1.
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa
Spika, kufuatia
taarifa iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo,
Mifugo na Maji, ninaomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee Taarifa ya
Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha
2020/2021 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa
Fedha 2021/2022.
2.
Mheshimiwa
Spika, naomba hotuba yote iliyowasilishwa mezani iingie kwenye
kumbukumbu za Bunge lako Tukufu, ili mimi niokoe muda kwa kusoma tu muhtasari
wa hotuba hiyo. Aidha Hotuba yote inapatikana pia kwenye tovuti ya Wizara,
www.kilimo.go.tz
3.
Mheshimiwa
Spika, awali ya yote ninapenda tena kuungana na Wabunge wote
kutoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu
Hassan kwa msiba mkubwa tulioupata wa kuondokewa na aliyekuwa Rais wetu, Hayati
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Ninatoa pole pia kwa Mheshimiwa Janeth
Magufuli, Mama Suzana Magufuli, watoto na ndugu wote wa Hayati Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli na Watanzania wenzangu wote. Tutaenzi mchango mkubwa wa Rais
wetu wa Awamu ya Tano katika ujenzi wa Taifa letu na tutajitahidi kuendeleza
uthubutu, uchapakazi na uzalendo kama alivyotufundisha Hayati Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli.
4.
Mheshimiwa
Spika, hivi
karibuni pia tulimpoteza aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, Hayati Maalim Seif Sharif Hamad.
Maalim Seif Sharif Hamad alikuwa ni kiongozi
maarufu sana hapa nchini na atakumbukwa
kwa mengi. Tutamkumbuka sana kwa kushirikiana na Rais wa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar katika kuleta maridhiano na
mshikamano wa Zanzibar baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2020. Ninatoa pole nyingi kwa
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi, familia ya
Hayati Seif Sharif Hamad na Watanzania wenzangu wote kwa msiba huu mkubwa wa
kuondokewa na Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad.
5.
Mheshimiwa
Spika, kipindi hiki pia tumempoteza aliyekuwa Katibu Mkuu
Kiongozi, Hayati Balozi John William Herbert Kijazi. Sote tunamkumbuka Balozi
Kijazi kwa uchapakazi wake na karama yake kuu ya kuwaheshimu wote aliofanya nao kazi kwa
ukarimu, na uwezo wake mkubwa wa kuelewa na kuusimamia utumishi wa umma kwa uadilifu
Mkubwa.
6.
Mheshimiwa
Spika, Bunge lako Tukufu limepata pia pigo la kuondokewa na
wabunge watatu; Hayati Atashasta Justus Nditiye aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Muhambwe,
Hayati Martha Jachi Umbulla, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Manyara
na Hayati Khatibu Said Haji aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Konde. Ninaungana tena
na Mheshimiwa Spika na wabunge wenzangu wote kuomboleza misiba hii mikubwa.
7.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na pigo kubwa sana na huzuni kuu ya kuondokewa na
aliyekuwa Rais wetu, Taifa letu limehimili vyema kwa sababu ya misingi imara ya
kikatiba ya nchi yetu na utamaduni wa kisiasa ambao uliasisiwa na Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na Chama cha Mapinduzi. Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekamata hatamu za uongozi wa nchi yetu, na
ametuongoza na kutufariji katika majonzi na amefanikiwa kuleta matumaini
makubwa. Ninamuombea afya njema na mafanikio makubwa katika kazi hii nzito ya
kuliongoza Taifa letu.
8.
Mheshimiwa
Spika, kama nitakavyoeleza katika hotuba hii, mikakati yetu
katika sekta ya kilimo tumeipanga kwa kuzingatia maelekezo ya Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, aliyoyatoa kupitia
hotuba yake hapa Bungeni ya tarehe 22 April, 2021
9.
Mheshimiwa
Spika, ninaomba nitoe pongezi za dhati kwa Makamu wa Rais,
Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi kwa nafasi za uongozi wa juu katika
Taifa letu ambazo wameaminiwa na kukabidhiwa. Ninawaombea afya njema na
mafanikio makubwa katika kutekeleza
majukumu haya makubwa.
10. Mheshimiwa Spika, ninampongeza
pia Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa
Majaliwa, kwa kuendelea na wadhifa wake huo
katika uongozi wa awamu ya sita, na ninamshukuru kwa kutusimamia na
kutuongoza vizuri.
11. Mheshimiwa Spika, pongezi
nyingi pia kwa Spika, Mheshimiwa Job Ndugai na Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt.
Tulia Ackson kwa kuchaguliwa kuendelea kuliongoza Bunge hili tukufu.
Ninawapongeza wabunge wenzangu wote kwa kuaminiwa na vyama vyetu na kuchaguliwa
kuwa wabunge. Kwa namna ya kipekee nawapongeza waheshimiwa Eliadory Felix
Kavejuru na Dkt. Florence George Samizi kwa kuchaguliwa kuwa wabunge wa majimbo
ya Buhigwe na Muhambwe mtawalia.
12. Mheshimiwa Spika, mimi
binafsi ninakishukuru sana Chama cha Mapinduzi kwa kuniteua kugombea ubunge
katika Jimbo la Rombo na ninawashukuru sana wananchi wa Rombo kwa kunichagua.
Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniteua kuwa Waziri wa Kilimo. Naahidi kwa
Chama cha Mapinduzi, Mheshimiwa Rais, wananchi wa Rombo na Watanzania wote kwa
ujumla kwamba nitatumikia nafasi za ubunge na uwaziri kwa bidii, maarifa,
weledi na uadilifu.
13. Kwa namna ya pekee namshukuru sana mke wangu, Beatrice,
na familia yangu kwa ujumla kwa upendo na uvumilivu wao wakati wote.
14. Mheshimiwa Spika,
ninapenda pia kutoa shukrani zangu za dhati kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, chini ya uenyekiti wa Mheshimiwa Dkt.
Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, na Makamu Mwenyekiti wake,
Mheshimiwa Almas Athumani Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kwa ushirikiano
mzuri na ushauri makini ambao wameendelea kuutoa kwetu katika kupitia Taarifa
ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Mwaka 2020/2021 na Mpango wa Bajeti ya
Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2021/2022. Ushauri wao umezingatiwa na tunaahidi
kuendelea kushirikiana kwa karibu na Kamati katika kuendeleza kilimo hapa
nchini.
15. Mheshimiwa Spika, kwa
namna ya pekee ninawashukuru viongozi na watumishi wote wa Wizara ya Kilimo kwa
ushirikiano wao na bidii yao katika kazi na maandalizi ya hotuba hii. Ninamshukuru sana Naibu Waziri wa
Kilimo, Mheshimiwa Hussein Mohamed Bashe (Mb), kwa jinsi tunavyosaidiana kwa
karibu katika kutekeleza majukumu ya Wizara tuliyokabidhiwa. Ninamshukuru
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Andrew Wilson Massawe na Naibu Katibu
Mkuu, Profesa Siza Donald Tumbo kwa kazi nzuri na ushirikiano mkubwa ambao wao
pamoja na wakurugenzi, wakuu wa taasisi, Bodi na Wakala zilizo chini ya Wizara
na watumishi wote wa Wizara kwa ushirikiano
wanaoendelea kuutoa.
16. Mheshimiwa Spika, nitakuwa
mchoyo wa fadhila nisipomshukuru aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw.
Gerald Musabila Kusaya ambaye kwa sasa ni Kamishna Jenerali wa Tume ya Kudhibiti
Madawa ya Kulevya kwa kunikaribisha na kufanya naye kazi kwa karibu kwa kipindi
chote nilichokuwa naye Wizarani.
2.
MCHANGO WA KILIMO KATIKA UCHUMI MWAKA 2020
17. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020, mchango wa kilimo katika Pato la
Taifa (GDP) ulikuwa ni asilimia 26.9. Aidha, katika kipindi hicho, sekta ya
kilimo imekua kwa asilimia 4.9 ikilinganishwa na asilimia 4.4 ya mwaka 2019. Vilevile,
uzalishaji wa sekta ndogo ya mazao umekua kwa asilimia 5.0 ikilinganishwa na
ukuaji wa asilimia 4.4 katika mwaka 2019. Pia, katika mwaka 2020, sekta ya
kilimo imechangia kwa asilimia 58.1 katika kutoa ajira nchini na kuchangia
zaidi ya asilimia 65 ya malighafi za viwanda nchini.
3. MAPATO
NA MATUMIZI KWA MWAKA 2020/2021
3.1 Makusanyo
ya Maduhuli
18.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2020/2021, Wizara ilikadiria kukusanya Shilingi bilioni 5.79 kutokana na vyanzo mbalimbali. Hadi Aprili 2021, Wizara imekusanya Shilingi bilioni
2.69 sawa na asilimia 46.48 ya makadirio.
3.2
Fedha
Zilizoidhinishwa
19. Mheshimiwa Spika, Wizara
ya Kilimo kupitia Fungu 43, Fungu 05 na Fungu 24 iliidhinishiwa Shilingi
bilioni 229.83. Kati ya fedha hizo
Shilingi bilioni 79.76 ni za
matumizi ya kawaida na Shilingi bilioni 150.07
za miradi ya maendeleo.
20. Mheshimiwa Spika, Wizara
ya Kilimo (Fungu 43) iliidhinishiwa Shilingi bilioni 202.50 ambapo Shilingi bilioni 65.23
ni fedha za matumizi ya kawaida na Shilingi bilioni 137.27 ni fedha za maendeleo. Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (Fungu
05) iliidhinishiwa Shilingi bilioni 17.72
ambapo Shilingi bilioni 4.92 ni za
matumizi ya kawaida na Shilingi bilioni 12.80
ni za miradi ya maendeleo. Tume ya Maendeleo ya Ushirika (Fungu 24) ilitengewa
Shilingi bilioni 9.60 kwa ajili ya
matumizi ya kawaida.
4.0 UTEKELEZAJI WA MALENGO MKAKATI KWA MWAKA 2020/2021
21. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2020/2021,
umezingatia yafuatayo:-
i. Ilani ya Chama cha
Mapinduzi mwaka 2015 – 2020;
ii. Mpango wa Maendeleo wa
Taifa wa Miaka mitano Awamu ya Pili (2015/2016- 2020/2021); na
iii. Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II).
22. Mheshimiwa Spika, miongozo hiyo, imezingatiwa katika kuboresha mifumo ya Kitaasisi,
Bodi na Sheria za Kilimo; kuunganisha wakulima wadogo na wakulima wakubwa; ujenzi
na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji, ghala na masoko, kuimarisha upatikanaji wa pembejeo na huduma
za ugani; kuimarisha maendeleo ya ushirika; Kuongeza matumizi ya teknolojia
bora; kuimarisha Vituo vya Utafiti, Vyuo vya Mafunzo na Vituo vya Wakulima; na
huduma za upimaji wa matabaka na ubora wa udongo.
4.1
Kuboresha Mifumo ya Kitaasisi, Bodi na Sheria za Kilimo
Mifumo ya
Kielektroniki ya kutoa huduma katika Sekta ya Kilimo
23. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutumia Mfumo
wa Utoaji wa Vibali kwa njia ya Kielektroniki (ATMIS), Mfumo wa Usajili wa Wadau wa Sekta ya Kilimo na Mfumo wa
M-Kilimo (Mobile – Kilimo). Mifumo hiyo imerahisisha utoaji wa
huduma zikiwemo vyeti vya usafi wa mazao ya mimea na vibali vya kuingiza na
kuuza mazao nje ya nchi kwa wakati; huduma za ugani; usajili wa wadau wa sekta
ya kilimo; na upatikanaji wa takwimu za kilimo.
4.2
Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Umwagiliaji, Masoko na uhifadhi
wa Mazao ya Kilimo
24. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Tume ya
Taifa ya Umwagiliaji imeendelea na ukarabati na ujenzi wa miundombinu ambapo
skimu 13 kupitia mradi wa SSIDP na skimu tano (5) kupitia mradi wa ERPP
zimekamilika. Vilevile, Tume kupitia IDF imekamilisha
ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji iliyoharibiwa na mafuriko katika skimu
ya Ruaha Mbuyuni
(Kilolo). Aidha, ukarabati wa Skimu za Mlenge na Magozi (Iringa DC) umefikia asilimia
80.
25. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mradi wa Kuongeza Uwezo wa
Kuhifadhi unaotekelezwa na NFRA inaendelea kujenga vihenge vya kisasa katika maeneo ya
Babati, Shinyanga, Songea, Makambako, Mbozi, Sumbawanga, Mpanda na Dodoma ili kuongeza
uwezo wa kuhifadhi nafaka kutoka tani
250,000 hadi tani 501,000 ambapo hadi Mei 2021, ujenzi umefikia asilimia
80.1.
4.3 Kuimarisha Uzalishaji wa Mbegu Bora za Mazao na Upatikanaji wa Pembejeo
a)
Mbegu bora
26. Mheshimiwa Spika, hadi Aprili, 2021 upatikanaji wa mbegu bora
nchini umefikia tani 50,589.43 zisizojumuisha miche, vikonyo na vipando ambapo tani 27,330.37
zimezalishwa nchini, tani 15,758.92 zimeingizwa kutoka nje na tani 7,500.14 ni bakaa ya msimu 2019/2020.
27. Aidha, TARI kwa kushirikiana na wadau imezalisha na kusambaza miche milioni 13.56 ya mazao ya viazi vitamu,
zabibu, minazi, parachichi, miwa, mkonge na pingili za muhogo
milioni 40.9. Vilevile, ASA
imezalisha miche 342,000 ya michikichi.
b) Upatikanaji wa
Mbolea
28. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu uzalishaji na uingizwaji wa mbolea nchini
ambapo hadi Aprili 2021, upatikanaji umefikia tani 678,017 sawa na asilimia
94.4 ya mahitaji ya tani 718,051 msimu wa 2020/2021. Kati ya kiasi hicho tani
426,572 zimeingizwa kutoka nje ya nchi, tani 32,239 zimezalishwa nchini na tani
219,206 ni bakaa ya msimu wa 2019/2020.
c)Upatikanaji wa Viuatilifu vya Mimea na Mazao
29. Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2021, upatikanaji wa viuatilifu vya
kudhibiti visumbufu vya milipuko umefikia lita 113,000 na kilo 5,000. Kati ya
hizo, lita 100,000 ni kwa ajili ya kudhibiti viwavijeshi, lita 5,000 kweleakwelea
na lita 7,000 nzige, lita 1,000 nzi wa matunda na kilo 5,000 za kudhibiti panya.
d) Udhibiti wa
Visumbufu vya Mimea na Mazao
30. Mheshimiwa Spika, Wizara
imedhibiti makundi ya nzige wa jangwani, kwelea kwelea na panya. Wizara
imefanikiwa kudhibiti makundi yote ya nzige wa jangwani waliovamia nchi yetu
pamoja na nzige wachanga walioanguliwa katika Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na
Manyara.
31.
Mheshimiwa Spika, naomba
nitumie Bunge lako Tukufu kuwashukuru Mhe. Dkt. Anna Mgwira aliyekuwa Mkuu wa
Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Idd Kimanta aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Mhe.
Joseph Mkirikiti aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, wakuu wa Wilaya za
Simanjiro, Siha, Longido na Monduli, Waheshimiwa Wabunge na wananchi wa Wilaya husika
kwa ushirikiano wao katika kupambana na nzige. Aidha, nitoe shukrani za dhati
kwa Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Anga na hasa Meneja wa Kiwanja cha Ndege Arusha,
Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja
wa Mataifa (FAO) kwa ushirikiano wao katika zoezi la kudhibiti nzige hao.
4.4 Kuimarisha Usimamizi wa Maendeleo ya Ushirika
32. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara kupitia Tume ya Maendeleo
ya Ushirika
imekagua Vyama vya Ushirika 4,494 kati ya 9,185. Aidha, kaguzi maalum zimefanyika kwa
vyama 35 na hatua stahiki zimechukuliwa kwa waliojihusisha na wizi na
ubadhilifu wa mali na fedha za vyama vya ushirika.
33. Mheshimiwa Spika, Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa
Vyama vya Ushirika (COASCO) limekagua vyama vya ushirika 6,021 na Serikali
imechukua hatua stahiki kwa vyama vyote ambavyo vimebainika kuwa na ubadhirifu
wa fedha na mali za vyama.
34. Mheshimiwa Spika, Tume imefuatilia mali za Vyama vya
Ushirika zilizochukuliwa kinyume na utaratibu ambapo mali zenye thamani ya Shilingi Bilioni 68.9 zimerejeshwa.
Aidha, Tume imehamasisha uanzishwaji wa Viwanda
vya kuchakata mazao ambapo viwanda vimeongezeka kutoka 374 mwaka 2019 hadi 452
mwaka 2020. Pia, ajira katika Vyama vya Ushirika imeongezeka kutoka 90,090
mwaka 2019 hadi 100,100 mwaka 2020.
4.5 Kuongeza Matumizi ya Teknolojia Bora katika Uzalishaji wa Mazao
Zana za Kilimo
35. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 matumizi ya trekta
yameongezeka kutoka asilimia 20 mwaka 2019 hadi asilimia 23 mwaka 2020. Ongezeko hilo limepunguza matumizi ya jembe la mkono
kutoka asilimia 53 mwaka 2019 hadi asilimia 50 mwaka 2020. Katika kipindi hicho
sekta binafisi imeingiza matrekta makubwa 1,124 na matrekta madogo ya mkono 459
nchini.
Huduma za Ugani
36. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha huduma za ugani Wizara imeandaa rasimu ya Mwongozo wa
Usimamizi na Uratibu wa Huduma za Ugani utakaotumiwa na sekta ya umma na
binafsi ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
37. Mheshimiwa Spika, Wizara
kupitia TARI imetoa mafunzo kuhusu teknolojia bora za kilimo kwa wakulima
51,304 na Maafisa Ugani 982 kupitia vituo 11 vya TARI na Kituo cha Usambazaji
wa Teknolojia (Nyakabindi AgriTecH). Wizara pia, imeratibu maonesho ya wakulima
(Nanenane) ambapo wadau 2,253 na Wakulima 1,250 walijifunza teknolojia bora za kilimo na
fursa za masoko.
Uzalishaji wa
Mazao
38. Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2020/2021, uzalishaji wa mazao asilia ya biashara ya Tumbaku, Pamba, Kahawa, Chai,
Pareto, Korosho, Mkonge na Sukari umefikia tani 876,510.83.
39. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 uzalishaji wa mazao ya mafuta umefikia tani
milioni 1.58 ikilinganishwa na tani milioni 1.23 mwaka
2018/2019.
40. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 upatikanaji wa mbegu bora za alizeti na ufuta umefikia tani 441.42 na 90.51
mtawalia. Aidha, mbegu milioni 3.82 za chikichi
zimezalishwa.
41. Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa mazao ya bustani umeongezeka
kutoka tani milioni 6.59 mwaka 2018/2019 hadi tani milioni 7.56 mwaka
2019/2020.
42. Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa mazao ya chakula yanayojumuisha mahindi, mpunga,
mtama/uwele, mikunde, ngano, ndizi,
muhogo na viazi kwa msimu wa
kilimo wa mwaka 2019/2020 umefikia tani 18,196,733.
Masoko ya Mazao
43. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara imeendelea kufuatilia
masoko ya mazao ya kilimo ndani na nje ya nchi. Wizara kupitia Bodi ya Korosho imeratibu minada 70 ya uuzaji wa korosho ambapo
tani 206,718.88 za korosho ghafi zenye thamani ya Shilingi bilioni 473.17
zimeuzwa. Aidha, Wizara
kupitia Bodi ya Tumbaku imekagua tani 20,381.4362 za tumbaku viwandani zenye
thamani ya Dola za Marekani milioni 74.85.
44. Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho tani 8,517 za chai
zenye thamani ya Dola
za Marekani milioni 11.69 zimeuzwa nje ya nchi na tani 1,795 za chai zenye thamani ya Shilingi milioni 16.19 zimeuzwa
katika soko la ndani.
Pia, tani 61,306 za kahawa zenye thamani
ya Dola za Marekani milioni 123.8 na tani 1,346.7 za choroko zenye thamani ya
Shilingi bilioni 2.4 zimeuzwa.
45. Mheshimiwa Spika, katika
kufungua masoko mapya ya mazao, Wizara ilifanya Mkutano wa wafanyabiashara wa
mazao ya nafaka ulioshirikisha Mabalozi wa Nchi za Rwanda, Misri, Burundi, DRC,
Zambia, Sudan Kusini, Malawi, Kenya, Uganda na Msumbiji waweze kuunganishwa na
masoko katika nchi hizo. Vilevile, Wizara imefungua masoko ya mazao mapya ya
parachichi katika nchi za India, Marekani na inakamilisha taratibu za kufungua
soko la zao hilo katika nchi ya China; maharage ya soya katika nchi ya China
ambapo hadi Aprili, 2021 jumla ya wafanyabiashara 49 wamesajiliwa kwenye
Mamlaka ya Forodha ya China kwa ajili ya kuuza soya.
4.6
Kuimarisha
Huduma za Upimaji wa Matabaka na Ubora wa Udongo
46. Mheshimiwa Spika, ili kuleta ufanisi katika matumizi ya chokaa kama virutubishi
vya udongo, Wizara imeandaa Mwongozo wa Matumizi ya Chokaa katika Kilimo
utakaotumiwa na Maafisa Ugani kufundishia wakulima.
5. VIPAUMBELE VYA KIMKAKATI
KWA MWAKA 2021/2022
47.
Mheshimiwa Spika, Mpango na Bajeti ya mwaka 2021/2022 ya Wizara umezingatia
yafuatayo:-
i. Ilani ya Uchaguzi ya Chama
cha Mapinduzi mwaka 2020-2025,
ii. Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano Awamu ya Tatu
(2021/2022 – 2025/2026, na
iii. Program ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP
II)
48. Mheshimiwa Spika, Miongozo yote iliyoainishwa imesisitizwa katika Hotuba ya Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, alipolihutubia
Bunge lako Tukufu tarehe 22 Aprili, 2021. Hotuba hiyo imeweka dira kwa kuanisha
vipaumbele vikubwa na vya kimkakati. Katika kupanga mipango ya mwaka 2021/2022
tumezingatia vipaumbele hivyo kama vilivyosisitizwa kwenye maelekezo ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi,
Mheshimiwa Daniel Chongolo, tarehe 20 Mei, 2021.
49. Mheshimiwa Spika, katika
hotuba yake, Rais aliainisha tija ndogo kama tatizo kubwa linaloikabili sekta
ya kilimo. Hili linaonekana wazi kwenye takwimu zinazohusu mchango wa Sekta ya
Kilimo katika Pato la Taifa ambao umefikia asilimia 26.9 kwa mwaka 2020
ikilinganishwa na asilimia 58.1 ya ajira. Hii ina maana kwamba takribani
theluthi mbili ya nguvukazi hapa nchini inachangia takriban theluthi moja ya
Pato la Taifa, hiki ni kielelezo tosha kwamba tija ni ndogo.
50. Mheshimiwa Spika, mpango mkubwa wa kimkakati ni kuongeza tija katika
uzalishaji. Hivyo, kipaumbele cha kwanza kikubwa cha kimkakati katika kuongeza tija ni
kuweka mkazo katika utafiti utakaozingatia ugunduzi wa aina za mbegu bora na
mbinu bora za kilimo. Ili kufikia malengo hayo tutafanya yafuatayo:-
i.
Kufanya
utafiti wa mbegu bora zenye tija kubwa kwa mfano tafiti zinaonesha kuwa TARI wamefanikiwa kugundua aina za mbegu za muhogo
inayozalisha wastani wa tani 22-50 kwa hekta ikilinganishwa na wastani wa tani
8 kwa hekta zinazozalishwa sasa na wakulima wengi.
Kwa upande wa
pamba tija ya sasa ni kilo 250-300 kwa ekari ikilinganishwa na uwezo wa kufikia
wastani wa kilo 1000-2000 kwa ekari,
ii.
kuongeza bajeti ya TARI kutoka Shilingi
bilioni 7.35 mwaka 2020/2021 hadi Shilingi bilioni 11.63 mwaka 2021/2022, na
iii.
kuimarisha upatikanaji wa fedha za maendeleo ya
utafiti wa kilimo kwa kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Utafiti kwa mujibu wa
Kifungu 26(1) cha Sheria Na. 10 ya mwaka 2016 iliyoanzisha Taasisi ya Utafiti
wa Kilimo Tanzania (TARI Act No. 10, 2016).
51. Mheshimiwa Spika, kipaumbele cha pili cha kimkakati cha kuongeza
tija ni kuongeza uzalishaji wa mbegu bora. Sote tunafahamu nchi yetu bado
hatujajitosheleza kwa mahitaji ya mbegu, hivyo kulazimika kuagiza kutoka nje ya
nchi.
52. Mheshimiwa Spika, ili kuongeza uzalishaji wa
mbegu bora nchi, Wizara imepanga kuendeleza mashamba 13 ya mbegu ya ASA kwa kuweka miundombinu ya umwagiliaji
kwa kutumia fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji; kuongeza bajeti ya uzalishaji
wa mbegu bora kutoka Shilingi bilioni 5.42 mwaka 2020/2021 hadi Shilingi
bilioni 10.58 mwaka 2021/2022; na kuendelea kushirikiana na Sekta Binafsi katika
kuzalisha mbegu bora nchini.
53. Mheshimiwa Spika, kipaumbele cha tatu cha kimkakati ni kuimarisha
huduma za ugani. Idadi ya Maafisa Ugani
wanaotoa huduma za ugani nchini katika
ngazi ya Kata na Vijiji ni 6,704. Idadi hiyo, ni ndogo ikilinganishwa na
mahitaji ya 20,538. Pamoja na idadi hiyo kuwa ndogo, Maafisa ugani hao
wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa vitendea kazi pamoja
na mafunzo rejea.
54. Mheshimiwa Spika, upungufu huo wa maafisa ugani pamoja na changamoto
wanazokabiliana nazo huchangia wakulima wengi kukosa huduma za ugani ikiwemo
matumizi ya mbegu bora, matumizi sahihi ya viuatilifu, zana bora, mbinu bora za
kilimo na taarifa za masoko.
55. Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto hizo, Wizara imeongeza bajeti ya eneo hilo kutoka Shilingi milioni 603 mwaka
2020/2021 hadi Shilingi bilioni 11.5 mwaka 2021/2022. Fedha hizo zitatumika
katika kuimarisha huduma za ugani nchini ikiwa
ni pamoja na kununua pikipiki 1,500, vifaa vya kupima afya ya
udongo, visanduku vya ufundi (Extension
Kit), simu
janja, kuwezesha uanzishwaji wa mashamba ya mfano kwa kila Afisa Ugani na kutoa
mafunzo rejea. Vilevile, maafisa ugani
watasimamiwa katika kuanzisha mashamba darasa kulingana na mahitaji ya wakulima
kwa ajili ya kuendeleza kilimo katika eneo husika.
56.
Mheshimiwa Spika, tutaianza safari yetu ya
kuboresha huduma za ugani katika mikoa mitatu ya kielelezo ambayo ni Dodoma, Singida
na Simiyu. Mikoa hiyo ina fursa kubwa ya kuzalisha mazao ya mafuta hususan
alizeti na pamba. Katika Mikoa hiyo maafisa ugani wote watapewa pikipiki, vifaa
vya kupima afya ya udongo, visanduku vya ufundi (Extension Kits), simu janja, kuwezesha uanzishwaji wa mashamba ya
mfano kwa kila Afisa Ugani na kutoa mafunzo rejea yatakayozingatia mazao yote
yanayolimwa katika maeneo hayo. Pia maafisa ugani hao, watawezeshwa kuanzisha
mashamba darasa.
57.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwawezesha maafisa ugani hao, tunatarajia
utoaji wa huduma za ugani utaimarika, wakulima wengi watafikiwa kwa wakati na
tija ya uzalishaji itaongezeka. Kwa mfano matumizi ya simu janja yatawezesha
wakulima kupata utatuzi wa changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo taarifa za masoko ya mazao ya kilimo
wanayozalisha. Mafanikio yatakayopatikana katika mikoa hiyo ya kielelezo, yataenezwa
katika mikoa mingine nchini.
58.
Mheshimiwa Spika, Wizara pia itaendelea kushirikiana na Sekta
Binafsi katika kuimarisha huduma za ugani kwa kutumia mbinu zilizoonesha
mafanikio katika kuongeza tija. Kwa mfano, TAHA inatoa mafunzo ya kilimo bora
cha mazao ya bustani na kuwaunganisha wakulima na watoa huduma za pembejeo na
masoko. Vilevile, Kampuni ya kutoa huduma kwa wakulima wadogo wa chai Njombe (Njombe Outgrowers Services Company) imeajiri
maafisa ugani, na inatoa huduma za uvunaji na uuzaji wa majani mabichi ya chai
kwenye kiwanda cha Uniliver. Pia, Chama kikuu cha Ushirika Kahama (KACU)
kimeajiri maafisa ugani kwa ajili ya kutoa huduma kwenye mazao ya tumbaku na
pamba.
59.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua mtawanyiko wa mazao ya kilimo
yanayozalishwa nchini na mahitaji ya soko, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya
Rais TAMISEMI na wadau wengine wa kilimo itasimamia utoaji wa huduma za ugani
katika mikoa yote ili kuongeza tija katika mazao kulingana na viwango vya
uzalishaji vinavyohitajika.
60. Mheshimiwa Spika, kipaumbele
cha nne cha kimkakati ni kuimarisha kilimo cha umwagiliaji. Kama
tunavyofahamu, kilimo chetu nchini kinategemea mvua kwa asilimia kubwa ambazo
hazitabiriki kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Aidha, Kilimo cha umwagiliaji
kinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ubovu wa miundombinu,
kutokamilika kwa baadhi ya miradi ya umwagiliaji, kukosekana kwa miundombinu ya
umwagiliaji yenye fursa za umwagiliaji, mitaji ya ujenzi wa miundombinu ya
umwagiliaji na elimu ndogo ya matumizi ya teknolojia za umwagiliaji.
61. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha kilimo cha umwagiliaji nchini,
Wizara imepanga kuongeza eneo la umwagiliaji kwa
kuhamasisha wadau kuwekeza katika ujenzi miundombinu, uvunaji wa maji na
uchimbaji wa visima kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Aidha, Wizara kupitia
Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji (IDF) ulioanzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha
52 cha Sheria ya Umwagiliaji Na. 4 ya mwaka 2013 itakamilisha ujenzi wa
miundombinu ya umwagiliaji ikiwemo mashamba 13 ya mbegu ya ASA, kukarabati
miundombinu ya umwagiliaji, kukamilisha miradi ya umwagiliaji, kujenga mabwawa
na kufanya upembuzi yakinifu kwenye miradi mipya.
62. Mheshimiwa Spika, Wizara imeanza kufanya tathmini ya skimu zote za
umwagiliaji na maeneo yanayofaa kwa umwagiliaji. Lengo ni kuhakiki eneo
linalomwagiliwa, kubaini mahitaji halisi ya rasilimali za kuendeleza kilimo cha
umwagiliaji kwa ajili ya kuboresha Mpango Kamambe wa Uendelezaji wa Kilimo cha
Umwagiliaji Nchini.
63. Mheshimiwa Spika, kipaumbele cha tano cha kimkakati ni kuimarisha upatikanaji wa masoko
ya mazao ya kilimo. Changamoto ya masoko nchini ina sura kuu mbili; kwanza ni
uzalishaji mdogo usiokidhi mahitaji ya soko na pili ni kuwepo kwa uzalishaji
mkubwa ikilinganishwa na upatikanaji wa masoko. Kwa mfano, viwanda vya kukamua
mafuta ya alizeti vinafanya kazi takribani miezi minne kwa mwaka kutokana na
ukosefu wa malighafi. Kwa upande wa mazao ya nafaka ikiwemo mahindi na mpunga,
uzalishaji wake ni mkubwa na ziada inakosa soko.
64. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha upatikanaji wa masoko ndani na nje ya
nchi, Wizara itaimarisha
utekelezaji wa kilimo cha mkataba katika mazao ya shayiri, ngano, alizeti,
zabibu, maharage ya soya na mazao mengine kwa kutoa mwongozo wa mikataba baina
ya wakulima na wenye viwanda vya kusindika mazao.
65. Aidha, Wizara itaratibu ubia wa kibiashara baina ya
wafanyabiashara wa mazao hapa nchini na nchi za nje zenye fursa kubwa ya masoko
ikiwemo Sudani Kusini, DRC, Saudi Arabia, Falme za Kiarabu, Msumbiji, Kenya,
Vietnam na China. Uratibu huo utahusisha safari za wafanyabiashara kwenda
katika nchi hizo na kuanzisha vituo vya kuonesha bidhaa za mazao ya kilimo
kutoka Tanzania.
66. Mheshimiwa Spika, Wizara itawezesha upatikanaji wa masoko ya
uhakika wa mazao la shayiri na hivyo kuongeza uzalishaji wa ndani; inaendelea
kuratibu uwekezaji wa kampuni za bia ili kuwekeza Dola za Marekani milioni 42 katika
kiwanda cha kutengeneza kimea kitakachojengwa Jijini Dodoma chenye uwezo wa
kusindika shayiri tani 35,000 kwa mwaka kutoka kwa wakulima. Wizara kupitia Bodi
ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko imeingia mkataba na wakulima kwa lengo la
kununua tani 21,600 za ngano.
67. Mheshimiwa Spika, Wizara pia, itaendelea kuratibu
makubaliano kati ya wasindikaji na wakulima ambapo wasindikaji watanunua kwanza
ngano inayozalishwa ndani kabla ya kuagiza kutoka nje. Aidha, katika kuimarisha
kilimo cha mkataba cha zao la alizeti, Wizara itaendelea kuwaunganisha wakulima
na wasindikaji na kuandaa mazingira bora ya uwekezaji katika viwanda vya
kusindika alizeti.
68. Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kufungua mipaka ya kuuza mazao nje ya
nchi na kutoa elimu ya utumiaji wa mfumo wa utoaji vibali kwa njia ya
kielektroniki (ATIMS) kwa ajili ya kusafirisha mazao nje ya nchi. Ninapenda
kutoa wito kwa wafanyabiashara wa mazao kutumia mfumo huo. Aidha, ninaviomba
vyombo vya usalama wa raia tushirikiane kuwezesha biashara ya mazao ya kilimo.
69.
Mheshimiwa Spika, kipaumbele cha sita cha kimkakati ni kuimarisha KILIMO ANGA kwa ajili
ya kudhibiti visumbufu vya milipuko na vihamavyo kama vile nzige, kwelea kwelea
na viwavijeshi vamizi. Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, kumekuwa na
ongezeko la visumbufu vigeni vinavyoathiri uzalishaji wa mazao na kusababisha
upotevu wa mazao hadi asilimia mia moja endapo havitadhibitiwa kikamilifu na
kwa wakati. Aidha, baadhi ya visumbufu kama vile nzige na kwelea kwelea
udhibiti wake unahitaji vifaa maalum kama vile ndege kwa ajili ya savei na unyunyuziaji
wa viuatilifu.
70. Mheshimiwa Spika, Ili kutekeleza kipaumbele hicho, Wizara imeongeza bajeti ya KILIMO ANGA
kutoka Shilingi milioni 150 mwaka 2020/2021 hadi bilioni tatu (3) mwaka
2021/2022. Fedha hizo, zitatumika kununua ndege moja mpya kwa ajili ya udhibiti
wa visumbufu hivyo.
71. Mheshimiwa Spika, kipaumbele cha saba cha kimkakati ni kuimarisha
mifumo ya upatikanaji wa mitaji.
Upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya shughuli za kilimo umekuwa na changamoto
kutokana na riba kubwa zinazotozwa, masharti ya kupata mikopo kutoka taasisi za
fedha na vihatarishi katika sekta ya kilimo.
Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa ni asilimia 30 tu ya wakulima
wanaofikiwa na huduma za mikopo. Aidha, ni asilimia kati ya 7 na 9 ya mikopo
iliyotolewa na mabenki ya biashara katika kipindi cha miaka mitano iliyopita imeelekezwa
kwenye sekta ya kilimo.
72. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2021/2022, Wizara itafanya tathmini ya mifumo ya upatikanaji wa mitaji
kwa wakulima wadogo na wawekezaji wengine kwenye sekta ya kilimo ili kuibua
vizuizi na kuvitafutia majawabu kwa ajili ya kuimarisha ugharamiaji wa mazao
katika mnyororo wa thamani. Aidha, Wizara imeunda jopo maalum linalohusisha watendaji
wakuu wa taasisi za fedha, ambalo litaongozwa na Naibu Waziri wa Kilimo
Mheshimiwa Hussein Bashe (Mb), kwa ajili ya kupitia minyororo ya thamani ya
mazao na kushauri namna bora ya upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya uendelezaji
wa kilimo nchini.
73. Mheshimiwa Spika, vilevile Wizara imeunda Timu ya Wataalam inayopitia na
kuchambua mifumo ya kikodi katika sekta ya kilimo kwa lengo la kuvutia
uwekezaji katika mnyororo wa thamani ya mazao ya kilimo. Katika hatua za awali,
Timu imeanza kazi hiyo katika tasnia za mazao ya alizeti, shayiri na dhamana za
mikopo. Maelezo zaidi na mambo mengine ya vipaumbele yanapatikana kwenye Hotuba nzima iliyowekwa mezani.
SHUKRANI
74.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii
kuzishukuru Nchi na Mashirika ya Kimataifa ambayo yamesaidia Wizara katika
kuendeleza kilimo. Naomba kutaja baadhi ya Nchi na Mashirika ya Kimataifa kama
ifuatavyo: Serikali za Japan, Marekani, Uingereza, Ireland, Malaysia, China,
Indonesia, Korea ya Kusini, India, Misri, Israel, Ubelgiji, Ujerumani, Finland,
Norway, Brazil, Uholanzi, Vietnam, Canada na Poland. Ninayashukuru pia Mashirika na Taasisi za
Kimataifa zifuatazo: Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, AU, IFAD,
DFID, UNDP, FAO, JICA, EU, ENABEL, GIZ, UNICEF, WFP, CIMMYT, ICRISAT, ASARECA,
USAID, KOICA, ICRAF, IITA, IRRI, ILRI na CABI. Nyingine ni EAC, SADC, AVRDC,
AGRA, KILIMO TRUST, CIP, CIAT/PABRA, UNEP, WARDA, Shirika la Kudhibiti Nzige wa
Jangwani (DLCO-EA) na HELVETAS. Wadau
wengine ni Shirika la Kudhibiti Nzige Wekundu (IRLCO-CSA), Bill and Melinda Gates Foundation, Gatsby Trust, Rockfeller Foundation, Clinton Foundation, Aga
Khan Foundation, TAHA
na Asasi
zisizo za kiserikali nyingi ambazo hatuwezi kuzitaja zote hapa.
75.
Mheshimiwa Spika, natoa shukrani kwa wakulima wote kwa kazi kubwa wanazofanya kuendeleza
kilimo nchini. Ni wazi kuwa mafanikio ya kilimo yanatokana na juhudi na
ushirikiano mkubwa na Serikali. Kipekee nirudie kuwashukuru wananchi wa Jimbo
langu la Rombo kwa namna wanavyoniunga mkono na kunipa ushirikiano. Naomba wote
watambue kuwa kilimo ni maisha, uchumi, biashara, viwanda na ajira.
7. MAOMBI
YA FEDHA KWA MWAKA 2021/2022
7.1
Makusanyo ya Maduhuli
76. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2021/2022, Wizara
inatarajia kukusanya Shilingi 34,495,000,000 kutokana na ada za ukaguzi
wa mazao yanayouzwa nje ya nchi au kuingizwa nchini, uuzaji wa nyaraka za
zabuni, ukodishaji wa mitambo ya Tume ya Umwagiliaji. Kati ya fedha hizo,
Shilingi 4,480,000,000 zitakusanywa
katika Fungu 43 na Shilingi 30,015,000,000
zitakusanywa kwenye Fungu Na.05.
7.2
Fedha kwa Mafungu yote (43, 24 na 05)
77. Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2021/2022, Wizara ya Kilimo inaliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla
ya Shilingi 294,162,071,000 kupitia
Fungu 43, Fungu 05 na Fungu 24 kama ifuatavyo;
7.2.1 Fedha
kwa Fungu 43
78.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Wizara inaomba kuidhinishiwa
jumla ya Shilingi 228,871,243,000 kupitia Fungu 43 kwa ajili ya matumizi ya
Kawaida na Maendeleo.
Kati
ya fedha hizo, Shilingi 164,748,000,000
ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Maendeleo ambapo Shilingi 82,180,000,000 ni fedha za ndani na
Shilingi 82,568,000,000 ni fedha za
nje. Aidha, Shilingi 64, 123,243,000 ni kwa ajili ya matumizi ya
kawaida, ambapo Shilingi 42,492,457,000
ni kwa ajili ya mishahara na Shilingi 21,630,786,000
ni kwa ajili ya matumizi mengineyo.
7.2.2 Fedha kwa Fungu 05
79.
Mheshimiwa Spika, jumla ya Shilingi 51,487,450,000
zinaombwa. Kati ya fedha hizo, Shilingi 46,500,000,000
ni kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo ambapo Shilingi 35,000,000,000 ni fedha za Ndani na
Shilingi 11,500,000,000 ni fedha za
Nje. Aidha, kati ya fedha zinazoombwa, Shilingi 4,987,450,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ambapo Shilingi 3,349,266,000 ni kwa ajili ya Mishahara
ya Watumishi wa Tume na Shilingi 1,638,184,000
ni kwa ajili ya Matumizi mengineyo.
7.2.3 Fedha kwa Fungu 24
80.
Mheshimiwa Spika, jumla ya Shilingi 13,803,378,000 zinaombwa. Kati
ya fedha hizo, Shilingi 6,549,009,000
ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ya Tume na Shilingi 4,654,984,000 ni kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi wa Tume.
Aidha, Shilingi 1,000,000,000 ni kwa
ajili ya Matumizi ya kawaida ya COASCO
na Shilingi 1,599,385,000 ni kwa ajili ya mishahara ya
COASCO.
81. Mheshimiwa
Spika, hotuba
hii pia inapatikana katika tovuti ya Wizara: www.kilimo.go.tz
8. HITIMISHO
82.
Mheshimiwa Spika,
NAOMBA KUTOA HOJA
0 comments:
Post a Comment