
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.
********************************
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo ametoa siku sita kwa wakusanya mapato wa halmashauri nne za mkoa
huo ambao hawajawasilisha makunsanyo yao benki ili kuweza kusomeka
katika mfumo wa kukusanya mapato ngazi ya halmashauri (Local Government
Revenue Collection Information System – LGRCIS).
Amesema kuwa wadaiwa hao
wanatakiwa kurudisha shilingi 1,217,350,090.85 ya mapato ambapo hadi
tarehe 23.9.2019 fedha hizo zinasomeka kwenye mfumo lakini bado
hazijapelekwa benki na hivyo kuhisiwa kuwa zimo kwenye mifuko ya wadaiwa
hao huku halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ikiongoza kwa kuwa na deni
kubwa la shilingi 695,288,837.45.
Ameyasema hayo katika kikao maalum
cha kuwasilishiwa taarifa ya hali ya mapato Mkoani humo iliyofanywa na
timu ya uhakiki na ufuatiliaji wa mapato ya ndani kwenye mfumo
iliyoongozwa na Katibu Tawala msaidizi seksheni ya serikali za Mitaa,
kikao ambacho kimehudhuriwa na wakurugenzi, wakaguzi wa ndani pamoja na
maafisa TEHAMA wa halmashauri.
“Hawa wadaiwa wote hawa ambao
majina yao ninayo hapa, wako wengi, wengi sana, ninawapa siku sita,
wadaiwa wote wawe wamerudisha fedha hizi, zote zirudi na siku kama hii
wiki ijayo jumanne wote waje hapa, ntakaa nao kikao, wawe wamemaliza
madeni yao yote na mifumo yenu yote muwe mmeikamilisha na katika kikao
hicho kutakuwa na kamati ya ulinzi na usalama wote tutakuwa hapa, sina
mchezo na upande wa kukusanya mapato, tusipokusanya vizuri inamaana hata
ile 10% ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu haitatolewa vizuri,”
Alisisitiza.
Aidha, Alimuagiza Katibu Tawala wa
mkoa kuhakikisha anawalinda wakaguzi wa ndani ambao ndio jicho la
kwanza ndani ya halmashauri kabla ya kuingia kwa mkaguzi wa nje na
kuwataka wakaguzi hao kutokatishwa tamaa na mtu yeyote mwenye lengo la
kujipatia umaarufu wa kisiasa na kuongeza kuwa mapendekezo yanayotolewa
na wakaguzi hao ni wajibu kufanyiwa kazi kwa haraka ili kuepukana na
hoja za ukaguzi kutoka kwa wakaguzi wa nje.
Awali akitoa taarifa ya uhakiki na
ufuatiliaji wa mapato ya ndani kwenye mfumo wa kielektroniki, Katibu
Tawala msaidizi seksheni ya Serikali za Mitaa Albinus Mgonya alisema
kuwa miongoni mwa masuala yaliyobainika katika ukaguzi huo ilionekana
kuwa kuna tatizo kubwa la kuwepo kwa matumizi ya fedha kabla ya
kupelekwa benki na mapato mengine kuwepo kwenye mikono ya watu kwa muda
mrefu hali ianyopelekea kujikopesha na kushindwa kurudisha.
“Upo udanganyifu kwenye baadhi ya
vituo vya kukusanya mapato kama vile stendi za mabasi, Minada, maegesho
ya magari n.k ambapo watoa ushuru kwa maana ya wateja hawana uhitaji wa
risiti kulingana na uharaka wao kwenye kazi zao, pia kuna udhaifu kwenye
usajili wa POS (Point Of Sales Machine) ambapo baadhi ya halmashauri
zimebainika kusajili kwa jina la sehemu au cheo mfano VEO au WEO badala
ya jina la mhusika na kusababisha mdaiwa halisi kutojulikana na
kuwajibishwa kisheria,” Alisema.
Kwa upande wake mkaguzi wa ndani
wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Sigridi Mapunda alioroddhesha
changamoto kadhaa ikiwemo udhaifu wa utekelezwaji wa hoja anazoziibua
katika kazi yake ya ukaguzi, udhaifu katika ofisi ya mweka hazina pamoja
na afisa TEHAMA wa halmashauri kushindwa kushughulikia miamala
iliyolipwa ili kuweza kufutwa katika mfumo.
“Wale wakusanya mapato, watendaji
wa kata huwa hawawashi zile mashine na hivyo hufanya kazi ‘offline’
wanapokuja kuchukua bili huwa wanawasha muda mfupi mara ile miamala
inapofunguka wanapewa bili ambayo ni ndogo kwasababu miamala mingine
inakuwa bado haijafunguka lakini baadae katika mfumo madeni ya wale
wakusanyaji yanapanda kutokana na kufunguka kwa ile mialamala,” Alisema.
Hadi kufikia tarehe 23.9.2019
mapato ambayo hayajawasilishwa (defaulters) kwa Manispaa ya Sumbawanga
ni shilingi 45,454,992,68, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ni
Shilingi 695,288,837.45, Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo ni Shilingi
255,883,853.32 na Halmashuri ya Wilaya ya Nkasi ni Shilingi
220,722,407.40.
0 comments:
Post a Comment