METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, January 28, 2023

JAMII YAHIMIZWA KUMZINGATIA MTOTO TANGU AKIWA TUMBONI MWA MAMA

Na Joyce Kasiki,Dodoma

MKURUGENZI Idara ya Maendeleo ya Mtoto,Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wanawake na Makundi Maalum Sebastian Kitiku ameihimiza jamii kumzingatia mtoto tangu akiwa tumboni kwa mama kwa kuhakikisha mama mjamzito anapata lishe pamoja na afya bora ili kumlinda mtoto aliye tumboni asidhurike kwa namna yoyote ile. 

Kitiku ameyasema jijini Dodoma katika shule ya Msingi Chisichili wakati Jumuiya ya wanafunzi wanaosoma shahada ya kwanza ya elimu katika fani ya Elimu Awali (UECESA) kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) walipotembelea shule hiyo ili kuelimisha wazazi kuhusu umuhimu wa Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kwa watoto wenye umri wa miaka 0-8.

“Lishe na afya bora vina umuhimu mkubwa katika kumlinda mtoto lakini katika kukuza ubongo wa mtoto tangu akiwa tumboni kwa mama yake,lakini baada ya kuzaliwa mtoto anahitaji uchangamshi,malezi yenye muitikio ,anapaswa kulindwa dhidi ya ukatili ili asiathiriwe ubongo wake .”amaesema na kuongeza kuwa

“Ukatili kwa mtoto mwenye umri chini ya miaka minane una athari kubwa kwatika ukuaji wa ubongo wake ,ndiyo maana tunasema hata katika maeneo ya shule na maeneo mengine tupunguze viboko na vipigo kwa watoto hawa.”

Programu Jumuishi ya Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto 2021/22-2025/26,inalenga kuharakisha upatikanaji wa matokeo chanya ya maendeleo ya awali ya mtoto kwa kuboresha mfumo shirikishi wa kisekta katika malezi jumuishi ya watoto.

Kwa mujibu wa Programu hiyo,inalenga kutoa elimu kwa jamii ili iweze kumlea mtoto kwa kuzingatia vipengele muhimu vitano ambavyo ni Afya bora,Lishe ya kutosha,malezi yenye mwitikio,ujifunzaji wa awali na Ulinzi na usalama wa mtoto na kwamba kwa kuzingatia hayo yote mtoto atakua vizuri na kufikia utimilifu wake na kuwa mwenye tija kwa Taifa hasa katika kutafakari na kuamua mambo mbalimbali.

Kwa upande wake Mlezi wa wanafunzi hao Dkt.Ignasia Mligo kutoka UDOM amesema vijana hao kutoka UDOM wanaandaliwa kwa ajili ya kuwalea watoto wadogo katika shue za msingi na vituo vya kulea watoto.

“Kwa hiyo tumekuja kuhamasisha wazazi na walezi mjue umuhimu wa elimu kwa watoto wetu wadogo,mjue umuhimu wa malezi ,makuzi na maendeleo ya awali ya watoto wetu hawa wadogo.”amesema

Kwa mujibu wa Dkt.Mligo ni kuona wazazi wanatimiza wajibu wa kuwalea watoto na kuwazingatia katika kuwapatia mahitaji muhimu hasa katika kipindi cha umri wa miaka 0-8 ili aweze kujifunza vizuri.

Amesema katika kipindi hicho mtoto anahitaji lishe bora,ulinzi na usalama ,malezi yenye muitikio(kumpenda mtoto na kuwa naye karibu ),kutimiza jukumu la ujifunzaji wa awali wa mtoto tangu anazaliwa.

“Kwa hiyo nina furaha sana wazazi mtaondoka na ujumbe na hamtawafungia watoto nyumbani ,watoto wanatakiwa waje shule wacheze na wenzao ,wafurahi,na ili uandikishaji upande mzazi una jukumu la kumleta mtoto shule ,ile kucheza na wenzake ndiyo kujifunza kwenyewe hata kama hajaandika .”amesisitiza

Awali Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Apollo Ihonde amesema katika shule hiyo wanafunzi 49 tu ndiyo wameandikishwa mwaka huu huku akisema idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na ukubwa wa kijiji hicho.

Amewaasa wazazi waendelee kujitokeza kuwaandikisha watoto ili wajifunze licha ya kuwa wana uhaba wa walimu ambapo amesema wapo walimu tisa na kwamba wanaoingia darasani ni walimu wanane na mmoja yupo masomoni .

Aidha, watoto wa miaka mitatu au minne wanaweza kujiunga na Elimu ya Awali katika mfumo rasmi iwapo walimu watawafanyia upimaji wa awali na kubaini kama wana utayari wa kujiunga katika ngazi hiyo ya elimu ambapo upimaji huo utazingatia uwezo wa kujitegemea,uwezo wa kujieleza na uwezo wa kufuata maelekezo rahisi.

Akisoma risala ya UECESA Zubeda Kigoda amesema,tangu kuzindiliwa kwa Programu ya Kitaifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto 2021,wao wamekuwa sehemu ya wadau wakubwa wanaoitekeleza kwa kufanya shughuli mbalimbali chuoni na kwenye jamii kwa ukubwa wake.

“Tayari tumeshatembelea shule za msingi za Ng’ong’ona,Makulu,Mapinduzi Mhande za wilaya ya Dodoma na shue ya msingi Zanka katika wilaya ya Bahi ambapo katika maeneo hayo yote hayo tumekuwa tukitoa elimu kuhusiana na Malezi ,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto,

“Na pia tumetoa afua stahiki kwa watoto kutokana na mazingira wanayoishi na kuwaelimisha wazazi umuhimu wa kuwalea watoto wao vizuri ili wafikie ukuaji timilifu na wenye tija kwa Taifa.

Kwa niaba ya wengine,mzazi aliyejitambulisha kwa jina la Yohana Chipali amesema elimu hiyo ni muhimu katika jamii kwani inatoa mwanga kwa wazazi na walezi katika kuwalea watoto ili wakue vizuri.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com