Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na wawakilishi wa Makampuni ya Upangaji, Upimaji pamoja na Watendaji wa Sekta ya Ardhi nchini wakati wa kikao kilichofanyika jijini Dodoma leo Tarehe 17 Agosti 2021.
Sehemu ya wawakilishi wa Makampuni ya Upanagaji, Upimaji pamoja na Watendaji wa sekta ya ardhi wakiwa katika kikao na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi leo tarehe 17 Agosti 2021.
Sehemu ya wawakilishi wa Makampuni ya Upanagaji, Upimaji pamoja na Watendaji wa sekta ya ardhi wakiwa katika kikao na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi leo tarehe 17 Agosti 2021.
Na Munir Shemweta, DODOMA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ametangaza kupunguzwa gharama za urasimishaji makazi holela kutoka shilingi 150,000 hadi 130,000 na kusema kila mmiliki wa ardhi anayeishi mjini sasa lazima awe na hati.
Aidha, Waziri Lukuvi alisema wananchi wasio na uwezo wa fedha kwa ajili ya zoezi hilo sasa watakopeshwa na Benki ya NMB ambayo imeingia makubaliano na Wizara ya Ardhi kwa ajili ya zoezi hilo.
Alisema, si suala la hiari mmiliki wa ardhi kuwa na hati bali ni lazima na kubainisha kuwa katika kipindi cha miezi mitatu taratibu za kutambua maeneo ya urasimishaji zifanyike ili kuanza zoezi.
Zoezi la urasimishaji makazi holela limenzishwa kwa ajili ya kutambua maeneo yaliyojengwa kihole bila kufuata taratibu za mipango miji na zoezi hilo lilianza mwaka 2013 na kutarajiwa kukamilika 2023.
Awali katika katika zoezi hilo, wananchi walitakiwa kulipia kwa viwango tofauti kuanzia 350,000, 250,000 na baadaye Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alipunguza hadi kufikia 150,000.
Akizungumza na makampuni ya Upangaji, upimaji na watendaji wa sekta ya ardhi mkoani Dodoma leo tarehe 17 Agosti 2021, Waziri Lukuvi alisema, zoezi hilo ni la lazima na kila mwananchi mwenye nyumba au kiwanja anayeishi mjini lazima awe amemilikishwa na kupatiwa hati.
“Uhamasishaji lazima ufanyike ili wananchi wajue kama wanapaswa kuingia katika zoezi hilo na kuelewa umhimu wa upatikanaji miundombinu, mfumo wa ukusanyaji na utumiaji fedha za urasimishaji makazi holela katika maeneo mbalimbali haukuwa mzuri na kwa kiasi kikubwa umekwamisha zoezi kwenda kwa kasi ” alisema Lukuvi
“Tumekwama muda mrefu katika urasimishaji na sasa tumekubaliana na Benki ya NMB iwakopeshe na kulipa kwa riba ya asilimia 10” alisema Lukuvi
Aidha, Waziri wa Ardhi aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri za wilaya kuanza kutambua na kuanisha makampuni yatakayofanya kazi za urasimishaji kwa kuangalia uwezo wa kila kampuni na kuunda kamati ya urasimishaji ya mtaa na kuanza zoezi.
“Mtakaoenda kufanya kazi lazima mfanye tathmini ya kazi au miradi iliyofanyika kwenye maeneo yenu ili kuona kazi zilizofanyika na zile zilizoshindwa kufanyika” alisema Lukuvi.
Akifafanua zaidi, Lukuvi alisema baada ya kukamilika zoezi la utambuzi, Benki ya NMB itatoa mkopo wa shilingi 130,000 na katika fedha hizo kampuni itapewa 120,000 huku 6000 ikienda halmashauri kwa ajili ya miundombinu ya barabara na nyingine ikibaki kwa halmashauri kwa ajili taratibu za hati.
Hata hivyo, Lukuvi alitoa angalizo kwa kusema kuwa, kuna baadhi ya mitaa wananchi wake tayari wameshatoa fedha kwa ajili ya zoezi la urasimishaji hivyo watendaji wa sekta ya ardhi wanatakiwa kufanya ukaguzi ili wananchi wasije kutoa fedha mara mbili.
” Nitoe angalizo kule katika mitaa kuna fedha zimetolewa na baadhi ya wananchi kwa ajili ya urasimishaji hivyo mkafanye ukaguzi ili wananchi wasije kuchangishwa mara mbili na hili siyo zoezi jipya na kama mtu ametoa 70,000 basi iongezwe ili itimie 130,000 na fedha zote zipitie benki ya NMB na mkopo uatarejeshwa katika kipindi kisichozi miezi 24″ alisema Lukuvi.
Waziri Lukuvi alisema, ni lazima wananchi wakopeshwe fedha ili wakalipie gharama zote za urasimishaji na kuwataka watendaji wa sekta ya ardhi kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wananchi wanapata na hati sambamba na kila mtaa kuwa na uhakika miundombinu ya barabara.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi Deogratias Kalimenze alizitaja baadhi ya changamoto zilizochangia kuzorota kwa zoezi hilo kuwa ni uhaba wa fedha za utekelezaji miradi, kampuni kuwa na mitaa mingi kuliko uwezo, uchangiaji fedha usioridhisha pamoja na baadhi ya kampuni kutokuwa na mitaji.
Kwa Mujibu wa Kalimenze hangamoto nyingine ni ufuatiliaji hafifu kwa baadhi ya watendaji wa sekta ya ardhi, baadhi wananchi kukataa kuachia maeneo kwa ajili ya huduma za jamii pamoja na baadhi ya ofisi kuchelewesha kazi za uidhinishaji michoro.
0 comments:
Post a Comment