Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Jijini Dar es salaam Ndg John Lipesi Kayombo leo Octoba 13, 2017 amefanya kikao Maalumu na wamiliki wa Nyumba za kulala wageni na Hoteli.
Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Manispaa hiyo uliopo kata ya Kibamba Mtaa wa kibamba Chama kilikuwa na lengo la kutoa uelewa juu ya kodi na tozo mbalimbali za Serikali zinazokusanywa na Manispaa ya Ubungo ikiwa ni pamoja na kutoa Elimu juu ya ulipaji wa Kodi na tozo za Serikali.
Kikao hicho pia kiliongozwa kwa mtazamo wa pamoja ambapo upande wa serikali ulisikiliza changamoto zinazowakabili wafanyabishara hao ambapo imeahidi kuzishughulikia haraka iwezekanavyo.
Akizungumza na wafanyabishara hao katika kikao hicho kilichohudhuriwa pia na wakuu wa Idara zote, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo alisema kuwa serikali ya awamu ya 5 inayoongozwa na Mh Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli imedhamiria kutoa huduma bora kwa Watanzania wote pasina kujali maslahi ya kisiasa, Itikadi, Dini Wala kabila.
Alisema ili kuboresha Huduma hizo mategemeo makubwa ya serikali Ni kukusanya Kodi na tozo mbalimbali hivyo alisisitiza kulipwa kwa wakati ili Manispaa hiyo ya Ubungo ambayo Ni mpya iweze kutekeleza miradi ya maendeleo kwa manufaa ya Wananchi wote.
MD Kayombo Alisema kuwa Sheria ya fedha kifungu cha 30 (D) imetoa maelekezo juu ya ushuru wa Hoteli hivyo kikao hicho kilidhamiria pia kutoa uelewa wa pamoja juu ya sheria hiyo na ushuru huo kwa undani ili utekelezaji uwe na ufanisi kwani lengo ni kuijenga Manispaa hiyo na Taifa kwa ujumla wake.
Mkurugenzi Kayombo aliwahakikishia wafanyabishara hao kuwa hoja zingine ambazo zipo chini ya mamlaka yake atazishughulikia Mara moja na zile zilizomhusu Mkuu wa Wilaya ataziwasilisha kwake kwa wakati na zile ambazo zinazomuhusu Mkuu Wa Polisi Wilaya kwamba ataziwasilishakwa Mh DC haraka kwa ajili ya utekelezaji.
Aidha, MD Kayombo Alisema kuwa kwa hoja zinazohusu serikali kuu zitafanyiwa kazi ikiwemo kuijulisha mamlaka husika iweze kuzishughulikia ikiwa ni pamoja na ombi la kulipwa kwa pamoja kodi mbalimbali anazotakiwa kulipa mfanyabiashara katika biashara zao na pia ikiwa ni pamoja na kufanyia kazi suala la ombi la elimu kwa walipa kodi ambalo ofisi ya mkurugenzi Kayombo italisimamia kikamilifu.
Pia amewataka wamiliki hao kuwa wavumilivu kutokana na kile wanachoona kama ni changamoto kutokana na mabadiliko yanayoletwa na serikali ya awamu ya tano kwani nia ni kujenga na kuleta maendeleo endelevu.
Sambamba na hayo pia MD Kayombo ametoa onyo kali dhidi ya watumishi wa Manispaa hiyo kuacha haraka vitisho kwa wafanyabiashara wote katika Manispa hiyo badala yake kutumia taaluma zao katika kuwaelewesha kila wanapokosea ili kuongeza ufanisi katika kipato Chao na Pato la serikali kwa ujumla.
Kwa upande wake Mwanasheria wa Manispaa ya Ubungo Ndg Merick Luvinga alitumia nafasi hiyo pia kutoa ufafanuzi juu ya Sheria hiyo ambapo pamoja na mambo mengine alimpongeza MD Kayombo kwa kuona umuhimu na kuamua kufanya kikao hicho ambacho kilikuwa na tija kwa kiasi kikubwa Sana kwa Wafanyabiashara hao.
Luvinga alisema kuwa ushuru huo unaotakiwa ni asilimia 10 ya mapato yanayopatikana ambapo Kati ya hayo ni mapato ya vyumba pekee ambayo hayahusishi mapato ya "BAR" au Kumbi iwapo hoteli inatoa huduma hizo.
Katika Kikao hicho wamiliki wa Hoteli na nyumba za kulala wageni walipata fursa ya kuuliza maswali na kutoa maoni yao juu ya Sheria hiyo ikiwa ni pamoja na kutaka kufahamu juu ya viwango vya ushuru katika maeneo yote hayo.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara hao Katibu wa Umoja wa wamiliki wa Hoteli na Nyumba za kulala wageni Mzee Lema amemshukuru Mkurugenzi Kayombo kwa kikao hicho huku akikiri kuwa ni jambo ambalo halijawahi kufanyika tangu wameanza biashara zao miaka ya 80's
Alisema Mkurugenzi huyo ameonyesha kuwa ni kiongozi imara Huku akiahidi mbele ya kikao hicho kutoa ushirikiano wa dhati katika kila hatua ya kuijenga Manispaa ya Ubungo na Kulipa Mapato hayo ya Hotel levy kwa wakati.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment