Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa na waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) amewaagiza jumuiya ya wazazi mkoani Kagera kutimiza wajibu wao uliosababisha jumuiya hiyo kuanzishwa kwa kusimamia maadili na mienendo ya vijana.
Bashungwa ameyasema hayo kwenye hafla ya maadhimisho ya kutimiza miaka 46 ya kuzaliwa CCM iliyofanyika Kimkoa wilayani Karagwe chini ya Jumuiya ya wazazi Mkoa wa Kagera, ambapo amesema kuwa maadili kwa vijana yameporomoka sana hivyo jumuiya ya wazazi inatakiwa kutimiza wajibu wake.
Ameongeza kuwa kumekuwepo na kukithiri kwa matendo ya ukatili katika jamii sambamba na matukio ya matumizi ya madawa ya kulevya kwa vijana hali inayopunguza nguvu kazi ya taifa.
“Lengo la kuanzishwa jumuiya hii moja wapo ni kusimamia malezi na maadili ya vijana, hivyo tunapoona maadili kwa vijana wetu yanamomonyoka tunarudi na kujiuliza uwepo wa jumuiya hii na utekelezaji wa majukumu yao, niwaombe hebu tuamke tutimize wajibu wetu ili kukiokoa kizazi chetu.” Ameeleza Bashungwa.
Sambamba na hayo Bashungwa ameitaka Jumuiya jumuiya hiyo kutokuwa wanyonge wanapo simamia utekellezaji wa ilani ya CCM kwakuwa wao pia ni sehemu ya chama hicho na kuwataka kuendelea kusimamia miradi wanayoianzisha kwa masilahi mapana ya chama chao.
Awali mwenyekiti wa jumuiya hiyo mkoa wa Kagera Alphonsina Barongo amemshukuru Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miradi mingi ambayo anaeitekeleza mkoani Kagera kwa kuwa wao kama wazazi wanaridhishwa na kazi zake.
Barongo amesema kuwa jumuiya imejipanga kuweka wawakilishi kwenye maeneo mbalimbali kama bunge na baraza la madiwani ili kuweza kushiriki vikao hivyo ambavyo vitaweza kujadili uwepo wa mmomonyoko wa maadili kwa vijana na jamii kwa ujumla.
Ameongeza kuwa Jumuiya ya wazazi Mkoa wa Kagera imejipanga kuhakikisha miradi yote ambayo ipo chini ya jumuiya hiyo inasimamiwa vyema na kuleta matunda yaliyokusudiwa, huku akiahidi kuboresha hali ya jumuiya hiyo ndani ya mkoa.
Katika kuadhimisha sherehe za kuzaliwa miaka 46 ya kuzaliiwa CCM, Jumuia ya wazazi mkoa wa Kagera umepanda miti katika hospitali ya wilaya Karagwe sambamba na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba ya katibu wa jumuiya hiyo ya wilaya Karagwe katika kata ya Ihanda.
0 comments:
Post a Comment