METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, May 16, 2021

SHAKA: Zitto Acha Ulalamishi na Siasa za Kitoto

Na Mwandishi wetu, Kigoma. 

Chama Cha Mapinduzi kimesema Kiongozi wa ACT Wazalendo Zitto  Kabwe ameanza kutapatapa na kutafuta mchawi baada ya kuona Jahazi la Chama chake likienda mrama kufuatia matokeo ya awali katika majimbo ya Muhambwe na Buhigwe, ambapo CCM imeongoza kwenye Vituo vilivyokwishatangaza matokeo kwa zaidi ya asilimi 90.

Mwenezi Shaka amesema uzushi wa Zitto ni kuelekea kufilisika kisiasa na kwamba hautakinusuru chama chake, kwani Wananchi wamemkataa Mgombea wa Chama hicho na pia hakikuwa na mtandao wa kisiasa unaoweza kukipa kura za ushindi. 

Shaka ameongeza kuwa propaganda za kale anazofanya Zitto haziwezi kubadili matokeo ya wapiga kura ya jimbo la Muhambwe na Buhingwe.

Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi wa  CCM amesema hayo jioni hii kufuatia madai ya uzushi yaliyosambazwa na Kiongozi Mkuu wa Chama Cha  Act Wazalendo Zitto Zubeir Kabwe katika mitandao ya kijamii.

Shaka alieleza kuwa ikiwa  Zitto alishindwa kupata ushindi jimbo la Kigoma mjini mwaka 2015 anaweza vipi kuwashawishi wananchi wa Buhigwe na Muhambwe kukiamini Chama chake.

Aidha, Shaka amemtaka Zitto kukomaa kisiasa na kuonyesha kupevuka, kwani kudai kuna kura feki na kwamba amevamiwa na mapanga ni propaganda nyepesi na haziwezi kukisaidia chama chake ikiwa kimeshindwa kujiandaa mapema kunadi sera, kupata Mgombea anayekubalika na kuwa na mikakati ya kampeni na ushindi.

“Chama chake kimeshindwa kuingiza timu uwanjani iliyojiandaa vizuri... sisi tumejiandaa muda mrefu na wagombea wetu wanakubalika bila shaka yoyote” alisema Shaka.

Aidha  amesema wanajiandaa mara baada kutangazwa rasmi matokeo hayo na Tume ya Uchaguzi  kuwasindikiza Wabunge wao kutoka Buhigwe na Muhambwe kwenda kuapa Bungeni kama itakavyoelekezwa na mamlaka zinazohusika.

MWISHO.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com