Wajumbe
wa mataifa aya Afrika wa mashindano ya Soka bara la Afrika
kwa wenye ulemavu (CANAF) wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mhe.
Bashungwa, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo mara baada ya kufungua Mkutano
Mkuu wa Shirikisho hilo la Afrika Disema 3, 2021 jijini Dar es Salaam.
Na. John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe. Innocent Bashungwa amesema Tanzania ipo tayari kuwa mwenyeji wa mashindano ya dunia mchezo wa soka kwa wenye ulemavu (WAF) baada ya kumalizika mashindano ya dunia ya mchezo huo Oktoba , 2022 nchini Uturuki.
Mhe. Bashungwa ameyasema hayo leo Disemba 3, 2021 alipoambatana
na Katibu Mkuu wa Wizara yake, Dkt. Hassan Abbasi, Mkurugenzi wa Michezo Yusuph
Omary na Kaimu Katibu wa Baraza la Michezo la Taifa, Neema Msitha wakati
akifungua Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka la Bara la Afrika kwa wenye
Ulemavu jijini Dar es Salaam ambao pamoja na mambo mengine una lengo la
kuwachagua viongozi wakuu wa Shirikisho hilo.
Aidha, ametoa wito kwa mkutano huo wa ngazi ya juu kabisa
Afrika kufikiria kuyaleta mashindano hayo kutokana na mazingira wezeshi na
utashi mkubwa wa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Amewataka kutumia mashindano haya kuelimisha dunia kupinga ubaguzi
na mila potofu za kuwatenga na kuwabagua wenye ulemavu kwa kuwa ni binadamu
sawa na wengine na kwamba wanauwezo sawa na wengine.
Ametumia tukio hilo muhimu kukaribisha mataifa yote ya
Afrika kuja kutembelea kilele cha Afrika; Mlima Kilimanjaro na vivutio
mbalimbali vya utalii ikiwa ni pamoja na utalii wa baharini katika kisiwa cha
Zanzibar.
Naye Makamu wa pili wa Shirikisho la soka dunia kwa wenye
ulemavu (WAF) Mateus Wildack ametuma salamu za pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu kwa uongozi mahiri wa kuiletea Tanzania
maendeleo ya haraka na kuwashirikisha kikamilifu wenye ulemavu na kuwapa
kipaumbele kwenye maendeleo hayo ikiwa ni pamoja na eneo la michezo ambayo
imefanya vizuri sana.
Ameisifia Serikali kwa uratibu makini iliyofanya kwenye
mashindano hayo yaliyofanyika kwa siku saba jijini Dar es Salaam na
kuelezea kuwa yamefanyika kitaalam.
Rais wa Shirikisho hilo wa Afrika (FAAF) Mchungaji Richard Nii
Adesah amepongeza Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano na uwezeshaji
iliyotoa katika kipindi chote cha mashindano ambapo amesema mkutano huo utasaidia
kuleta mabadiliko makubwa kwenye michezo ya walemavu katika Bara la
Afrika.
Aidha amewataka mataifa yote ya Afrika kutokubali kugawanywa na kitu chochote kutokana na umoja imara uliojengeka baina ya nchi zote kutokana na mashindano hayo ya Afrika.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment