Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew (kushoto) akichangia mawazo wakati akizindua kituo cha mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa vitendo katika Ndaki ya Teknolojia za Habari na Mawasiliano (CoICT) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kituo hicho kilichojengwa kwa msaada wa kampuni ya Huawei Tanzania kilizinduliwa wakati wa kongamano la Maadhimisho ya Miaka 60 ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam na miaka 10 ya CoICT yaliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Huawei Tanzania Bw. Shang Xiaofeng akitoa hotuba yake wakati wa kongamano la Maadhimisho ya Miaka 60 ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam na miaka 10 ya CoICT yaliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye ( wa tatu kulia), Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Huawei Tanzania Bw. Shang Xiaofeng ( wa pili kushoto), Rasi wa Ndaki ya Teknolojia za Habari na Mawasiliano, Prof. Joel Mtebe ( wa pili kulia) na viongozi wengine waandamizi kutoka taasisi hizo mara baada ya uzinduzi wa kituo cha mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa vitendo katika Ndaki ya Teknolojia za Habari na Mawasiliano (CoICT) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu-Dar es Salaam
Kampuni ya Mawasiliano ya Huawei Tanzania na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wamezindua kituo cha mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa vitendo katika Ndaki ya Teknolojia za Habari na Mawasiliano (CoICT) iliyopo eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Mradi huo unaolenga kutoa uzoefu wa kivitendo kwa wanafunzi na wataalamu wa Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ulizinduliwa na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew wakati wa kongamano la Maadhimisho ya Miaka 60 ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam na miaka 10 ya CoICT yaliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Akizungumzia hatua ya Huawei, Mhandisi Kundo, aliipongeza kampuni hiyo ya China kwa jitihada zake za kuendeleza na kukuza sekta ya Habari na Mawasiliano nchini huku akibainisha kuwa serikali imefurahishwa sana na mchango wa kampuni hiyo katika kuchochea ukuaji wa sekta hiyo muhimu.
“Ni mwaka mmoja tu umepita tangu nilipozindua maabara ya TEHAMA ya Huawei katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na leo tena nimezindua kituo cha mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa vitendo hapa CoICT ambacho pia kinatokana na ufadhili wa kampuni ya Huawei. Hili ni jambo kubwa na tuna kila sababu ya kuwashukuru na kuwapongeza Huawei kwa juhudi zao,” alisema.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Huawei Tanzania Bw. Shang Xiaofeng alisema kuwa kituo hicho kinalenga kutoa mafunzo kwa wahandisi zaidi ya 200 kila mwaka wakiwemo wanafunzi na wahitimu ili kukuza mfumo wa ikolojia wa vipaji nchini katika miaka ijayo.
“Kujenga uhusiano wa muda mrefu, kutafuta njia nzuri za kuzitumia rasilimali tulizonazo, juhudi za kuleta za maendeleo, na manufaa kwa pande zote ni jukumu letu sote. Ninaamini kabisa kituo hiki pamoja na kituo cha Mafunzo cha Huawei cha Chuo Kikuu ch Dodoma vitakuwa msingi katika kufikia mafanikio haya ya pamoja” alisema Bw. Shang
Kulingana na Bw. Shang, kampuni hiyo kwa sasa inatekeleza miradi mingi inayowanufaisha maelfu ya wanafunzi na watendaji wa sekta hiyo kwa nia ya kujengea uwezo kwenye nyanja ya TEHAMA na kuboresha maendeleo ya nyaja hii nchini.
“Miradi hii ni pamoja na programu ya mafunzo ya TEHAMA ya Huawei, Shindano la TEHAMA la Huawei pamoja na mradi wa Seeds for the Future,’’ aliitaja na kuongeza kuwa miradi hiyo ni muhimu kwa ajili ya kutimiza Dira ya Taifa ya 2025 kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza.
Alibainisha zaidi kuwa Huawei itaendelea kujitolea katika uvumbuzi wa miundombinu ya kidijitali, ili kujenga thamani kwa wateja na washirika.
‘’Huawei tunasisitiza kuwekeza zaidi ya 10% ya mapato yetu ya mauzo katika Utafiti na Maendeleo kila mwaka, na tunapanga kuendelea kuongeza uwekezaji huu. Mnamo mwaka 2021, tulitumia Dola za Marekani bilioni 2.4 katika utafiti na maendeleo, ikilinganishwa na jumla ya Dola za Marekani bilioni 120 katika muongo mmoja uliopita.’’
“Tumeanzisha maabara 86 za kimsingi duniani kote, na kuwekeza zaidi ya dola bilioni 3 katika utafiti wa kimsingi kila mwaka’’ alibainisha
Katika hotuba yake wakati wa hafla hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye alipongeza uhusiano uliopo kati ya chuo hicho na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo kampuni ya Huawei.
0 comments:
Post a Comment