Na Eleuteri Mangi, WUSM, Dar
es Salaam
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema watanzania lazima waenzi na kutumia lugha
ya Kiswahili kwa ufasaha.
Waziri Prof. Mkenda amesema
hayo Julai 5, 2022 jijini Dar es Salaam
alipokuwa Mgeni Rasmi katika Mdahalo kuhusu Lugha ya Kiswahili na Elimu
ambayo ni sehemu ya kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani Julai 7,
2022.
“Roho ya nchi ni utamaduni
wake, sisi Watanzania ni lazima tuwe mstari wa mbele kuhakikisha tunaongea
Kiswahili fasaha, hili ni jukumu letu. BAKITA na BAKIZA muwe mstari wa mbele
ili kukuza na kuendeleza matumizi ya Kiswahili na istilahi za Kiswahili”
amesema Prof. Mkenda.
Katika kuhakikisha Kiswahili
fasaha kinatumika, Prof. Mkenda amesema Wizara yake itaendelea kushirikiana na
Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Barazala Kiswahili la Taifa
(BAKITA) na Braza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) katika kusukuma mbele masuala
ya filamu ili kusaidia kukuza na kueneza Kiswahili ndani na nje ya nchi.
Waziri Prof. Mkenda ametumia
fursa hiyo kuhimiza uandishi wa mashairi, riwaya, tamthilia pamoja na hadithi
ili kusaidia kukuza lugha ya Kiswahili.
“Angalieni fursa za Kiswahili
nje ya Tanzania, ukisoma Kiswahili, ni ‘dili’ na kitakupeleka ng’ambo,
tunahitaji walimu wenye ufasaha katika lugha ya Kiswahili na Kiingereza na uwezo
mzuri wa kufundisha” amesema Prof. Mkenda.
Kilele cha Maadhimisho ya
Siku ya Kiswahili Duniani hapa nchini yatafanyika Julai 7, 2022 katika ukumbi wa
Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam ambapo dunia nzima
itasherehekea siku hiyo kwa mara ya kwanza baada ya Shirika la Umoja wa Mataifa
la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kutangaza rasmi Julai 7 ya kila mwaka
kuwa siku ya Kiswahili duniani.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment