Na Mathias Canal, Wizara ya kilimo-Kahama
Chama Kikuu Cha Ushirika Kahama (KACU) kimewalipa malipo ya pili wakulima wa Pamba waliouza Pamba msimu wa mwaka 2019/2020
Akizungumza leo tarehe 18 Mei 2021 katika hafla ya kukabidhi fedha hizo kwa wakulima wa Pamba iliyofanyika katika Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga, Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Tanzania Marco Mtunga amekipongeza Chama Kikuu Cha Ushirika Kahama (KACU) kwani kimekuwa chama mkombozi katika zao la Pamba nchini.
Kadhalika Mtunga amesema kuwa kiasi cha Fedha kitatengwa kwa ajili ya Tume ya Maendeleo ya ushirika ili Afisa Ushirika aweze kuzungukia Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) mara kwa mara kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali kwenye AMCOS badala ya kusubiri mwisho wa msimu.
Amesema kuwa Bodi ya pamba Tanzania imekusudia Kutumia mahakama inayotembea ili kuwabaini wabadhilifu wa mali za Ushirika na kuwachukulia hatua za haraka.
Akisoma taarifa ya chama hicho Mwenyekiti wa KACU Ndg Emmanuel Cherehani amesema kuwa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020 Mfuko wa Pembejeo ulikosa Fedha za kuhudumia zao hilo hivyo KACU walifanikisha kukopa Tsh Bilioni 8 iliyopelekea kupatikana kwa pembejeo ambazo zilitumika katika msimu wa mwaka 2020/2021.
Amesema kuwa KACU imejipanga kunua Pamba katika msimu huu kwa bei nzuri ambapo amewataka wakulima wa Pamba kutumia fursa hiyo ya kujiongezea kipato kutokana na uwepo wa KACU.
Cherehani amewapongeza Viongozi mbalimbali nchini kwa kusimama kidete katika kuimarisha sekta ya Ushirika nchini ambapo amewataja viongozi hao kuwa ni pamoja na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri na Naibu Waziri wa Kilimo, Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Shinyanga iliyokuwa ikiongozwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe Zainab Telack.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe Anamringi Macha ambaye ndiye alikuwa Mgeni rasmi katika hafla hiyo amesema kuwa KACU kimekuwa ni chama cha mfano kwani kimesimamia kwa weledi na ufanisi wa mali za Ushirika.
Amesema kuwa Chama hicho kimetekeleza vyema majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuwalipa wakulima malipo ya awali na hatimaye kimefanikiwa kuwalipa malipo ya pili jambo ambalo huenda likapelekea katika miaka ijayo wakulima wakaweza kulipwa malipo ya awamu ya tatu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe Nyabaganga Taraba amewasisitiza wakulima wa Pamba nchini kusimamia ubora wakati wote wa msimu wa kilimo kwani kufanya hivyo kutaongeza wigo wa kuingiza pato kubwa wakati wa uuzaji wa Pamba.
Amesema kuwa vipo vyama vingi vya Kilimo lakini vimeshindwa kusimamia majukumu yake ipasavyo hivyo amevitaka kutumia nafasi zao kujifunza kupitia KACU.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment