya jumla ya sh mil 751.5 kutokana na ushuru wa kilo mil 21 za tumbaku zitakazouzwa na wakulima ambapo kila kilo itatozwa sh 35.79 na fedha hizo zitatumika kwa shughuli za maendeleo.
Alitaja shughuli zitakazofanyika kuwa ni pamoja na ununuzi wa gari mpya aina ya Toyota Land cruiser Hard top itakayonunuliwa kwa sh mil 250 na ununuzi wa trekta aina ya new holand (HP 90) sh mil 16 ambazo ni malipo ya awali.
Alisema kwamba matumizi mengine ni malipo ya sh mil 207 ya sehemu ya deni la CRDB la dola za kimarekani 90, 000, malipo ya deni la Mpigwa AMCOS awamu ya I sh mil 28.5, deni la Bytrade awamu ya II sh mil 184.1, Ikonongo AMCOS sh .mil 11.5, deni la ATT LTD sh mil 29.06 na deni la Mtazamo AMCOS awamu ya II sh mil 25.3.
0 comments:
Post a Comment