METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, September 15, 2022

WAKATI MAADHIMISHO YA JUMA LA ELIMU YA WATU WAZIMA YAKIFANA KONGWA, DC MWEMA AHAIDI KULA SAHANI MOJA NA WAZAZI WANAOTOROSHA WATOTO KWENDA KUFANYA KAZI ZA NDANI






Maganga Gwensaga Kongwa, Dodoma

Kila ifikapo tarehe 8 Sept, Dunia huadhimisha  Juma la Elimu ya watu wazima ambapo Wilayani Kongwa Maadhimisho hayo  Kiwilaya yalifanyika Katika uwanja wa ofisi ya Mtendaji kata ya Hogoro lengo likiwa ni kujenga uelewa na kutambua changamoto mbalimbali zinazoikabili tasnia ya Elimu ya watu wazima. 

Maadhimisho hayo ambayo huanza Kila Septemba Mosi na Kilele chake ikiwa ni Septemba nane yaliasisiwa na UNESCO 1966 yakiwa na Lengo la kuikumbusha jamii umuhimu wa elimu ya watu wazima kama suala la heshima na haki za binadamu. 

Akitoa taarifa ya Maadhimisho hayo Mbele ya Mgeni, Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Kongwa Eugen Shirima alisema Wilaya ya Kongwa inaadhimisha Juma la Elimu ya watu wazima Kwa kuwaleta pamoja wadau wa maendeleo kufanya tathmini ya pamoja juu ya maendeleo ya Elimu ya watu wazima kwa kuzingatia mafanikio, changamoto na ufumbuzi wake Kwa lengo la kuboresha Mazingira ya kujifunza, kusoma, kuandika na kuhesabu.

Alisema Kiwilaya Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa ina jumla ya wakazi ambao ni watu wazima wenye umri kuanzia miaka 18 na zaidi 204, 831 ambao ni sawa na 52% ya idadi yote ya watu kwa sensa ya watu iliyofanyika mwaka 2012.

“Kufuatia sensa ya 2012 watu wanaojua kusoma na kuandika Halmashauri ya Kongwa ni 61% huku wasiojua kusoma na kuandika ni 38% ” Alisema Shirima

Akitolea mfano kata ya Hogoro  yenye watu wazima 11,291 Shirima alisema kwa sensa ya mwaka 2012 wanaojua kusoma na kuandika ni 6,969 sawa na 61.7% ambapo wanaume ni 3,274 na wanawake 3,692 huku wasiojua kusoma wakiwa 4,325 sawa na 38.3%.

Aidha alisema kufuatia ushahidi wa takwimu ni dhahiri kuwa Halmashauri ya Kongwa ina tatizo la watu wazima la kutojua kusoma, kuandika na kuhesabu kwa kiwango kikubwa hivyo Kuna haja ya kuboresha Mazingira ya  kusoma, kuandika na kuhesabu ili kupunguza au kumaliza tatizo hilo. 

Alizungumzia juhudi mbalimbali ambazo zimeendelea kuchukuliwa ni pamoja na mpango maalumu wa elimu ya Msingi kwa WANAFUNZI waliokosa (MEMKWA) mpango ambao unampa nafasi mtoto aliyekosa nafasi ya Elimu ya Msingi Katika mfumo rasmi ambapo mpaka sasa Wana vituo 9 vyenye jumla ya WANAFUNZI 174. 

Naye Afisa Maendeleo ya Jamii  Wilaya ya Kongwa kutoka ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Bi. Faraja Susuwi aliitaka jamii kuendelea kutoa kipaumbele Katika kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu ili kupunguza ujinga na wakipunguza ujinga wataepuka umaskini.

Akisoma Risala kwa Mgeni Rasmi Bi. Jane Lutego Afisa Elimu ya watu wazima wa Wilaya alizitaja shughuli mbalimbali zilizotelekezwa Katika Juma la Elimu ya watu wazima ni pamoja na kukutana na viongozi wa kata na vijiji  kuwajengea uelewa juu ya dhana ya Elimu ya watu wazima na kuweka mipango na mikakati  ya pamoja Katika kufanikisha MAADHIMISHO hayo. 

Pia kuwatambua na kupata mawasiliano ya Viongozi watano  wahamasishaji wa uanzishwaji wa vikundi wa kata na viongozi 46 wa vikundi 23 vya kata ya Hogoro.

Aliongeza kuwa hayo ni mafanikio makubwa kwa upande wao Katika kutekeleza zoezi la sensa ya kuonyesha takwimu ya Elimu ya watu wazima na Elimu nje ya mfumo rasmi wa kielimu.

Akizungumza na Wananchi waliojitokeza Katika Maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema aliwapongeza waandaaji kwa ngazi ya kata akifurahishwa na shughuli mbalimbali yakiwemo maonyesho ya bidhaa mbalimbali za vikundi vya wajasiliamali. 

“Nichukue nafasi hii kuwapongeza sana, sikutegemea kama kungekuwa na maandalizi makubwa ya namna hii kwa ngazi ya kata na zaidi nikiwa Katika kutembelea mabanda ya wajasiliamali  nimefarijika kuona Akina mama, vijana na akina baba wakijishughulisha na mambo mbalimbali ya kuongeza kipato.”Alisema DC  Mwema 

Mbali na pongezi hizo Mkuu wa Wilaya amesikitishwa sana na idadi kubwa ya watu wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu akitaja kuwa ni kikwazo kikubwa Cha maendeleo na chanzo Cha migogoro. 

“Tuna mlolongo mkubwa wa kesi na migogoro Katika Wilaya yetu na sehemu ya migogoro hiyo ni watu kutojua kusoma, kuandika na kuhesabu.” Alisema Mhe. Mwema

Alisema wazee wengi wanawaamini watoto na kuingia kwenye makubaliano mengi  yakiwemo masuala ya kuuza ardhi na mwisho wa Siku wale watoto Wanafanya ulaghai matokeo yake ni hasara kubwa kwa wahusika. 

Aliongeza kuwa amekuwa akipokea kesi nyingi za migogoro na ukichunguza kwa umakini utagundua sababu kubwa ni kutojua kusoma na kuandika kwani vijana kwa ujanja wamekuwa wakiwalaghai wazee wao. 

Mkuu huyo alihoji kwanini hali hiyo imeendelea kuwepo mwaka hadi mwaka hivyo  amezitaka mamlaka husika na jamii kwa ujumla  kuchukua hatua za makusudi kukabiliana na tatizo Hilo. 

“38% ya watu wa Kongwa ambapo ni wastani wa watu 60,000 hawajui kusoma na kuandika ni lazima tuangalie chanzo ni nini, mfano tatizo la utoro limekuwa kubwa ni jukumu la Kila mmoja sasa  kupambana Katika hili.“ Alisema 

Katika kukabiliana na hali hii ya  kutojua kusoma, kuandika Ofisi yake  itaendesha operesheni maalumu ya kuondoa utoro ambapo  watawarudisha watoto mashuleni lakini pia kupambana na wazazi ambao wanawatoa watoto wao kwenda mijini kufanya kazi za ndani.

“Tukitaka tufanikiwe kusimamia misingi ya Elimu hii kuanzia kwenye mzizi ni lazima tusiwe na mchezo kwenye Elimu, na mara zote ninasema suala la Elimu sio la Mkuu wa Wilaya tu ni la Kila Mwananchi .” Aliongeza

Historia ya Elimu ya Watu wazima Tanzania, ilianza mwaka 1961 ambapo ilibainika kuwa ujinga, kutokujua kusoma, kuandika na kuhesabu ni chanzo Cha kuchochea umaskini, magonjwa , ukandamizwaji na unywonywaji Katika jamii. 

Hivyo utoaji wa elimu kwa Wananchi wote imekuwa ikipewa  kipaumbele Katika sera na matamko mbalimbali ya kiserikali hapa Nchini. 

Katika kufanikisha utekelezaji wa sera ya matamko ya elimu ya watu wazima ilibainika kuwa ni nyenzo muhimu kutoa elimu kwa watu wote. 

Hivyo elimu ya watu wazima hutumika kama dhana ya kuleta ufumbuzi wa haraka wa changamoto zilizopo kwenye jamii Katika kuleta maendeleo ya haraka.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com