Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
WAZIRI wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda anasema wakati
akilihutubia bunge kwa mara ya kwanza Rais wa Awamu ya sita Samia Suluhu Hassan
alitumia takribani asilimia 14 ya mambo yote aliyozungumza kwenye masuala ya
kilimo.
Hayo aliyabainisha hivi karibuni wakati akitoa maelezo
kuhusu siku 100 za Rais Samia akiwa madarakani tangu kifo cha Rais wa awamu ya
tano, Hayati Rais John Magufuli kitokee.
Waziri huyo anasema jambo moja ambalo Rais, alilitamka ni
umuhimu wa kuongeza tija katika kilimo kwakuwa bila kufanya hivyo nchi inaweza
isiende vizuri kwenye sekta hiyo.
Alitolea mfano kuwa sasa hivi kwenye kahawa uzalishaji
unaweza kuongezwa tija mara tatu ya kahawa inayozalishwa kwa sasa licha ya kuwa
kwa sasa tija ni ndogo hivyo kupatikana theluthi tuu ya uzalishaji.
Amesema kwa upande wa Pamba kwenye hekari moja unapata
takribani kilo 200 mpaka 350 lakini kwa nchi nyingine za Afrika Magharibi
wanapata mpaka kilo 1000 hivyo tija bado ni ndogo.
”Bila hata kuongeza eneo la kulima tunaweza tukaongeza
uzalishaji hivyo ukienda zao moja hadi jingine unakuta kwamba tija ni ndogo
sana” Amesema
Anasema Rais Samia alielekeza nguvu kubwa ielekezwe
katika kuongeza tija hivyo bajeti ya wizara ya Kilimo iliyosomwa bungeni
imeanisha mikakati ya kuongeza tija na fedha katika maeneo ya kupaumbele.
Anaeleza waliona cha muhimu katika yote ni suala la
utafiti wa mbegu bora ambazo zinaongeza tija, na kilimo bora.
Amesema hayo ni mafanikio makubwa kwa sababu alitembelea
baadhi ya vituo vya utafiti ambavyo watu wameanza kukata tamaa na kuhisi kwamba
serikali ilikuwa ikipuuza suala hilokwa sababu hautoi matokeo mara moja hali
inayosababisha watu kutafuta vitu vyenye matokeo ya haraka.
Alisema suala la pili ni kuzalisha mbegu
bora zaidi kutokana na uhaba wake kuwa ni kikwazo kikubwa cha uzalishaji wa
tija huku akitolea mfano zao la alizeti ambalo kwa sasa serikali imekusudia
kuongeza wazalishaji nchini licha ya kutokuwepo mbegu.
”Tumeamua mashamba yote ya mawakala wa mbegu Tanzania 13
tutayafufua, kuyamawagilia ili yaanze kuzalisha mbegu ziwafikie wakulima na
tumeongeza bajeti kubwa kwenye suala la uzalishaji wa mbegu,” Alisema.
Alifafanua kuwa bajeti imeongezwa kwenye huduma ya ugani
ambayo ilikuwa milioni 603 tuu hadi bilioni 11.5 licha ya kuwa hazitoshi hivyo
nguvu itawekwa mikoa mitatu ya Dodoma, Singida na Simiyu kuonyesha namna huduma
hiyo inatakiwa ifanyike ili kuongeza tija.
Pia, alisema utaanzishwa mfuko wa umwagiliaji kwa ajili
ya kuhakikisha kwamba uzalishaji wa ekari unaongezeka.
Alieleza pamoja na mambo hayo kuna masuala ya masoko ili
kuhakikisha kwamba mkulima anapolima anaweza kuuza huku akieleza tatizo lipo la
aina mbili ambapo ni uzalishaji ambao wakulima hawajui wauze wapi bidhaa zao.
”Sasa hivi tuna mchele mwingi, mahindi lakini hatuna
wananunuzi wakutosha na ukiongea na wakulima mengine wanaona hii haitaleta
hamasa ya kuendelea na kilimo huko mbele ya safari,”alisema.
Alieleza kwenye hilo wanafanya mazungumzo na nchi
mbalimbali na mwisho wa mwezi Julai hatimaye inawezekana Sudani Kusini
wamekubali kwamba wanaweza kutupokea mwisho wa wiki ambapo wataenda na
wafanyabiashara kwa ajili ya kuangalia masoko ya huko jinsi tunavyoweza kuuza
mchele, mtama, mahindi.
Aidha, alibainisha kwa nchi za DRC, Zimbabwe wataangalia
vilevile masoko ya mchele, kwa maana umeanza kuuzwa katika nchi ya Swaziland na
wanaangalia uwezekano wa kuuza Afrika Kusini.
Alieleza hayo yote yanahitaji wajasiriamali kuchangamka
kwa kuwezeshwa kujenga mazingira bora ili wachangamkie fursa ikiwa ni pamoja na
kuchakata mazao kabla ya kuyauza maana ukitaka kuuza mchele vizuri ni lazima
uchakatwe na kupelekewa kwenye masoko ya Afrika nzima.
Alibinisha katika suala hilo la masoko ambapo wakulima
wanakosa mahali pa kuuza moja ya changamoto ilikuwa ni ndani ya nchi kwamba
wafanyabishara wa mazao walikuwa wakati mwingine wanapata usumbufu mkubwa kwa
kusimamishwa na kukamatwa hivyo kuwa kama wanafanya biashara haramu.
Alivishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwamba kwa sasa
wanasaidia biashara iende na kwamba kauli ya Rais Samia kuboresha mazingira ya
biashara inaweza kuwa imesaidia kwa namna moja ama nyingine.
”Sisi tunasema mazao sio bidhaa haramu kwahiyo acha
ziuzwe na sisi kwa kilimo tunasema acha bidhaa hizi ziuzwe popote na kwa namna yoyote
ile ili kuongeza tija na masoko,”alisema.
Alifafanua aina nyingine ya changamoto ya masoko ni pale
ambapo sisi tunahitaji mafuta ya kula lakini hatuzalishi bidhaa hiyo japo kuwa
tungeweza kulima alizeti lakini hatulimi ya kutosha na wakulima wanahitaji
fedha hivyo wangefanya hivyo wangepata fedha za kutosha.
Alieleza tunatumia nusu trilioni za fedha za nchi yetu
kwenda kununua mafuta nje ya nchi sasa hapa tumeshindwa kuzalisha kile ambacho
kinahitajika ndani ya nchi, tatizo hilo pia lipo kwenye ngano, Shayiri, hivyo
hilo nalo watapambana nalo katika mkakati wa bajeti ili kuongeza tija.
Kuhusu suala la kuwekeza mitaji na kufanyia kazi katika
kilimo na kilimo anga, alisema nzige kwa wakati fulani lilikuwa kama tatizo
kubwa ikabidi ahamie eneo la tukio ’site’ kuhakikisha kuwa suala hilo linaisha.
Alibainisha wakati wa kupambana na nzige aligundua kuwa
tatizo moja wapo ni kwamba mitaji iliyopo zinamilikiwa pamoja na nchi nyingi
huku akitolea mfano ndege za kupambana na nzige ambazo zinamilikiwa chini ya umoja
wa kupambana na nzige wa jangwani nchi ambazo zinaunganisha Tanzania, Uganda,
Kenya, Somalia, Elitrea, na Sudani Kusini.
Alisema inabidi kupeleka kule taarifa ya kutaka kuletewa
ndege hali iliyosababisha ufanisi kuwa mbaya kwa sababu ilikuwepo ndege moja
ambayo ipo Moshi lakini rubani yupo Nairobi hivyo wakaanza kuhisi kwamba kama
hali ingekuwa kubwa na tishio lingekuwa kubwa katika nchi nyingi ingekuwa ni
vigumu kugombana nao.
”Wakati wa kupambana na nzige ilikuwa changamoto kubwa
hadi uangize ndege kule inakuwa ngumu ndio maana tukaamua kujenga uwezo wa
ndani kwa kurudisha kilimo anga kwa sababu uharibifu wa mazao vilevile
unapunguza tija,”.
Alisema hayo ni masuala ambayo yamejitokeza kipindi hiki
cha siku 100 za Rais Samia ambaye anawapa watanzania matumaini makubwa katika
kilimo ndio maana fedha zimeongezwa kwa ajili ya kusukuma vipaumbele
vitakavyoongeza tija kwenye sekta hiyo.
Akizungumzia juhudi ambazo zimefanywa na Rais katika
kuimarisha mazingira ya biashara, alisema hiyo ni pamoja na nchi kuwa na amani
na utulivu, uchumi mpana ulitengamaa, kuwa na miundombinu wezesha na huduma za
kiuchumi ikiwemo nishati.
Aidha, kuwa na mfumo mzuri wa masuala ya kanuni na
usimamizi wa shughuli za kiuchumi maeneo mbayo mara nyingi yamekuwa yakitolewa
malalamiko.
Alisema nchi imeimarisha mifumo ya biashara ambapo awamu
ya tano iliwekeza zaidi kwenye miundombinu lakini Rais Samia amekuwa akitoa
matamko ya kuongeza imani ya watu ambao walikuwa wanahisi kwamba pengine dola
halitabiriki sana katika shughuli zake za uwekezaji.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment