METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, November 14, 2021

WATOTO 961 WAOKOLEWA KUTOKA KATIKA UTUMIKISHWAJI



Shirika lisilo la kiserikali  la kutetea haki za wafanyakazi majumbani na kupinga biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu la Jijini Mwanza WOTESAWA limefanikiwa kuwaokoa  Zaidi ya watoto 900 waliokuwa wakifanya kazi za majumbani chini ya miaka 14.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari wakati wa maadhimisho ya miaka 10 kuanzishwa kwa  shirika hilo novemba 9, 2021 Mkurugenzi wa shirika Anjela Benedicto ameyataja hayo kama sehemu ya mafanikio ya shirikia hilo, pamoja changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.

Mbali na mafanikio hayo amesema kupitia wafadhili mbalimbali shirika limeweza kuwapa ujuzi watoto katika fani mbalimbali ikiwemo utengenezaji wa nywele na kuwawezesha kufungua ofisi zao huku wengine wakipata wafadhili kwa ajili ya kuendelea na masomo.

“watoto hawa baada ya kuwaokoa tuliwapa msaada wa kisheria, wengine tumewawezesha kimafunzo yakiwemo ya kiuchumi mfano mafunzo ya saluni na hivi tunavyozungumza wapo ambao wameshaacha kazi za ndani na kuajiriwa na wengine  wamefungua ofisi zao.” Alisema

Aidha amesema bado jamii haijamthamini sana mtoto wa kike na ndo maana matukio mbalimbali ya ukatili yanaendelea kujitokeza likiwemo hilo la kuwatumikisha kwani baadhi ya jamii hasa akina baba kukwepa majukumu yao ikiwemo kutunza familia hivyo mtoto wakike hutumiaka kama sehemu ya kipato cha familia.

“Unajua hili suala sio la mtu mmoja tunapaswa kushirikiana kwa pamoja, nasi kama Wote sawa tumekuwa tukishirikiana na taasisi nyingine katika kuhakikisha tunawalinda hawa watoto mfano wakati Fulani tulikutana na watoto ambao wanatoka nje ya nchi hivyo kwa kushirikiana na mamlaka nyingine tunafanikisha kuwarejesha watoto hawa.” Aliongeza.

Akizungumzia ziara ya Balozi wa Marekani katika kituo hicho amesema ujio wa balozi huyo ni fursa ya kipekee kwao kutembelewa na ugeni huo ni fahari na faraja kubwa sana kwao, wakiamini kwamba ni mwanzo mzuri wa mafanikio makubwa ya shirika hapo baadae.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel  aliyeambatana na ugeni huo, aliitaka jamii kutokalia kimya matukio yoyote ya ukatili yanayofanyika na hivo taarifa ziweze kutolewa ili kukomesha vitendo hivyo.  

“Sisi kama Serikali tutashirikiana nae, na niwaombe mtoe taarifa mtakapoona mtoto mwenye umri wa kwenda shule hapatiwi haki hiyo na endapo mtaona mtoto anatumikishwa kwa namna yoyote ile basi mtoe taarifa kwa mamlaka husika ili waweze kurejeshwa kwenye familia zao.” Alisema

Aidha amelipongeza shirika la wote sawa kwa kushirikiana pamoja na Serikali na wanapata faraja sana kuona Mkoa unakuwa na vituo vya makimbilio kwa watoto ambao wamekuwa wakikutana na changamoto mbalimbali kutoka kwenye jamii.

Akizungumza na wafanyakazi na viongozi wa shirika hilo Balozi wa Marekani hapa nchini Donald Wright awali alimpongeza Mkurugenzi wa shirikia hilo kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha watoto wanapata haki yao na kuwa na maono hayo makubwa kwa kipindi cha miaka 10.

“Nichukue nafasi hii kukupongeza Anjela kwa maono haya makubwa ya kuhakikisha unawajengea uwezo watoto na hasa wanawake katika Nyanja mbalimbali hasa katika kuwapatia ujuzi kupitia fani mbalimbali, najua kuna changamoto nyingi sana katika kufanikisha hili lakini hongera kwa namna ambavyo umelianzisha na unavyoendelea kulisimamia.” Alisema Balozi Donald Wright

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com