METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, November 18, 2022

RAIS SAMIA ANATHAMINI MCHANGO WA WALIMU KATIKA SEKTA YA ELIMU - WAZIRI BASHUNGWA

Na Mwandishi Wetu, Karagwe - Kagera

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Mhe. Innocent Bashungwa amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan anathamini Mchango wa Walimu katika kuendeleza Sekta ya Elimu nchini.

Ameyasema hayo leo tarehe 18 Novemba 2022 wakati akifungua Mkutano wa Umoja wa Walimu Wakuu wa shule za msingi ndani ya wilaya ya Karagwe (TAPSHA), Mkoani Kagera.

“Kwa muda ambao nimehudumu katika maeneo mbalimbali kumsaidia Mheshimiwa Rais Samia, nimeona anavyothamini Mchango wa Walimu katika kuendeleza sekta ya elimu nchini” Amesema Waziri Bashungwa.

Waziri Bashungwa amesema Serikali inaendelea kuweka Mazingira wezeshi ya ujifunzaji kwa wanafunzi na ufundishaji kwa Walimu ikiwa ni pamoja na kuangazia mahaitaji ya Walimu na miundombinu katika vituo vyao vya kazi.

Amesema katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23, Mheshiwa Rais ameiwezesha Serikali kutenga fedha za kujenga nyumba za Walimu kwa kuanzia katika maeneo ambayo miundombinu sio rafiki kijografia ambapo utaratibu huo utaendelea kila mwaka.

Aidha, Waziri Bashungwa amewahakikishiwa Walimu hao, kuwa atafikisha risala na maombi yao kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Angellah Kairuki ambayo yanaelezea umuhimu na dhamira ya kuendeleza Umoja wao wa TAPSHA ambapo yeye ndiye Mlezi wao.

Vile vile, Bashungwa amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kupeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika wilaya Karagwe, ikiwa ni pamoja na Ujenzi wa Shule na nyumba vya madarasa, Mradi wa maji rwakajunju , Ujenzi na ukarabati wa Barabara, pia Miradi katika sekta ya Afya.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com