Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu kanali Jimmy Matamwe akizungumza na wajumbe walioshiriki warsha ya kupunguza madhara ya maafa nchini (hawapo pichani) wakati wa kufunga warsha hiyo Februari 1, 2019 iliyofanyika Ukumbi wa Mazengo Dodoma Hotel.
Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa
Shughuli za Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu kanali Jimmy Matamwe akimkabidhi cheti
cha ushiriki Bw. Bashiru Taratibu ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara hiyo
anayeshughulikia Mipango na Tafiti wakati wa kufunga Warsha yakupunguza madhara ya maafa
nchini iliyofanyika Jijini Dodoma.
NA MWANDISHI WETU
Serikali imedhamiria kuendelea
kuchukua hatua za upunguzaji wa athari za maafa kwa kuwa ni moja ya eneo
lililopewa kipaumbele katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka wa Mitano,
2016/17- 2020/21.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa
Idara ya Uratibu wa Shughuli za Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu kanali Jimmy Matamwe
alipokuwa akifunga warsha ya kupunguza madhara ya maafa nchini na kuimarisha uthabiti kwa
nchi na jamii dhidi ya majanga ya asili katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la
Sahara Februari 1, 2019 Jijini Dodoma.
Ameeleza kuwa,
hatua hiyo ni muhimu katika mkakati wa upunguzaji wa madhara yatokanayo na
maafa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa malengo
ya msingi ya Mfumo wa Sendai wa Kupunguza Madhara ya Maafa wa mwaka 2015 – 2030
sambamba na malengo endelevu ya mwaka 2030 na makubaliano ya Paris juu ya
mabadiliko ya tabianchi.
“imeelezwa kuwa mmepata fursa ya
kuandaa mkakati wa kupunguza madhara mafuriko na ukame kwa kutumia
taarifa ya muhtasari wa vihatarishi mlioujadili na hii imetoa fursa ya
kujiamini katika kusimamia na kutatua majanga haya ambayo yamekuwa yakiikumba
nchi mara kwa mara na kusababisha hasara kubwa za kiuchumi na kuongeza wigo wa
umasikini nchini”,alisema Kanali Matamwe
Katika kuhakikisha mipango hiyo
inakuwa endelevu Kanali Matamwe alitoa rai kwa washiriki wa warsha hiyo
kuainisha maeneo yanayohusu sekta zao na kuyafanyia kazi katika mipango ya
bajeti na kuendelea kuongeza nguvu kwa kutenga bajeti ya kutosha katika masula
ya kukabiliana na majanga.
“Tukumbuke uwekezaji katika kupunguza
madhara ya maafa ni hatua muhimu katika kupunguza matumizi ya fedha nyingi kwa
ajili ya kukabiliana na madhara ya yanayoweza kutokea”,alisisitiza Kanali
Matamwe
Serikali kwa kuzingatia Sheria ya
Usimamizi wa Maafa Na.7 ya mwaka 2015 na kanuni za usimamizi wa maafa za mwaka
2017 zimeanzisha Kamati za Usimamizi wa maafa ngazi ya Mkoa hadi Kijiji kwa
lengo la kupunguza madhara ya maafa ili kuwa na jamii stahimilivu.
Kwa upande wake mshiriki wa warsha
hiyo Bw. John Kiriwai alieleza kuwa, kuna umuhimu wa kuwekeza nguvu na fedha
katika masuala ya maafa kulingana na takwimu na taarifa zinazoeleza umuhimu wa
kuwa na mikakati madhubuti ili kuwa mipango endelevu katika kukabili maafa.
“Ni wakati sasa kuendelea kutumia
fursa zilizopo kwa kuwekeza kwa kiwango kikubwa na kutumia taarifa za watafiti
mbalimbali na kuziweka katika mipango yetu ya maendeleo ili kupunguza athari za
maafa,”alisema Kiriwai.
Naye Mwakilishi kutoka Wakala wa
Barabara Bi.Zaharani Madai alieleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali hawana budi kuendelea kuwa na jitihada za makusudi za kuimarisha
miundombinu kwa kuzingatia mazingira yaliyopo kwa kutumia wataalam katika
kujenga na kuimarisha maeneo yanayodhaniwa kuwa hatarishi pindi maafa
yanapotokea.
“Ni wakati sasa wa kujijenga upya ili
kuwa na mikakati inayotekelezeka katika kutatua na kukabili maafa kwa
kuimarisha miundombinu tuliyonayo ili kuendana na mazingira ya kukabili maafa
nchini,”alisisitiza Madai.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment