METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, May 5, 2022

RASIMU YA MTAALA YAANZA KUANDIKWA




Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imeanza kazi ya uandishi wa rasimu za mitaala ya elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Ualimu.

Akifungua kikao kazi cha uandishi wa rasimu  leo tarehe 05/05/2022  katika chuo cha Veta Jijini Dodoma  ambapo  mwenyekiti wa kamati ya Kitaifa ya uboreshaji wa  Mitaala Prof. Makenya Maboko amesema kuwa kazi hiyo ni muhimu kwa maslahi ya taifa  na kuwataka wataalam mbalimbali kutumia nafasi hiyo kuifanya kwa weledi mkubwa. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) amesema Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kupitia TET imekamilisha zoezi la kuchakata maoni ya wadau juu ya hali ilivyo sasa  ya mitaala ya elimu nchini, hatua inayofuata sasa ni kuandaa rasimu za mitaala hiyo.

Amesema kuwa rasimu zitakazoandaliwa ni rasimu ya Mitaala ya Elimu ya Malezi, Awali, Msingi, Sekondari, Sekondari ya juu na Ualimu. 

Aidha amewataka wataalamu mbalimbali wanaoshiriki katika kazi hiyo ya uandishi kuifanya kazi kwa kuangalia maslahi ya taifa kwa kuwa Serikali inahitaji mageuzi makubwa kwenye elimu.

" Mmeaminiwa kuisaidia Serikali katika kuleta mageuzi kwenye Elimu, maoni ya wadau ni kuwa Mitaala imejaa vitu vingi visivyo na msaada kwa watoto, ninawaomba muangalie vitu vitakavyowasaidia kulingana na karne tuliyopo" amesema Dkt. Komba

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Ubunifu na Ukuzaji wa Mitaala Dkt. Godson Lema amesema kuwa, kazi hiyo inawashirikisha wataalam kutoka vyuo vikuu Tanzania Bara na Zanzibar, Wataalamu kutoka VETA, vyuo vya ualimu, vyuo vya ufundi, wadhibiti ubora, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), wataalamu kutoka wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum, walimu kutoka shule za msingi na sekondari pamoja na wakuza mitaala kutoka TET.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com