METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, August 17, 2021

UJENZI WA MAJENGO YA GHOROFA MTUMBA WASHIKA KASI

Katibu wa kikosi kazi cha Taifa cha kuratibu Serikali kuhamia Dodoma na ujenzi wa mji wa Serikali Mtumba Bwana Meshack Bandawe akiongoza Kikao cha wakurugenzi wa utawala na rasilimali watu wa Wizara zote kwa ajili ya kujadili utekelezaji wa ujenzi wa ofisi za ghorofa za wizara zitakazojengwa awamu ya pili katika mji wa Serikali.

Wakurugenzi wa utawala na rasilimali watu wa Wizara zote  wakiangalia wasilisho la michoro ya usanifu na ubunifu wa mji wa serikali na majengo ya wizara yatakayojengwa awamu ya pili katika mji huo wakati wa kikao cha kujadili utekelezaji wa ujenzi wa ofisi za ghorofa za wizara kilichofanyika Mtumba  Dodoma.

Katibu wa kikosi kazi cha Taifa cha kuratibu Serikali kuhamia Dodoma na ujenzi wa mji wa Serikali Mtumba Bwana Meshack Bandawe akiwa katika picha ya pamoja na wakurugenzi wa utawala na rasilimali watu wa Wizara zote baada ya kikao cha kujadili utekelezaji wa ujenzi wa ofisi za ghorofa za wizara zitakazojengwa awamu ya pili katika mji wa Serikali.

Katibu wa kikosi kazi cha Taifa cha kuratibu Serikali kuhamia Dodoma na ujenzi wa mji wa Serikali Mtumba Bwana Meshack Bandawe  amekutana na wakurugenzi wa utawala na rasilimali watu wa Wizara zote ili kujadili  maandalizi na utekelezaji wa ujenzi wa ofisi za ghorofa za Wizara zitakazojengwa awamu ya pili katika mji wa Serikali Dodoma.

Kikao hicho ni kufuatia maelekezo ya Mhe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyezitka Wizara kuanza taratibu za ujenzi wa ofisi za awamu ya pili baada ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kutoa kiasi cha shilingi bilioni 300 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa miundombinu na majengo ya ghorofa yatakayotumiwa na wizara mbalimbali katika mji wa Serikali Mtumba.

“Kwakuwa wakurugenzi wa utawala na rasilimali watu wa Wizara ndiyo timu ya ufundi ya usimamizi wa ujenzi na wasaidizi wa makatibu wakuu ni vyema tukajipanga kikamilifu ili kutekeleza ujenzi kwa tija, ufanisi, ubora, muda, kanuni, taratibu  na kwa mujibu wa bajeti iliyotengwa na Serikali” alisema bwana Bandawe katika kikao hicho.

Kwa mujibu wa bwana Bandawe, kikao hicho pia ni maandalizi ya vikao vitakavyofuata vya makatibu wakuu na mawaziri kwa ajili ya kupokea maagizo na maelekezo ya Serikali katika kutekeleza shughuli za ujenzi kwa ufanisi.

Awamu ya kwanza ya ujenzi wa mji wa Serikali ilikamilika Aprili, 2019 na kuwezesha Wizara na taasisi mbalimbali kuhamishia ofisi zake mkoani Dodoma ambapo ujenzi wa awamu ya pili ya mji huo unatarajiwa kuanza muda wowote kuanzai sasa baada ya Serikali kutoa pesa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi huo.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com