METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, October 10, 2022

ACC YAWAKUTANISHA USTAWI WA JAMII, MAENDELEO YA JAMII NA VIONGOZI WA DINI


Na Rasul Kidindi,Dodoma

MAAFISA Maendeleo ya jamii na Ustawi wa jamii pamoja na viongozi wa Dini wamekutana  kwa ajili ya kuweka mpango kazi wa pamoja katika utekelezaji wa Programu  ya malezi na makuzi ya watoto.(PJT-MMMAM).

Mkutano huo umeandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na masuala ya Malezi na Makuzi ya Watoto ‘Action for Community Care (ACC) umefanyika mwishoni mwa wiki jijini hapa. 

Akizungumza katika mkutano huo Afisa Mradi wa Mradi wa Watoto Kwanza Magreth Mukama amesema,lengo la kuweka mpango kazi wa pamoja katika utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ni pamoja na kutaka jamii ijue umuhimu wa Makuzi ya mtoto.

 Mukama alisema,kwa kuwakutanisha wadau hao  inakwenda kuchochea utekelezaji wa Programu hiyo na hatimaye kujenga watu ambao watakuwa na tija katika Taifa.

 “Serikali inatekeleza Programu ya Taifa ya Malezi ,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ya Miaka mitano kwa kushirikiana na wadau mbalimbali,kwa hiyo leo tumewakutanisha wadau hawa tuweze kuwapitisha katika Mwongozo wa PJT-MMMAM,"alisema Mukama.

 Huu mkutano umewafanya watu kuelewa na hatimaye waweze kufikisha elimu hii katika jamii kila mmoja kwa nafasi yake.

Wakizungumza katika kikao kazi hicho viongozi wa dini walisema,Progframu hiyo imekuja kwa wakati muafaka na wao kama viongozi wa dini watatuia nafasi zao kuhakikisha elimu inafika kwa jamii ambayo ni waumini wao.

Kuhani Raha Halisi wa Kanisa halisi la Mungu Baba la wilayani Kondoa alisema,kwa kutumia nafasi zao watahakikisha ujumbe wa Malezi ,Makuzi na Maendeleo ya Mtoto unafika kwa waumini kupitia nyumba zao za ibada.

“Sisi viongozi wa Dini tuna watu wengi na tunaaminika,kwa hiyo hili jambo limekuja kwa wakati muafaka na sisi tutahakikisha tunashirikiana na Serikali katika utekelezaji wa suala hili ili watoto wapate malezi ambayo yatawafanya wakue vyema na baadaye kuleta tija katika Taifa.”amesema Kuhani huyo

Naye Afisa Ustawi wa Jamii Elizabeth Shoo kutoka wilaya ya Kondoa amesema,wakati wa utekelezaji wa Programu hiyo utakidhi haja na kurejesha msingi wa malezi na makuzi ya watoto.

“Siku hizi na huu utandawazi uliopo kila mtu amekuwa ‘busy’ wazazi wamejisahau jukumu lao la malezi wameliacha kwa wasichana wa kazi,u-busy wa kutafuta pesa umefanya wazazi hawajui hata kuhusu ulinzi na usalama wa watoto wao,lakini kwa ujio wa Programu hii sasa wazazi watakwenda kuamka na kulea watoto kwa kufuata misingi iliyowekwa na kuwawezesha kukua kwa utimilifu wao.”amesema Shoo

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com