Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akisisitiza jambo wakati wa
hafla fupi ya kuwapokea wanamichezo wanafunzi waliotoka kushiriki
mashindano ya Shule za Sekondari za Jumuiya ya Afrika Mashariki (FEASSA)
leo Jijini Dar es Salaam. Katikati ni Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo
la Taifa (BMT) Bw. Mohamed Kiganja na Mratibu wa Michezo Shule ya
Sekondari Makongo Kapteni Abdul Mbaruka Tika.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akimpongeza mmoja wa
mwanamichezo aliyeibuka mshindi wa tatu katika riadha kwenye mashindano
ya FEASSA, Winfrida Makenji wakati wa hafla fupi ya kuwapokea
wanamichezo hao waliotoka kushiriki mashindano ya Shule za Sekondari za
Jumuiya ya Afrika Mashariki (FEASSA) leo Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akipokea bendera ya taifa
kutoka kwa Kapteni wa timu ya wanafunzi wa Sekondari za Tanzania
walioshiriki mashindano ya michezo kwa Shule za Sekondari za Jumuiya ya
Afrika Mashariki (FEASSA) katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa
Idara ya Habari (MAELEZO) Jijini Dar es Salaam leo.
Mkuu wa Msafara wa timu ya
wanafunzi wa Sekondari za Tanzania walioshiriki mashindano ya michezo
kwa Shule za Sekondari za Jumuiya ya Afrika Mashariki (FEASSA) Mwl.
Vitalis Shija akielezea jambo mbele ya Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (wapili kushoto) wakati wa
hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Jijini
Dar es Salaam leo. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo
Bw. Alex Nkenyenge na Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Mohamed Kiganja. Picha na: Frank Shija – MAELEZO.
Na Thobias Robert- MAELEZO
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amewapongeza vijana walioshiriki
mashindano ya Shirikisho la Michezo Afrika Mashariki (FEASSSA)
yaliyofanyika mwaka huu katika Mji wa Gulu Nchini Uganda.
Pongezi hizo amezitoa leo Jijini
Dar es Salaam wakati akikabidhiwa bendera ya Taifa na vijana hao mbele
ya Waandishi wa Habari mara baada ya kurejea kutoka kwenye mashindano
hayo ambayo hushirikisha timu za Shule za Sekondari za jumuiya ya Afrika
Mashariki.
“Nataka kuwadhitibishia Watanzania
kwamba tutaenzi daima michezo ya UMITASHIMITA na UMISETA maana vipaji
ndiyo vinapoanzia, niwapongeze sana vijana kwa kushinda medali nawatie
moyo muendelee ili muweze kushiriki katika mashindano ya kimataifa
yakiwemo Olimpiki, maana nyninyi ndiyo warithi wa Simbu na wanariadha
wengine waliowahi kufanya vyema hapa nchini,” alisema Dkt. Mwakyembe.
Aidha Dkt. Mwakyembe amewaasa
vijana hao wasithubutu kutumia njia zisizo halali ili kushinda, bali
wajitume katika mazoezi na wawe na nidhamu ya hali ya juu kwani michezo
ni ajira ya uhakika kwa vijana wengi sio tu Tanzania bali hata katika
mataifa yote ulimwenguni.
“Tusisikie kabisa kelele za
kwamba, unaweza ukafanya hiki au ukatumia njia za mkato, hakuna mchawi
wa michezo zaidi ya mazoezi kwani huwezi kupata ushindi kwa kupitia njia
za kishirikina, haiwezekani kwani hizo ni hadithi tu za abunuwasi njia
pekee ni mzaoezi,” alisisitiza Dkt. Mwakyembe.
Vilevile Dkt. Mwakyembe amesema
kuwa serikali imejipanga mwaka ujao itaongeza idadi ya washiriki katika
mashindano yatakayofanyika Rwanda na amewasisitiza vijana pamoja na
walimu wa michezo mashuleni kuendelea kuwalea vijana na kuibua vijana
wengi ili kukabiliana na na tatizo la upungufu wa ajira kwani michezo
imekuwa ajira ya uhakika duniani.
Kwa upande wake, Vitalis Shija
Mkuu wa Msafara wa timu ya vijana iliyoshiriki mashindano hayo amesema
kuwa, Tanzania ilikuwa na wanamichezo 73, katika michezo yote
iliyoshiriki ikiwemo, Mpira wa miguu, kurusha vitu vizito pamoja na
Riadha.
Katika michezo hiyo Tanzania
imepata medali 10, kwa upande wa riadha na mchezo wa kupokazana vijiti
na kushika nafasi ya tatu, lakini pia imeshika nafasi ya tatu kwa upande
wa mashindano ya mpira wa miguu kwa wasichana na kuishia hatua ya robo
fainali kwa upande wa timu ya wavulana.
Aidha katika medali 10 Mwanafunziu
Winfrida Mkenji kutoka Shule ya Sekondari Makongo alipata medali nne,
kwa upande wa riadha na mchezo wa kupokezana vijiti Mita 100, Kefleni
Simon medali 1, Jane Maiga medali 2, Mary Emily medali 2, kwa upande wa
mita 100 na mita 400 katika mchezo wa kupokezana vijiti pamoja na Sarah
Joel medali 1 katika mchezo huohuo kwa mita 400.
“Katika mashindano hayo kuna ada
ya ushiriki kwa kila nchi pia kila mshiriki anapaswa kulipiwa dola 7 kwa
siku 10 kwahiyo unapopeleka idadi kubwa ya wanafunzi gharama
zinaongezeka hivyo nikushukuru Waziri na Baraza la Michezo kwa
kutuwezesha kuisafirisha timu na kushiriki michezo kwa siku zote,”
alifafanua Bw. Shija.
Katika mashindano hayo vijana
waliowakilisha nchi walitoka katika Shule za Alliance mkoani Mwanza,
Simiyu katika Shule ya Sekondari Mwashilole, Dar es Salaam katika Shule
ya Sekondari ya Makongo, Pwani katika Shule ya Lord Baden, Tabora katika
Shule ya Sekondari Ulaya pamoja na Mkoa wa Morogoro Sekondari ya
Treefarms.
Mashindano haya yamekuwa
yakifanyika kila mwaka katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afika
Mashariki na mwaka huu yamefanyika katika mji wa Gulu Uganda, kwa
udhamini wa kampuni ya Brokeside ambapo Uganda ilikuwa na washiriki
1045, Kenya 840, Rwanda 650, Burundi 380, Sudani Kusini 150 na Tanzania
washiriki 73.
0 comments:
Post a Comment