METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, November 14, 2021

WILAYA YA KWIMBA YAJA NA MKAKATI WA UBORESHAJI ZAO LA PAMBA KUHAKIKISHA INAFIKIA LENGO LA TANI 30,000 WALILOWEKEWA

Mkuu wa wilaya ya Kwimba Johari Mussa Samizi

Balozi wa zao la Pamba nchini Aggrey Mwanri aliyevaa koti la blue akifundisha.

Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza katika msimu mpya wa kilimo cha zao la pamba mwaka 2021/2022 imejiwekea mikakati mbalimbali ili kuhakikisha inafikia malengo waliyowekewa na serikali ya kuzalisha tani 30,000.

Katika kufikia malengo hayo Wilaya hiyo kwa kushirikiana na balozi wa zao la Pamba nchini Aggrey Mwanri wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kilimo bora cha zao hilo kwa kutumia vipimo vipya ambavyo vimefanyiwa utafiti na kituo cha utafiti cha Ukiriguru.

Akizungumza na City fm Radio na City Digital  iliyotaka kufahamu mikakati gani ambayo wilaya imekuja nayo, Mkuu wa wilaya ya Kwimba Johari Mussa Samizi  alisema mbali na elimu kutolewa na balozi watahakikisha maafisa ugani kwa kushirikiana na maafisa wa kilimo na umwagiliaji wa wilaya wanazungukia wakulima wote katika hatua zote za awali kuhakikisha wanatumia maarifa yote waliyopata.

“Kihistoria Wilaya ya Kwimba ndo ilikuwa kinara wa uzalishaji wa zao la pamba hapa nchini, sasa tumepitia changamoto nyingi ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi lakini sasa tumeamua kuhakikisha kwamba Kwimba inarudi kwenye nafasi yake na hili linawezekana”. Alisema

“Kama unavyofahamu upandaji unatarajia kuanza Novemba 15 kwahiyo kwa sasa tupo katika kuhakikisha wananchi wote wanafatilia mafunzo haya ikiwemo vipimo vipya vya upandaji ambavyo ni sentiminta 60 kwa 30 na kwa mujibu wa wataalamu kupitia vipimo hivi tutaongeza uzalishaji tofauti na vile ambavyo vilitumika awali”. Aliongeza

“ Mbali na vipimo kwa kushirikiana na balozi wa zao la Pamba wakulima wameelekezwa namna bora ya kuanda mashamba na uzuri elimu hii ilianza kutolewa na wataalamu wa kilimo kutoka wilayani na mpaka kufikia hatua hii sasa ya upandaji na tunaamini kwa kuzingatia hili mwakani wilaya yetu itafanya maajabu makubwa sana.”

Kwa upande wake afisa kilimo na umwagiliaji wilayani humo Mhandisi Magreth Kavalo amelitaja zao la Pamba kuwa ni moja wapo ya mazao ya biashara wilayani humo, na kuwataka wakulima kuzingatia mafunzo yote yaliyotolewa na balozi wa Pamba kwa ajili ya kuongeza tija katika zao hilo.

“Lengo kuu tulilonalo kwa sasa ni kuongeza tija kwenye uzalishaji kutoka kilo 100, 200 na 300 na katika hilo tumeanza mikutano ya uhamasishaji kupitia maafisa ugani, maafisa kilimo na maafisa kutoka halmashauri  pia tumeunda vikundi vya  wakulima wahamasishaji tunawafundisha mbinu za kilimo bora na hasa zile kanuni kumi bora za kilimo cha zao la pamba  ili wawafikie wakulima kwenye maeneo mbalimbali.”

Aidha amewata wakulima wilayani humo kuwasiliana na idara ya kilimo nha umwagiliaji kila wanapokutana na changamoto yoyote katika hatua za kilimo cha zao hilo nao wako tayari katika kumshika mkulima mpaka kufikia lengo walilojiwekea.

Katika kuhakikisha wakulima wa wilaya ya Kwimba wanafikia malengo yao, Bodi ya Pamba Tanzania imegawa pikipiki kwa maafisa ugani, imesambaza mbegu za kutosha , imegawa mifuko ya kubebea,  imetoa kamba za vipimo pamoja na kutoa elimukwa wakulima kupitia balozi wa Pamba nchini.

Naye Balozi wa zao hilo nchini Aggrey Mwanri alisema baada ya utafiti wa zao hilo kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Senegal, Brazil, Benin , Sudan ambao wanazalisha heka moja kilo 2500 lakini hapa kwetu mtu wa juu kabisa katika heka moja anatoa kilo 100 zimezidi sana 300.

Hivyo basi bodi ya Pamba waliamua kufanya mabadiliko kwenye vipimo, lakini pia waligundua kuna makosa mbalimbali yanayofanywa na wakulima na hivyo kuleta uzalishaji hafifu na usio na tija.

“Tuligundua baadhi ya wakulima hawaharibu masalio  shambani, hawapulizii vizuri dawa ya kuulia wadudu, hawapalilii vizuri, wengine wanachanganya mazao Zaidi ya mawili katika shamba moja, wengine baada ya kulima wanavuna vibaya na hivyo Pamba yetu inaonekana ni chafu dhidi ya mataifa mengine yanayolima zao hilo.” Alisema

“Kupitia mafunzo haya tumewaelekeza wakulima vipimo vipya, namna bora ya upuliziaji dawa za kuua wadudu, namna bora ya kurudishia udongo kwenye mashimo, namna na ya kupalilia, namna ya kuvuna na namna ya kutunza pamba pamoja na matumizi ya samadi.”

“Tunaamini kama wakulima watazingatia tutarajie uzalishaji mkubwa wa zao hili katika nchi yetu na tunaamini itakuwa hivyo kwani utafiti haudanganyi” alimalizia kusema.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com