METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, October 14, 2020

MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUONGEZA KASI YA USHIRIKA

Makamu Mkuu wa Chuo cha Ushirika Moshi Prof. Alfred Sife akifungua rasmi Maadhimisho Kuelekea Siku ya Kimataifa ya Vyama vya Akiba na Mikopo Duniani, yanayoendelea Jijini Arusha.

Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Bw. Charles Malunde akieleza utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika katika kusimamia Sekta ya Ushirika nchini wakati wa Uzinduzi wa Maadhimisho ya kuelekea Siku ya Kimataifa ya Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) yaliyoanza tarehe 12 na kilele chake kufikia 15 Oktoba, 2020 Jijini Arusha. 

Wanaushirika wa Vyama vya Akiba na Mikopo kutoka maeneo mbalimbali nchini wakisikiliza na kufuatilia kwa makini mada mbalimbali zilizokuwa zikiendelea wakati wa Maadhimisho Kuelekea Siku ya Kimataifa ya Vyama vya Akiba na Mikopo Duniani, yanayoendelea Jijini Arusha.

Wanaushirika wa Vyama vya Akiba na Mikopo wameshauriwa kuendelea kujifunza kuhusu Ushirika pamoja na kuendeleza ubunifu na matumizi ya Tehama katika kuboresha huduma za Ushirika kwa Wanachama.

Hayo yamebainishwa na Makamu Mkuu wa Chuo cha Ushirika Moshi Prof. Alfred Sife akiwa mgeni rasmi Oktoba 13, 2020 katika Uzinduzi wa Maadhimisho ya Kimataifa ya kuelekea siku ya Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS), Jijini Arusha.

Prof. Sife ameeleza kuwa ni wakati kwa Wanaushirika kuongeza matumizi ya Teknolojia na mifumo ya TEHAMA itakayosaidia katika kukuza na kuongeza utoaji wa huduma kwa haraka na usahihi zaidi kwa Wanachama wa Vyama vya Akiba na Mikopo. Aliongeza kuwa kufanya hivyo kutaongeza na kuendeleza tija na ufanisi ya utendaji wa Vyama hivyo vya Ushirika na kupunguza malalamiko pamoja na vitendo kinyume na taratibu za Ushirika.

“Wanaushirika tuboreshe kwa kubuni huduma mpya zinazohitajika kwa Wanachama kulingana na mazingira ili tuendane na teknolojia za kisasa zinazoenda na wakati,” alisema Prof. Sife

Aidha, Makamu Mkuu huyo ametoa Rai kwa Vyama vya Akiba na Mikopo kuendelea kujisajili ili kupata Leseni za Uendeshaji kwa mujibu wa Sheria Na. 10 ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018) ili kuhakikisha Vyama vinatekeleza majuku yao kwa kufuata Sheria husika.

Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Bw. Charles Malunde akiongea katika Ufunguzi huo amesema Tume ya Maendeleo ya Ushirika itaendelea kutoa Miongozo mbalimbali ya uendeshaji wa Vyama vya Ushirika ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Ushirika inaimarika na kuendelea kutoa mchango katika Pato la Taifa.

“Tume ya Maendeleo ya Ushirika ina wajibu wa kutoa Miongozo kwa Sekta ya Ushirika kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika Na.6 ya mwaka 2013,” alisema Naibu Mrajis Malunde

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Muungano wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SCCULT) Somoe Nguhwe amesema Maadhimisho hayo mwaka huu ni ya 11 kuadhimishwa hapa nchini kwa Kauli mbiu isemayo “Kuchochea matumaini kwa Jumuiya ya Kimataifa” Akifafanua kuwa Kauli mbiu hiyo inatokana na hali ya Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) kuwa sehemu ya wananchi kupata matumaini ya kiuchumi hususani kwa wananchi wa kipato cha chini. Aliongeza kuwa Vyama hivi vinajiendesha kutokana na mtaji, hisa na akiba zinazotokana na Wanachama wenyewe hivyo amewataka Wanaushirika kuzingatia ukopaji wenye tija na urejeshaji kwa wakati.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com