Na Mathias Canal,
WEST-Dar es salaam
Kuanzia sasa serikali itaanza kuzitazama ajira za vyuo vikuu
badala ya kuangalia ubora wa ufaulu yaani GPA pekee sasa waajiriwe kwa kupimwa
uwezo wao kwa kufanya usaili.
Kuangalia ufaulu pekee wa wanafunzi haitoshi kuboresha elimu
badala yake ni muhimu kuongeza vigezo hivyo katika mapitio ya sera na mabadili
ya mitaala jambo hilo litatazamwa kwa weledi mkubwa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof ADOLF MKENDA
ameyasema hayo leo tarehe 12 Disemba 2022 mbele ya mgeni rasmi Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt PHILIP MPANGO wakati wa mahafali ya
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania iliyofanyika Kinondoni Jijini Dar es salam.
Amesema wakati serikali inaongeza udahili wa wanafunzi haitakuwa
tayari kuona ubora unapungua hivyo serikali inaendelea na mkakati wake wa
kuhakikisha ubora wa elimu hususani katika vyuo vikuu unaimarika.
"Zamani ilikuwa rahisi kuwa Profesa ukiandika tu kwenye
magazeti unakuwa Profesa lakini kwa sasa vigezo vya kuwa Profesa vimezidi kuwa
vigumu kwa sababu tunataka maprofesa wetu wawe sawa na wale wa nchi
zingine" Amekaririwa Prof Mkenda
Amesema katika mageuzi ya elimu yanayokuja ambapo wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia ipo katika mapitio ya sera na mitaala miongoni mwa
mambo yatakayofanyiwa kazi itakuwa ni pamoja na kuhakikisha wanaoajiriwa ni
wanafunzi wenye sifa zinazotakiwa.
Pia, Waziri Mkenda amesema kuwa serikali kwa sasa inaendelea na
Ujenzi wa Kampasi mpya za Vyuo Vikuu katika mikoa 14 Tanzania pamoja na upande
wa Zanzibar (Unguja na Pemba) katika maeneo ambayo hayana vyuo vikuu ukiacha
vyuo huria.
Mikoa hiyo ambayo inatarajiwa kuwa na kampasi za vyuo vikuu
mbalimbali hapa nchini ni pamoja na Tabora, Katavi, Kigoma, Kagera, Singida,
Manyara, Lindi, Rukwa, Mwanza, Simiyu, Tanga, Ruvuma, Shinyanga na Dodoma.
Kadhalika, Waziri Mkenda amesema kuwa hapa nchini karibu kila
mkoa una kampasi ya chuo kikuu huria cha Tanzania hivyo ametoa rai kwa
watanzania wengi kuitumia fursa hiyo.
Kuhusu mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, Waziri Mkenda
amesema kuwa serikali imejipanga kuongeza bajeti ya mikopo kwa wanafunzi lakini
mikopo yote itatolewa kwa haki na vigezo vilivyowekwa.
"Hakuna kitu kibaya kama kuachia madaraka makubwa kwamba
aniletee kimemo mimi nimuangalie mtoto fulani ndio nimsaidie kupata mkopo
wakati muhusika mwenyewe anaweza akamsomesha mwanae, wakati mkopo wenyewe
hautoshi, mimi ningependa tuwape wenye mahitaji makubwa zaidi"
"Mtu yeyote anayefanya kosa la kumnyima yatima fursa ya
kusoma kwa sababu tu ya kujipendekeza kumpa mtoto wa fulani mkopo huyo nadhani
atalaaniwa vilevile" Ameseisitiza Waziri Mkenda
Waziri huyo wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf
Mkenda amemuhakikishia mgeni rasmi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe Dkt PHILIP MPANGO kuwa ataendelea kusimamia utoaji wa mikopo bila
kutetereka ili kuwe na uwazi na utoaji wa mikopo kwa haki.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment