METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, February 2, 2019

Balozi Kijazi aagiza Makatibu Wakuu kuhimiza michezo


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Bi Maimuna Tarishi (mwenye miwani) akisalimiana na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Mhandisi Dr. Leonard Chamuriho kabla ya kuanza kwa mbio fupi (jogging) za bonanza la michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Taasisi, Wakala wa Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI), iliyoanzia kwenye uwanja wa Jamhuri hadi Ofisi za Bunge na baadaye kurudi Jamhuri.
Mgeni Rasmi wa Bonanza la Shirikisho la Michezo Wizara, Idara, Taasisi, Wakala wa Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI), Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Bi. Maimuna Tarishi (mwenye miwani) jana akiongoza mbio fupi (jogging) zilizoanzia kwenye uwanja wa Jamhuri hadi Bunge na kurudi Jamhuri. Wa pili kushoto ni Hab Mkwizu kutoka Utumishi (aliwahi kuwa Mwenyekiti Shimiwi miaka ya 1990) na wa pili kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Mhandisi Dr. Leonard Chamuriho.

Na Sifa Lubasi, Dodoma

KATIBU Mkuu Kiongozi, ambaye pia ni Mkuu wa Utumishi wa Umma, Balozi Mhandisi John Kijazi amewaagiza Makatibu Wakuu kuhimiza michezo mahala pa kazi kwa vitendo ili kuwa na watumishi wa Umma wenye afya njema.

Kauli hiyo iliwakilishwa jana na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Bi. Maimuna Tarishi aliyemwakilisha Balozi Kijazi katika Bonanza la michezo lililoandaliwa na Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala wa Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI), na kufanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Bi. Tarishi ameweka msisitizo kwa kuwa michezo ni kazi na kazi ni michezo, ambapo sasa Makatibu Wakuu waweke mazingira yatakayowezesha watumishi wa umma kupitia taasisi zao waweze kushiriki kwenye michezo mbalimbali, ambayo inajenga umoja na ushirikiano baina ya watumishi.

“Haya ni maagizo ya Katibu mkuu kiongozi amenituma nije niseme kwa kuwa yupo katika kazi nyingine, wito ni kwa Makatibu Wakuu wote na wakuu wa taasisi kuhakikisha wanaweka mazingira wezeshi yatakayowezesha watumishi kufanya mazoezi mara kwa mara na hata katika michezo kama hii ya Shimiwi,” amesema Bi. Tarishi.

Amesema sasa uwekwe utaratibu kwa Watumishi wa Umma kushiriki michezo ambayo haitatumia gharama kama wanavyodhania wengine. “Kwa waajiri hatuna budi kuweka mazingira wezeshi ya kuwawezesha Watumishi kuwa na utaratibu wa kushiriki kwenye michezo yeyote na hii inafanyika bila gharama yeyote kabisa kwani wakati mwingine tunakimbilia hatuna fedha au hajatenga kifungu katika bajeti wakati hata hapa ukiangalia hakuna gharama kubwa iliyotumika,” amesisitizaBi. Tarishi.

Bi. Tarishi amewataka watumishi wa umma kufanya mazoezi ya kila wakati ili kujiweka katika afya kwa wakati wote, ambayo itawasaidia kufanya kazi kwa weledi.

Bi. Tarishi ametoa pia maagizo kwa viongozi wa Shimiwi, kwa kuwa sasa wameanza kufufua michezo hii baada ya kusimama kwa muda mrefu, na sasa waendelee mbele kwani yanawakutanisha Watumishi wa maeneo mbalimbali ya kazi ya serikali na husaidia kubadilishana uzoefu.

“Hii ni rai yangu kwenu kwa kuwa sasa mmeanza tena michezo yenu hii tunapenda tuone inasonga mbele kwani hushirikisha watumishi kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali, na yanajenga umoja kama watumishi wa umma, na tuwekee maanani na kutekeleza haya,” amesema Bi. Tarishi.

Hatahivyo, amesema michezo ni nidhamu hivyo kuwe na nidhamu kwenye michezo kwani kutasaidia watumishi kufanya kazi kwa bidii na kuwa na ubinifu wa hali ya juu.
Naye Mwenyekiti wa SHIMIWI, Bw. Daniel Mwalusamba amesema wachezaji wanahimizwa kufanya mazoezi kwa ajili ya kujenga, kulinda na kuimarisha afya zao.

“Michezo ni kazi hivyo wanapaswa kuzingatia taratibu na miongozo inayokuwa imetolewa kila wakati na serikali, na kama agenda ya kitaifa ilivyo ya kujenga Tanzania ya Viwanda, na ili tufanikiwe tunahitaji kuwa na Watumishi wenye afya bora wanaoweza kufanya majukumu yao kwa wakati na kushiriki michezo mbalimbali, ambapo sasa wanaweza kuandaa mabonanza sehemu za kazi kwa siku ya za mwishoni mwa wiki,” amesema Bw. Mwalusamba.

Hatahivyo, amesema katika kikao cha juzi kilichofanyika kwenye ukumbi wa Hazina na kuwahusisha Wenyeviti na Makatibu wa klabu za michezo mahala pa kazi, ambapo wamekumbushwa kusimamia michezo kwa kuwa ni sehemu ya kazi na wanapaswa kusimamia na kutekeleza majukumu yote yanayotolewa na serikali.

Katika michezo iliyochezwa jana kwa upande wa kuvuta Kamba wanaume timu ya Waziri Mkuu wametoa jasho na Mambo ya Ndani na kutoka sare ya mvuto 1-1; wakati katika netiboli timu ya Utumishi imechapwa na Tamisemi magoli 24-17; huku Afya wakiwashinda GST magoli 9-6.

Katika mchezo wa soka Utumishi wamewachapa Afya magoli 2-0; huku Ardhi wamewashinda Mwanasheria Mkuu kwa magoli 4-0.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com