Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake Machi O2, 2018 Mjini Bariadi
Na Stella
Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema
Serikali Mkoani humo haijawakataa wadau wa Afya kutoka katika Mashirika mbalimbali
ya Kitaifa na Kimataifa wanaofanya kazi mbalimbali katika kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye Sekta
ya Afya , bali inatambua mchango wao na inawaomba kufanya kazi kwa kuzingatia
vipaumbele vya Kitaifa na Mkoa kwenye Sekta ya Afya.
Mtaka ameyasema hayo katika mazungumzo maalum na
waandishi wa Habari wakati alipokuwa akifafanua kauli aliyoitoa katika kikao
kilichofanyika Februari 25 na 26 Mjini Bariadi kati ya Viongozi wa Mkoa huo na
Wadau Afya mkoani humo ya kuwataka kuelekeza zaidi fedha zao katika kujibu
mahitaji ya wananchi kwenye Afya badala ya semina na mafunzo kwa watumishi.
Amesema Serikali
inatambua mchango wa Mashirika na wadau wa Afya Mkoani humo kutokana na mambo
waliyoyafanya kuunga mkono Serikali kutatatua changamoto mbalimbali za Sekta ya
Afya, ikiwa ni pamoja na kutoa magari, kujenga majengo ya upasuaji katika
baadhi ya Vituo vya Afya na kuwajengea uwezo watumishi wa afya.
Ameongeza kuwa
pamoja na michango hiyo Mashirika mengi yanayofanya kazi Mkoani Simiyu katika
Sekta ya Afya yameonekana kujikita zaidi katika kutoa fedha nyingi kwa ajili ya
semina na mafunzo kwa watumishi wa Afya , badala ya kusaidia katika kutatua
changamoto ambazo ni vipaumbele vya Kitaifa na Mkoa pia katika Sekta ya Afya.
Aidha. Mtaka
amebainisha kuwa Vipaumbele vya Kitaifa na Mkoa katika Sekta ya Afya ni pamoja na Ujenzi wa Miundombinu
ya Afya ambayo ni majengo ya zahanati, vituo vya afya, vyumba vya upasuaji,
hospitali), Vifaa pamoja na vifaa tiba, ambapo alieleza kuwa Mkoa huo una upungufu wa
Hospitali ya Mkoa, Hospitali mbili za Wilaya, Vituo vya Afya 112 na Zahanati
291.
“Tumepitia
bajeti za mashirika haya 11 kwa ujumla wake mwaka 2018 yatatumia zaidi ya
shilingi bilioni 21, hizi ni fedha nyingi ambazo kama zitafanya kazi
inayoonekana huduma za Afya ndani ya mkoa zitaimarika, changamoto kubwa ambayo
mimi kama mkuu wa mkoa na viongozi wenzangu tumeiona ni fedha nyingi kati ya
hizo kuelekezwa kwenye mafunzo ya watumishi wa afya” alisema
“Kwanza
nimeyaomba mashirika yanayofanya kazi za Sekta ya Afya ndani ya Mkoa kila moja kuonesha kazi wanazofanya, pili
natoa wito kwa mashirika haya kuelekeza fedha nyingi kwenye kuongeza idadi ya
vituo vya afya, zahanati, vifaa na vifaa tiba ili tunapojenga uwezo kwa
watumishi wetu wa Afya wawe na mahali pa kwenda kufanyia kazi mafunzo
wanayopata” alisisitiza Mtaka
Ameongeza kuwa
Ofisi yake imeandika barua Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa ili Viongozi kutoka Wizara hizo mbili wakutanishwe
pamoja na Viongozi wa Wizara ya Afya na Viongozi wa Mkoa wa Simiyu kwa lengo la
kujadili na kuchambua tija ya fedha za wadau/mashirika hayo kwenye Sekta
ya Afya.
Mmoja wa wadau hao
Mwakilishi kutoka Shirika la Mkapa
Foundation Bi.Adeline Saguti akichangia hoja katika kikao chao na Viongozi wa
Mkoa wa Simiyu alisema Wadau wa Afya Mkoani humo wameahidi kushirikiana na Mkoa
huo kufanyia kazi maeneo yenye uhitaji katika
Sekta ya Afya.
Wadau wa Afya
(mashirika ya ndani na nje ya nchi) wanaofanya kazi na mkoa wa Simiyu ni pamoja
na AMREF, AGPAHI, CUAMM, UNFPA, Mkapa Foundation, AMERICARE, Red Cross, ICAP,
TAMA, INTRAHELTH, WORD VISION na BORESHA AFYA.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment