Wakala wa Majengo Tanzania (TBA),
umetakiwa kutekeleza miradi wanayoisimamia kwa wakati na kuzingatia
weledi ili kuongeza tija na uzalishaji katika Wakala huo.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Arch. Elius
Mwakalinga, wakati akifungua kikao cha siku mbili cha Baraza la
wafanyakazi wa Wakala huo, jijini Dodoma.
Agizo la Katibu Mkuu huyo limefuatia
baada ya kupata malalamiko kutoka kwa baadhi ya wateja wa Wakala huo
amabapo wamesema kuwa Wakala huo umekuwa ukichelewesha miradi, hivyo
amewataka kupitia Baraza hilo kujiwekea malengo na mpango mkakati wa
kutekeleza miradi hiyo na kuikamilisha kwa wakati.
“Nina uhakiaka suala hili lipo chini ya
uwezo wenu endapo mtajipanga vizuri na kufanya kazi kwa mshikamano na
weledi huku mkithamini mchango wa kila mmoja wenu katika eneo la kazi,
basi mtafanikiwa,” amesema Mwakalinga.
Aidha, ameutaka Wakala huo kujiwekea
maazimio yatakayowasilishwa Wizarani ambayo yatajikita katika uboreshaji
wa maslahi ya watumishi, ikiwemo kuwajengea uwezo utakaowafanya
kutimiza majukumu yao kwa wakati na ufanisi zaidi.
Kuhusu madai ambayo Wakala unadai Taasisi
nyingine za umma, Katibu Mkuu Mwakalinga ameutoa hofu Wakala huo kwa
kusema kuwa suala hilo halitafumbiwa macho na atahakikisha kuwa madeni
yote yanalipwa baada ya kuhakikiwa.
“Wekeni kumbukumbu zenu za madai vizuri
ili ziweze kuhakikiwa kabla ya kuwasilishwa kwa wahusika, nami naahidi
kufuatilia madeni haya na kuhakikisha kuwa yatalipwa,” amesisitiza
Katibu Mkuu.
Ameongeza kuwa Serikali inathamini
mchango wa Wakala huo katika kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda
ambapo amefafanua kuwa Wizara yake pamoja na Taasisi zilizo chini yake
imejiwekea agenda madhubuti ambazo anaamini zikitekelezwa basi Sekta ya
Ujenzi nchini itakuwa kwa kasi.
Naye, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TBA Arch.
Daudi Kondoro amemhakikishia Katibu Mkuu huyo kuwa atatekeleza maagizo
yote na pia atahakikisha maazimio watakayo jiwekea yanatekelezwa kwa
wakati.
Alisema kuwa taratibu za kupandisha
watumishi vyeo zinaendelea ambapo tayari watumishi 64 waliokidhi vigezo
wamepandishwa vyeo katika madaraja mbalimbali na watumishi 17
wamebadilishwa kada kulingana na taaluma zao.
Kikao hicho kimejumuisha zaidi ya wajumbe
62 ambao baadhi yao ni wakuu wa idara na vitengo, mameneja kutoka mikoa
yote, wawakilishi wa wafanya kazi kutoka idara na vitengo pamoja na
wawakilishi kutoka vyama vya wafanyakazi vilivyomo ndani ya Wakala.
0 comments:
Post a Comment