Na Mathias Canal, Dar es salaam
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof. Adolf Mkenda leo tarehe 29 Januari 2022 ametoa tuzo kwa walimu wa somo la hisabati ambao wanafunzi wao wamefanya vizuri katika mtihani wa kidato cha nne kwa mwaka 2021 na kupata wastani wa alama A na B katika somo hilo.
Tukio hilo limefanyika katika ukumbi wa Lecture Theatre I Chuo Kikuu Cha Dar es salaam (UDSM) na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe Heri James pamoja na Mbunge wa Jimbo la Ubungo Mhe Prof. Kitila Mkumbo.
Prof Mkenda amesema kuwa kutolewa kwa Tuzo hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya motisha kwa walimu wa somo la Hisabati inayotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ubunge iliyopewa jina la KiuHisabati ikiwa ni kuchochea kiu ya kujifunzia Hisabati.
Waziri Mkenda amepongeza Programu hiyo ambayo ni jitihada kubwa inayozaa matunda kwa kutoa motisha na utambuzi katika ufaulu wa wanafunzi nchini.
Akizungumzia kuhusu matokeo ya kidato cha nne amesema kuwa kwa mwaka 2021 watahiniwa wenye matokeo ya kidato cha nne ni 483,820. Takwimu za matokeo ya mtihani huo zinaonesha kuwa watahiniwa wamefanya vizuri katika masomo mengi ambapo ufaulu uko juu ya wastani kati ya asilimia 55.33 na 95.58 isipokuwa somo moja la Basic Mathematics ambapo ufaulu wa somo hili upo chini ya wastani.
Serikali inaendelea na jitihada zake za kuboresha miundombinu katika sekta ya elimu nchini ikiwemo Manispaa ya Ubungo ambapo kupitia mradi wa EP4R serikali ilitoa milioni 304,200,000 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu kwenye shule za msingi.
Kadhalika, Prof Mkenda amesema kuwa kupitia mradi wa SEQUIP Wizara imetoa fedha kiasi cha shilingi milioni 970 kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili mpya kwenye Manispaa ya Ubungo, pia inategemea kutoa milioni 260 kwa ajili ya ukamilishaji wa shule hizo.
Ameongeza kuwa serikali kupitia wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaendelea kufanya tathmini ya kubaini changamoto zinazoelekea ufaulu halikadhali tathmini ya kubaini kwanini wanafunzi wanafeli.
Mbunge wa Jimbo la Ubungo Mhe Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa ili kuonyesha msisitio na umuhimu wa elimu, serikali imeweka msisitizo mkubwa kwa kutoa kiasi cha Bilioni 3.2 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa kwenye shule za Wilaya ya Ubungo.
Amesema kuwa kupitia Programu hiyo iliyotekelezwa kwa muda mfupi imetoa mafanikio makubwa kwani kiwango cha ufauli kwa daraja A na B kwa mwaka 2022 umepanda ukilinganisha na mwaka 2021 ambapo hapakuwa na A hata moja sasa zipo A 30 katika shule nane zilizoingia kwenye Programu, huku daraja B zikiwa zimepatikana B 31 kutoka 9 mwaka 2021.
Prof Kitila amesema kuwa Walengwa wa Tuzo zinazotokana na Programu hiyo ni wanafunzi wanaofanya mtihani wa kidato cha nne na walimu wanaofundisha kidato cha nne katika shule zote za jimbo la Ubungo.
Walengwa wengine katika programu hiyo ni wazazi wa wanafunzi watakaopata daraja A na kujiunga na kidato cha tano watalipiwa ada yote wakati wote wa masomo ya kidato cha tano na sita, huku kwa wale watapata daraja B na kujiungana shule ya sekondari watalipiwa nusu ada wakati wa masomo ya kidato cha tano sita.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ubunge Mje Herry James amepongeza Programu hiyo kwani itajenga uelewa wa pamoja katika jamii juu ya masomo ya hesabu na masomo yanayoendana na masomo ya hesabu.
Ameongeza kuwa Utekelezaji wa Programu hiyo umethitisha matokeo ya tafiti zingine yanayoonyesha kuwa motisha kwa walimu ni nyenzo muhimu katika kuchochea kiu ya wanafunzi kujifunza na hivyo kufanya vizuri zaidi katika masomo yao.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment