Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kulia) akiongea katika kikao kazi cha kupata taarifa ya utekelezaji wa mradi wa kunenepesha mbuzi unaotekelezwa na taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) na taasisi inayojishughulisha na masuala ya kilimo biashara (PASS) katika kituo cha Kongwa kilichofanyika jijini Dodoma Juni 22, 2022. Katika kikao hicho Mhe. Ulega alizitaka taasisi hizo kuhakikisha zinajikita katika vipaumbele vichache vinavyoweza kupimika na kuleta tija inayotarajiwa. Kushoto ni Mkurugenzi, Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (sekta ya Mifugo), Dkt. Angelo Mwilawa
Mkurugenzi, Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (sekta ya Mifugo), Dkt. Angelo Mwilawa (kushoto) akieleza kwa ufupi lengo la kikao kazi cha kupata taarifa ya utekelezaji wa mradi wa kunenepesha mbuzi unaotekelezwa na taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) na taasisi inayojishughulisha na masuala ya kilimo biashara(PASS) katika kituo cha Kongwa kilichofanyika jijini Dodoma Juni 22, 2022.
Pichani ni Sehemu ya washiriki wa kikao kazi cha kupata taarifa ya utekelezaji wa mradi wa kunenepesha mbuzi unaotekelezwa na taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) na taasisi inayojishughulisha na masuala ya kilimo biashara (PASS) katika kituo cha Kongwa kilichofanyika jijini Dodoma Juni 22, 2022.
Na Mbaraka Kambona,
NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega ameitaka taasisi ya
Utafiti wa Mifugo(TALIRI) na taasisi inayoshughulika na kilimo biashara(PASS)
kupitia mradi wanaoutekeleza wa
kunenepesha mbuzi kuhakikisha vijana wengi wanapata ujuzi huo ili waweze
kuwa na fursa pana ya ajira na kukuza uchumi wao.
Ulega alitoa maelekezo hayo katika kikao kazi cha kupata taarifa ya
utekelezaji wa mradi wa kunenepesha mbuzi unaotekelezwa kwa ushirikiano na
taasisi hizo mbili kilichofanyika jijini Dodoma Juni 22, 2022.
Alisema mradi huo ni lazima ujikite katika kuwasaidia vijana wengi kupata
ujuzi wa kufuga kibiashara na kuwawekea mfumo mzuri utakaowasaidia kuwezeshwa
kifedha ili wawe na mitaji ya kutosha kuendesha biashara ya mifugo.
“Tunataka tutoe ajira kwa vijana, hivyo ni lazima kuwatengeneza vijana
wengi watakaokuwa na ujuzi wa kunenepesha mifugo, sasa hivi wanaofanya
unenepeshaji wapo na wanawezeshwa na benki zetu, lakini tunataka tupate vijana
wengi zaidi watakaotengenezwa kupitia mradi huu, tukiweka nguvu yetu hapo
vizuri naamini tutawezesha vijana wengi kujiajiri,”alisema.
Aidha, aliongeza kwa kusema kuwa sasa sekta ya mifugo inakabiliwa na
changamoto kubwa ya malisho hivyo ni
muhimu wakajikita katika kuzalisha malisho ili mifugo iwe na malisho ya kutosha
wakati wote jambo litakalopelekea mifugo hiyo kuwa na uzito wenye thamani
sokoni.
"Katika taarifa zenu nimewasikia hapa mmeeleza mambo mengi
mnayotarajia kufanya kupitia mradi mnaotekeleza, ushauri wangu ni muhimu
mkachagua mambo machache mtakayoweza kutekeleza vizuri awamu kwa awamu kuliko
kubeba mambo mengi na mwisho wa siku msiweze kufikia malengo," alisema
Ulega.
Kufuatia changamoto ya kufa kwa mifugo iliyoikumba nchi hivi karibuni
aliwataka wao kama Wataalamu kuhakikisha wanatumia taaluma zao kikamilifu ili
kupunguza vifo vya mifugo nchini.
Halikadhalika aliitaka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kusaidia wadau
hao wa sekta ya mifugo kwa kuandaa mipango mizuri ya biashara na kutoa mikopo
nafuu kwa wafugaji ili waweze kufanya ufugaji wenye tija.
Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani, Dkt. Angelo Mwilawa
alisema kuwa kwa muda sasa viwanda vingi vya kuchakata nyama hapa nchini
vimekuwa vikifanya kazi chini ya uwezo wake hivyo kupitia mradi huo
unaotekelezwa na TALIRI kwa kushirikiana na PASS ukisimamiwa vizuri utakwenda
kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto hiyo.
Aliongeza kwa kusema kuwa mradi huo pia utashirikisha Halmashauri nchini
ili vijana waliopo katika maeneo hayoo waweze kushirikishwa vizuri katika
kujifunza unenepeshaji wa mifugo na kuboresha maisha yao.
Mradi huo wa kunenepesha mbuzi umeanzishwa mahsusi kwa lengo la kuwaanda na kuwawezesha vijana kushiriki mafunzo ya ujasiriamali kwa vitendo ili hatimaye kuwekeza kwenye ufugaji kibiashara na kuongeza fursa za ajira kupitia sekta ya mifugo nchini.
0 comments:
Post a Comment