Kebwe ahimiza ujenzi wa maghala
Na John Nditi, Morogoro
SERIKALI ya mkoa wa Morogoro imeanza kampeni ya kuwahamasisha wadau, kujenga maghala ya kisasa ya kuhifadhi nafaka za aina mbalimbali. Hatua hiyo inatokana na mavuno makubwa ya chakula katika msimu wa mwaka huu.
Mkuu wa mkoa huo, Dk Kebwe Stephen alitoa rai hiyo wakati akitoa salamu za mkoa kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene. Simbachawene alikuwa ni mgeni rasmi katika ufunguzi wa warsha ya kujenga uelewa na utayari kuhusu utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) kwa wakuu wa mikoa, iliyofanyika hivi karibuni mkoani Morogoro.
Kebwe alisema katika msimu wa kilimo kwa mwaka 2016/2017, mkoa ulilenga kulima hekta 736,723. 56 ili kuvuna tani 2, 895,823.19 za mazao ya chakula . Hali ya mazao ya chakula ni nzuri kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha tangu mwezi wa Machi mwaka huu na katika baadhi ya maeneo, mfano wilaya za Gairo na Ulanga wameanza kuvuna mahindi.
Alisema kilimo cha mpunga kinaendelea vizuri na na katika maeneo ya milimani, uvunaji umeshaanza. Dk Kebwe alisema kuna ongezeko la mavuno kwa asilimia 44 na kufikia tano 2,316,658. 5 ukilinganisha na msimu wa mwaka 2015/2016, ambapo uzalishaji ulikuwa ni tani 1,597,895 .65 tu. Pamoja na mazao ya nafaka, wakulima wamepanda viazi vitamu, mihogo na maharage.
Mkoa ulilenga kulima hekta 210,363.17 ili kuvuna tani 3,289,168. 55 za mazao ya biashara. Dk Kebwe alisema katika msimu huu kulijitokeza mlipuko wa viwavijeshi, walioshambulia mahindi na mpunga katika maeneo mbalimbali. Udhibiti ulifanyika kwa kutumia dawa iliyotolewa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
0 comments:
Post a Comment