METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, October 9, 2022

Prof Mkenda Amhakikishia Waziri Biteko Ujenzi wa VETA wilaya ya Bukombe


Na Mathias Canal-WEST, Bukombe-Geita

Serikali inayo azma ya kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka huu wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni Mia moja (100 Bil).

Kiasi hicho cha fedha ni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi katika Wilaya 62 kwa Wilaya ambazo zilikuwa hazijajengewa Vyuo vya Ufundi Stadi. Aidha, Wilaya ya Bukombe ni miongoni mwa Wilaya hizo 62 ambazo zipo kwenye mpango wa kujengewa Vyuo vya Ufundi Stadi kwa mwaka huu wa fedha.

Akizungumza tarehe 10 Octoba 2022 wakati wa Sherehe ya Siku ya Mwalimu Duniani iliyoandaliwa na Chama cha Walimu wa wilaya ya Bukombe Mkoani Geita Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema, walimu wanaandaliwa vizuri katika kuboresha miundombinu ya elimu nchini na kutoa mfano kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kujenga madarasa zaidi ya 600 katika mkoa wa Geita na kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu ili kuweka mazingira mazuri ya ufundishaji.

Waziri Mkenda amesema kuwa Halamashauri ya Wilaya ya Bukombe inatakiwa kuandaa eneo maalumu zisizopungua Hekari 50 kwa ajili ya ujenzi huo utakaoanza hivi karibuni kama serikali ilivyopanga.

Kuhusu ruhusa za masomo kwa walimu, Waziri Mkenda amesema kuwa;

"Mwalimu akiomba ruhusa ya kwenda kusoma mpe ruhusa, mwalimu ni ufunguo wa maisha katika maendeleo ya nchi yetu, mafunzo kazini yataendelea, Serikali ya awamu ya sita imetenga bajeti kwa ajili ya kuwaendeleza walimu," amesema Dkt. Mkenda.

Aidha, Dkt. Mkenda amemhakikishia Dkt. Biteko kuwa, mwaka 2023 katika kusheherekea Siku ya Mwalimu Duniani Serikali itahakikisha siku hiyo inasheherekewa Kitaifa katika wilaya ya Bukombe ili walimu wakutane kwa pamoja.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Waziri na Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema mwalimu ni msingi wa elimu na Serikali inautambua mchango wa wao katika utoaji wa elimu.

Pia, amewataka walimu waendelee kushirikiana katika shughuli zao za kila siku, wakipendana, kuthaminiana na kusaidiana wao kwa wao ili kujenga umoja.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigela amempongeza mbunge wa Jimbo la Bukombe Dkt. Biteko kwa kuandaa Siku ya Mwalimu Duniani kwa kuadhimishwa katika wilaya ya Bukombe.

Shigela amesema, atahakikisha mwaka 2023 tukio hilo linakuwa kubwa na kuadhimishwa katika Halmashauri nyingine za Mkoa wa Geita ili kusheherekea kwa pamoja.

Siku ya Mwalimu Duniani imedhaminiwa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Waziri wa Madini Dkt Doto Biteko kama sehemu ya kuenzi mchango mkubwa wa Walimu wa Bukombe katika Kuinua Taaluma na kuambatana na utoaji wa tuzo kwa shule zilizofanya vizuri pamoja na zawadi kwa washindi kwenye mashindano ya Mwl Doto Cup.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com