METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, November 29, 2021

RAS SINGIDA - JUKUMU LA KUSIMAMIA MIRADI YA MAENDELEO NI LA KILA MTU

 Na Hamis Hussein - Singida

Watendaji wa Serikali katika ngazi ya Kata, Tarafa na vijiji mkoani Singida wametakiwa kutumia muda wao mwingi katika kusimamia ujenzi wa vyumba vya madarasa unao endelea katika maeneo mbalimbali mkoani hapa ili kufanikisha ujenzi huo kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa.

Mkoa wa Singida umepokea fedha za UVIKO 19 kiasi cha Sh.Bilioni 13.24 kwa upande wa elimu ili kujenga  vyumba vya madarasa 632 ambapo vyumba 330 ni kwa ajili ya shule za sekondari na 330 shule za msingi pamoja na  mabweni mawili (2) kwa ajili wenye mahitaji maalum ikiwa ni  matarajio ya Serikali kwamba fedha hizo zitasimamiwa na kukamilisha ujenzi huo.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorthly Mwaluko akiwa kwenye ziara ya kutembelea miradi ya ujenzi wa vyumba vitano (5) vya madarasa katika shule ya Sekondari Ibaga iliyopo Kata ya Ibaga mkoani Singida

Kauli hiyo imetolewa na  Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida  Dorothy Mwaluko, Novemba 29, 2021 wakati wa akikagua miradi mbalimbali ya ujenzi wa vyumba hivyo katika Wilaya ya Mkalama ambapo amebainisha kuwa hali ya ujenzi inaenedela vizuri na vyumba vingi vikiwa vimefikia katika hatua ya lenta na vingine vikisubiri kupauliwa.

RAS huyo wa mkoa wa singida  akawataka viongozi  wa Serikali kuanzia watendaji wa vijiji, Kata na Tarafa kuhakikisha haipiti siku bila kujua kinachoendelea katika miradi hiyo ambayo inatakiwa kukamilika kabla ya  tarehe 15 Desemba mwaka huu.

Ziara hiyo ya RAS imehusisha viongozi mbalimbali  wa Wilaya ya Mkalama ambapo walitembelea Miradi katika shule ya Ibaga Kata ya Ibaga ambapo kunajengwa vyumba vitano (5) vya madarasa, Shule ya Sekondari Nduguti kunakojengwa vyumba viwili (2), Shule ya Sekondari Gunda Kata ya Ilunda kunakojengwa chumba kimoja, Shule ya Sekondari Grace Mesaki kunakojengwa chumba kimoja, Kikhonda  Sekondari kwenye ujenzi wa vyumba vitatu (3) na Shule ya Sekondari Iguguno kunakojengwa vyumba vine (4) vya madarasa .

Akiwa katika ziara ya kukagua miradi hiyo Dorothy Mwaluko akatuma ujumbe kwa wakuu wa shule zote mkoani Singida zenye miradi inayotumia fedha za UVIKO 19 kuhakikisha wanajenga kwa kufuata michoro iliyokubalika na kuhakikisha kwamba wanafanya mawasiliano ya karibu na wahandisi wa Halmashauri za wilaya zao endapo kuna umuhimu wa kufanya hivyo ili kulinda ubora na viwango vilivyotajwa na wataalamu hao.

Aidha RAS akawataka viongozi kuhakikisha wanazishirikisha kamati za ujenzi wa madarasa  na kamati za mapokezi ya vifaa vya ujenzi, kiasi cha fedha zilizokuja na namna ya matumizi ya fedha hizo kama sehemu ya kuweka uwazi na kutengeneza dhana ya  ushirikishwaji.


RAS Singida Dorthly Mwaluko akitoa maelekezo kwa viongozi mbalimbali wa vijiji na Kata kuhusu usimamizi wa ujenzi wa miradi ya vyumba vya madarasa kupitia fedha za UVIKO 19.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo amesema wilaya imepokea fedha kwa ajili ya ujezi wa vyumba vya madarasa 63 na ya shule shikizi 16 ambazo kwa jitihada wanazofanya vyote vitakamilika ndani ya wakati.

Dc Sophia akabainisha kwamba hali ya ujenzi kwa sasa inaendelea vizuri baada ya kumaliza changamoto ya upatikanaji wa vifaa vya ujenzi ambavyo amesema vilikuwa havipatikani kwa kuwa zoezi la ujenzi wa vyumba vya madarasa unafanyika nchi nzima hivyo kusababisha changamoto za upatikanaji wa vifaa hivyo.

Amesema kwa sasa Wilaya imeshanunua vifaa vyote vinavyo hitajika katika ujenzi huo ambapo amebainisha kwamba 85% ya majengo yamefikia hatua ya  kufungwa lenta wakati asilimia 15% vinafungwa mkanda wa katikata ili kuondoa nyufa zinzoweza kutokea.

DC amefafanua kwamba mbao zitakazotumika kwa wilaya nzima tayari zimeshafika  kilichobaki ni kuzisambaza kwenye mashule mbalimbali na mpaka kufikia kesho jioni mabati nayo yatakuwa yamefika alibainisha Dc Sophia.

Wakimalizia ziara hiyo katika shule Sekondari Iguguno DC Sophia akazitaka kamati za mapokezi na za ujenzi kujipanga kupokea vifaa hivyo ambapo watatakiwa  kuongeza usimamizi ili kupata thamani ya fedha zilizotumika.

Mwisho DC Kizigo akamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassani kwa kutoa fedha hizi katika Wilaya ya Mkalama jambo ambalo amesema limeondoa kabisa changamoto ya uhaba wa madarasa.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com