METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, November 29, 2021

SERIKALI ITATENDA HAKI KUPATA WASHINDI WA TUZO ZA FILAMU 2021

  

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amesema Serikali itatenda haki katika mchakato wa kuwapata washindi wa tuzo za filamu kwa mwaka 2021.

Waziri Bashungwa ametoa kauli hiyo katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Mbeya wakati akielezea  maandalizi ya kilele cha Tamasha la Tuzo za Filamu Tanzania 2021.

“Kwa kuzingatia ukweli kwamba hizi ni Tuzo za kwanza za Serikali, hivyo Serikali haitakuwa sehemu ya kumnyima mtu haki ya ushindi kama kweli anastahili kushinda pasipo kutazama jina au umaarufu wa mtu, hata Wasanii wachanga wana haki ya kushinda Tuzo hizi”. Alisema Mhe. Bashungwa.

Waziri Bashungwa alieleza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imeanzisha Tuzo hizo kwa mara ya kwanza kwa lengo la kutambua mchango wa Wanatasnia ya Filamu nchini ambapo kilele  kitafanyika Desemaba18, 2021jijini Mbeya katika ukumbi wa Tughimbe.

Akielezea sababu ya kilele cha Tuzo hizo kufanyika jijini Mbeya amesama ni kutambua uwepo wa Wanatasnia ya Filamu pamoja na Wasanii wengine kwa ujumla wake Jijini humo, pamoja na kufungua milango ya fursa mbalimbali zilizoko Mbeya ikiwemo kutumia Tuzo hizo kuonesha vivutio mbalimbali vya Utalii vinavyopatikana jijini humo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera amesema kupitia tuzo hizo ni fursa ya kipekee kwa wadau wa maendeleo kutembelea Mkoa wa Mbeya kujionea uzuri wake na kuwekeza katika sekta mbalimbali.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com