Na Mwandishi Wetu, Dar
es salaam
Waziri wa Elimu, Sayansi
na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amewahimiza waombaji mikopo ya elimu ya juu
kwa mwaka 2022/2023 kusoma na kuuzingatia ‘Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa
2022/2023’ ili kuwasilisha maombi kwa usahihi.
Prof. Mkenda ameyasema
hayo katika hafla fupi ya kuzindua mwongozo huo iliyofanyika katika ofisi za
HESLB jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe, Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi wa HESLB Prof. Hamisi Dihenga na wadau wengine wa HESLB.
Prof. Mkenda amesema:
“Kuanzia leo (Jumanne, Julai 12), mwongozo huu utapatikana katika tovuti ya
HESLB (www.heslb.go.tz) na ya Wizara (www.moe.go.tz) katika lugha mbili za
Kiswahili na Kiingereza … na kuwapa fursa waombaji kuusoma. Dirisha la kupokea
maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao linatarajiwa kufunguliwa Julai 19 hadi
Septemba 30, 2022,” amesema na kuongeza:
“Dirisha la maombi ya
mikopo kwa mwaka wa masomo 2022/2023 litakuwa wazi kwa muda wa siku 70 kuanzia
Julai 19 hadi Septemba 30 mwaka huu, hivyo tunawasihi wanafunzi waombaji wasome
mwongozo kabla ya kuomba mkopo kwa kuwa ndiyo unataja sifa, vigezo na utaratibu
wa kuomba mkopo,” amesema Prof. Mkenda.
Akizungumza katika hafla
hiyo, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James
Mdoe amewakumbusha waombaji mikopo kuzingatia maelekezo yaliyomo kwenye
mwongozo ili kuondokana na changamoto ambazo hujitokeza kwa waombaji.
“Uzoefu unaonesha kuwa
wanafunzi waombaji wamekuwa hawazingatii taratibu wakati wa kufanya maombi.
Tunawasii mzingatie maelekezo ya mwongozo. Wakati wa dirisha la maombi
kumekuwepo na changamoto nyingi zinazojitokeza kwa waombaji”, amesema Prof.
Mdoe.
Naye Mkurugenzi Mtendaji
wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema kila mwaka mwezi Julai, HESLB huanza
kupokea maombi ya mkopo kwa mwaka wa masomo unaofuata ambapo mwongozo huo hutoa
maelezo ya kina kuhusu sifa na utaratibu wa kupanga mikopo kwa mwaka husika.
“Mwongozo huo
umekamilika na kuidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi. Kuanzia wiki ijayo,
tutaanza kuendesha programu za elimu kwa umma kupitia redio, televisheni,
mikutano katika Kambi za JKT na mitandao ya kijamii” amesema Badru.
Katika mwaka wa masomo 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha TZS 573 bilioni kwa ajili ya kutoa mikopo na skolashipu kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment