Mhe. Dr.
Charles John Tizeba (MB)
Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi
1.0 UTANGULIZI
Hadi kufikia katikati ya mwezi
Januari, 2017 hali ya chakula na upatikanaji wa chakula hapa nchini inaonyesha
kuwa bado ni ya kuridhisha na hasa upatikanaji wa vyakula kama mchele na
maharage ikilinganishwa na zao la mahindi. Pamoja na hali hii bei za baadhi ya
vyakula zimeanza kupanda kufuatia mazao kidogo kuingia sokoni kwa wakati huu
kunakochangiwa na mwenendo usioridhisha wa unyeshaji wa mvua za vuli na
kuchelewa kuanza kunyesha kwa mvua za msimu katika maeneo mengi ya nchi.
2.0 HALI YA
MAZAO MASHAMBANI
Hali ya mazao mashambani kutoka mikoa mbalimbali
katika kipindi cha mwezi Desemba, 2016, inaonyesha kutoridhisha katika baadhi
ya maeneo kutokana na uhaba wa mvua na mtawanyiko usioridhisha. Hata hivyo
maeneo mengi ya nchi yamekuwa yakiendelea na uandaaji wa mashamba, kupanda,
kupalilia na usambazaji wa pembejeo za kilimo. Kutokana na uhaba wa mvua na
kuwa na mtawanyiko usioridhisha, hali ya unyevunyevu katika udongo si ya
kuridhisha kwa ustawishaji wa mazao ya kilimo yanayohitaji maji mengi.
Taarifa ya hali ya upatikanaji wa mvua kutoka
mikoa inayopata mvua za vuli, zinaonyesha kuwa kwa ujumla mvua zimechelewa
kuanza na zimenyesha katika kiwango cha wastani na chini ya wastani zikiwa na
mtawanyiko usioridhisha. Mikoa ya
Kagera, Mwanza, Geita, Kilimanjaro, Arusha, Mara, Pwani, Tanga, Morogoro pamoja
na sehemu ya mkoa wa Shinyanga na Simiyu na zilipoanza kunyesha zilikuwa chini
ya wastani. Mazao yaliyopandwa katika baadhi ya maeneo hayo yameathirika
kutokana na ukame uliojitokeza ukiwamo mkoa wa Kagera wilaya za Kyerwa,
Missenyi na Karagwe. Mikoa iliyobakia mvua zimeanza kunyesha ingawa mtawanyiko
wake sio wa kuridhisha.
3.0 HALI YA UPATIKANAJI CHAKULA
KATIKA MIKOA
Kulingana
na taarifa kutoka mikoani hali ya upatikanaji wa chakula katika masoko yaliopo
katika halmashauri zote za mikoa unaridhisha isipokuwa bei ya mahindi imepanda
ikilinganishwa na mwaka 2016 kipindi kama hiki. Hii inatokana na kutoingia
sokoni kwa mazao mapya ya msimu wa mvua za vuli. Maeneo yaliyotolewa taarifa
kuwa na uhaba mengi ni yale yaliyoonekana wakati wa tathmini ya awali ya
uzalishaji msimu wa 2015/2016. Maeneo yaliyoongezeka ni kutoka katika mikoa ya
Geita, Tabora na Kagera. Pamoja na kuwa mvua za vuli hazijanyesha vizuri na
hivyo kutokuwepo kwa mazao mapya sokoni, mikoa bado imeonyesha kuwa na ziada ya
chakula. Takwimu katika Kiambatisho hiki, kwa mazao yasiyonafaka
hazijabadilishwa katika mlinganisho wa nafaka (Grain equivalent). Aidha, Mikoa yenye kivuli taarifa zake ni za mwezi Novemba
2016 na baadhi ya mikoa takwimu zake zimetolewa katika mfumo wa wanga na
zimeonyeshwa katika kipengele cha nafaka.
4.0 HALI YA
UNUNUZI NA HIFADHI YA CHAKULA
Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya
Chakula (NFRA) kwa mwaka wa fedha 2016/2017 umepanga kununua jumla ya tani
100,000 za chakula. Hadi kufikia tarehe 8 Januari, 2017, Wakala umenunua jumla ya tani
62,087.997 za mahindi sawa na asilimia 62 ya lengo ililojiwekea. Kati
ya kiasi hicho, tani 38,162.280
zimenunuliwa kupitia vituo vya ununuzi na tani
23,925.717 kupitia vikundi vya wakulima. Aidha, hadi kufikia tarehe 12
Januari, 2017 Wakala una akiba ya tani 88,152.443
za mahindi.
5.0 TATHMINI
YA KINA YA HALI YA CHAKULA NA LISHE
Wizara
kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, FAO, TFNC pamoja na Wadau wengine wanaendelea kufanya tathmini ya
kina ya hali ya chakula na Lishe nchini katika kipindi hiki. Tathmini
inatarajiwa kukamilika tarehe 28 Januari, 2017 na itazihusisha Halmashauri 55
zenye maeneo yenye uhaba wa chakula ili kubaini kaya zilizoathirika na uhaba wa
chakula na mahitaji yao. Tathmini hiyo inayosimamiwa na kuratibiwa na Ofisi ya
Waziri Mkuu, itaiwezesha Serikali kupata taarifa za uhakika zaidi kuhusu hali
ya chakula na lishe, hasa katika maeneo ambayo yalionekana kuwa na upungufu
katika tathmini ya awali na yale yaliyojitokeza mara baada ya kufanya tathmini
.
6.0 MWENENDO
WA BEI ZA MAZAO YA CHAKULA
Serikali inaendelea
kufuatilia mwenendo wa bei za mazao ya chakula hususan Mahindi na Mchele ili
kujiridhisha uwepo wake na upatikanaji wake sokoni. Mwenendo wa bei za mazao
haya sokoni kwa kipindi cha mwezi Desemba, 2016 kutoka kwenye masoko 13 kati ya
25 ya miji mikuu hapa nchini umekuwa ukipanda na kushuka kutokana na sababu
mbalimbali.
Bei za Mahindi, Mchele na Maharage
Bei ya wastani ya mahindi katika msimu wa chakula
na soko kwa mwaka 2016/2017 imekuwa na mwelekeo wa kupanda kuanzia mwanzo wa
mwezi Julai, 2016. Bei hii iko juu ikilinganishwa na bei katika kipindi kama hicho
mwaka 2015/16. Katika kipindi cha mwezi Desemba 2016, bei ya mahindi kwa gunia
la kilo 100 imepanda na kufikia wastani wa shilingi
84,577.00 ikilinganishwa na Desemba 2015 ambapo gunia la
kilo 100 liliuzwa kwa wastani wa shilingi
65,104.00.
Kwa upande wa mchele bei ina mwelekeo wa kushuka
ambapo bei ya wastani kwa mwezi Desemba 2016 kwa gunia la kilo 100 ilikuwa shilingi 151,957.00 ikilinganishwa na
kipindi kama hiki mwaka 2015 ambapo gunia liliuzwa kwa shilingi 176,237.00. Bei ya maharage inaonyesha kushuka kidogo
kutoka wastani wa shilingi 172,852.00 mwezi Desemba
2015 na kufikia wastani wa shilingi 171,251.00 mwezi Desemba 2016.
Kupanda na kushuka kwa bei kwa kipindi kama hiki
ni jambo la kawaida kwani mwanzo wa msimu hakuna mazao yanayoingia sokoni na
hivyo hupelekea bei kupanda na mwanzo wa mavuno bei hushuka kutokana na mazao
mengi kuingia sokoni. Aidha hali ya mwenendo usioridhisha wa unyeshaji wa mvua
za vuli na za msimu kwa kipindi cha 2016/17 kwa ajili ya upatikanaji wa chakula
kwa mwaka 2017/18 katika maeneo mengi ya nchi, imechangia wafanyabiashara wa
nafaka nchini na hasa zao la mahindi kuingiza zao hili kidogo kidogo sokoni,
hivyo kuongeza kasi ya uhitaji kutoka kwa wananchi na kusababisha bei kuzidi
kupanda.
Hali halisi ya mwenendo wa bei katika masoko,
unaonyesha kuwa bei ya juu kabisa ya mahindi imeonekana katika soko la Lindi
ambapo gunia la kilo 100 liliuzwa kwa wastani wa shilingi 150,000.00 wakati bei ya juu ya mchele pia imeonekana
katika soko la Lindi ambapo gunia la kilo 100 liliuzwa kwa wastani wa shilingi 245,000.00 na bei ya juu
kabisa kwa maharage imeonekana katika soko la Lindi ambapo gunia la kilo 100
liliuzwa kwa wastani wa shilingi 243,333.00.
Bei ya chini kwa mahindi ilionekana katika soko la Mbeya ambapo gunia liliuzwa shilingi 62,600.00. Mchele bei ya chini
ilionekana katika soko la Geita ambapo gunia liliuzwa kwa wastani wa shilingi 99,000.00 na maharage bei ya
chini yaliuzwa kwa shilingi 136,400.00
katika soko la Mbeya.
7.0 HITIMISHO
Serikali
itaendelea kufuatilia mwenendo wa uzalishaji na upatikanaji wa chakula hapa
nchini. Pale itakapobainika kuwa kuna uhitaji wa chakula, Serikali itachukua
hatua stahiki. Wafanyabiashara wanahamasishwa kununua mazao ya chakula katika
maeneo yaliyo na ziada na kuweza kuyauza katika maeneo yenye uhaba. Serikali
itaendelea kuhimiza kusindika mazao ya chakula kwa kuyaongezea thamani na
kuyauza katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Kutokana na hali ya mwenendo wa unyeshaji
wa mvua za vuli na msimu kutokuridhisha katika maeneo mengi ya nchi Serikali inapenda kutoa ushauri kwa wakulima
kutumia mbegu zinazokomaa mapema na kupanda mazao yanayostahimili ukame.
Wakulima wanashauriwa kutumia kwa uangalifu na kuhifadhi akiba ya chakula cha
kutosha kwa matumizi katika kaya. Sekta binafsi inahamasishwa kuendelea
kushiriki katika kutoa masoko ya kununua na kuuza mazao katika maeneo yenye
ziada na kuyauza katika maeneo yenye uhaba.
Mhe. Dr.
Charles John Tizeba (MB)
Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi
16
Januari 2017
0 comments:
Post a Comment