METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, December 31, 2025

DKT. NATU APONGEZA UBUNIFU NA UBORA WA JARIDA LA HAZINA YETU

 

Na. Joseph Mahumi, WF, Dar es Salaam

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, amepongeza ubunifu na ubora wa Jarida la Hazina Yetu Toleo la Tano ambalo limeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha Wizara ya Fedha.

Ametoa pongezi hizo wakati akipokea Jarida hilo kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Bw. Benny Mwaipaja, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam.

Dkt. Mwamba alisema Jarida hilo ambalo limeendela kuwa bora na kufika kila mahali duniani kwa njia ya kidigitali ni nyenzo muhimu katika kuwasilisha taarifa sahihi, za wazi na kwa lugha inayoeleweka kuhusu shughuli, mafanikio na mipango ya Wizara ya Fedha.

Dkt. Mwamba alipongeza jitihada za Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kwa kuendelea kuboresha mawasiliano na uelimishaji kwa umma pamoja na ubunifu na weledi unaooneshwa katika uandaaji wa Jarida hilo, akibainisha kuwa limeendelea kuwa chombo muhimu cha kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi katika masuala ya fedha na uchumi wa Taifa.

Kwa upande wake, Bw. Benny Mwaipaja alisema kuwa Jarida la Hazina Yetu linalenga kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Fedha pamoja na mchango wake katika maendeleo ya Taifa, akiahidi kuendelea kuliboresha ili liwe chombo chenye tija zaidi katika mawasiliano ya serikali.

Jarida la “Hazina Yetu Toleo la Tano” limesheheni maarifa mbalimbali kupitia Makala bora kabisa, habari, matukio ya picha na matangazo mbalimbali na linapatikana kwa njia ya nakala ngumu (hard copies) na nakala tete (soft copies) kupitia mitandao ya kijamii ya Wizara na wadau wengine wa habari pamoja na Tovuti ya Wizara ya Fedha www.mof.go.tz 


Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com