Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akihutubia wakati wa Maadhimisho hayo ya Siku ya Kimataifa ya Mbolea, leo mchana, tarehe 13 Oktoba, 2020.

Wakulima na Wadau wa mbolea wakifuatilia hotuba za Viongozi wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani, leo mchana, tarehe 13 Oktoba, 2020.

Mgeni Rasmi wa Siku ya
Mbolea, Mhe. Omary Mgumba, Naibu Waziri Kilimo katikati akiwa na Mkuu wa mkoa
wa Morogoro, Mhe. Loata Ole Sanare pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana
Gerald Kusaya wakisikiliza Mwakilishi wa Kampuni ya Minjingu mkoa wa Morogoro.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald
Kusaya amesema kuwa Serikali imejipanga vizuri ili kuhakikisha Wakulima wote
nchini wanapata mbolea kwa wakati na kwa bei nafuu.
Katibu Mkuu Kusaya ameyasema hayo
mchana wa leo, tarehe 13 Oktoba, 2020 kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mbolea
Kimataifa ambapo Kitaifa siku hiyo imeadhimishwa katika kitongoji cha Dakawa,
wilayani Mvomelo, mkoani Morogoro.
Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa
Wizara itaendelea kuhakikisha Wakulima wanapata pembejeo bora kwa wakati na kwa
bei nafuu, kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) na Wadau wengine.
“Wizara itaimarisha na kusimamia mifumo
iliyopo; Ikiwemo Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea (Bulk Procurement System – BPS) kwa
pamoja na tutawashawishi Wadau wa Maendeleo ili waendelee kushirikiana nasi ili
kuliletea taifa letu maendeleo kupitia Sekta ya Kilimo”. Amekaririwa Katibu
Mkuu.
Katibu Mkuu Kilimo Bwana Gerald Kusaya
ameongeza kuwa Wizara ya Kilimo kupitia Taasisi ya Utafiti wa Mazao ya Kilimo
(TARI) ipo mbio kukamilisha zoezi la kupima sampuli za udongo katika Kata zote
nchini ili kufahamu mahitaji ya virutubishi vya udongo wote kuanzia ngazi ya
Kata na kwa kufanya hivyo; Wizara itakuwa na kanzi data ambayo itatoa taarifa
ya mapungufu ya udongo ambapo ushauri kuhusu matumizi ya mbolea yatafanyika kisasa na kwa usahihi.
Katibu Mkuu amesema hayo wakati wa
Maadhimisho ya Siku ya Mbolea ambayo kwa mwaka huu imeadhimishawa katika
kitongoji cha Dakawa wilayani Mvomelo mkoani Morogoro.
Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa
Wizara itaendelea kuzisimamia Taasisi zake zote zilizo kwenye mnyororo wa
thamani wa kilimo ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ili
kuhakikisha Wakulima wanapata pembejeo bora kwa wakati na kwa bei nafuu.
Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa
Wizara kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II)
ili kuongeza tija na kuhakikisha mazao ya kilimo yanapata soko lenye bei nzuri
kwa kuziimarisha Taasisi ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA na Bodi
ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko CPB) ili zinunue mazao ya kilimo kwa kiwango kikubwa.
Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa
Wizara ipo kwenye mapitio ya Sera ya Kilimo ya mwaka 2013 na pamoja na kutunga
Sheria ya Kilimo ili kuiwezesha Sekta ya Kilimo kuongeza tija maradufu ili
kulifanya taifa kuuza chakula kingi nje ya nchi na kuongeza malighafi za
viwandani pamoja na kuongeza mchango mkubwa zaidi ya sasa kwenye pato la taifa.
Siku ya Mbolea Duniani huadhimishwa
kila mwaka tarehe 13 Oktoba ikiwa ni kumbukizi ya uvumbuzi wa kirutubishi aina
ya amonia kinachopatikana hewani, uvumbuzi uliofanywa na Bwana Fritz Haber,
Raia wa Ujerumani mwaka 1908.
Siku ya Mbolea Duniani iliadhimishwa
kwa mara ya kwanza tarehe 13 Oktoba 2016 nchini Uingereza na hapa nchini
Maadhimisho haya yanafanyika kwa mara ya tatu sasa. Kuadhimishwa kwa siku hii
ni mpango wa Kimataifa unaoungwa mkono na
Jumuiya za Sekta ya Mbolea Duniani kwa lengo la kuelimisha Umma kuhusu
matumizi ya mbolea na manufaa yatokayo na matumizi hayo na kutia moyo juhudi za
ubunifu katika teknolojia za mbolea katika
kilimo kwa mustakabali wa maendeleo endelevu.
Uvumbuzi huo ulichochea mapinduzi ya
kijani katika karne ya 20 yaliyowezesha kuongezeka kwa uzalishaji katika kilimo
kutokana na matumizi ya mbolea. Mapinduzi hayo yalisaidia kupunguza kwa kiasi
kikubwa janga la njaa na kuleta uhakika wa chakula katika nchi nyingi duniani.
0 comments:
Post a Comment