METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, June 27, 2020

WAKULIMA WAASWA KUCHANGAMKIA FURSA YA KILIMO CHA PARACHICHI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akipata maelezo kuhusu mitambo inayotumika kutengeneza na kusaga zao la parachichi kutoka kwa Meneja Uzalishaji wa kiwanda cha Olivado Bw. Ngukula Lihuluku wakati wa ziara yake katika kiwanda hicho kilichopo Wilaya ya Wanging’ombe Mkoani Njombe.
Meneja Uzalishaji wa kiwanda cha Maparachichi cha Olivado Bw. Ngukula Lihuluku akimuonesha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki mitambo maalum ya kutengenezea bidhaa zitokanazo na mafuta ya parachichi alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Wilaya ya Wanging’ombe mkoani  Njombe Juni 25, 2020
Wakulima nchini wameaswa kuchangamkia fursa za kilimo cha zao la parachichi kwa kuzingatia uwepo wa soko la uhakika ndani na nje ya nchi kwa kuongeza uzalishaji wa zao hilo kwa ubora unaokidhi viwango vya kimataifa.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji Mhe. Angellah Kairuki wakati wa ziara ya kutembelea maeneo ya uwekezaji mkoani Njomba.
Waziri Kairuki alipotembelea miradi ya kilimo tarehe 24 Juni, 2020 kwa lengo la kukagua, kusikiliza na kutatua changamoto za wawekezaji katika sekta mbalimbali ili kuendelea kuboresha mazingira ya wawekezaji nchini.
Waziri kairuki alielea hayo mara baada ya kukagua kiwanda cha kuzalisha maparachichi cha TANZANICE kilichopo Njombe mjini pamoja na OLIVADO kilichopo Wilaya ya Wanging’ombe mkoani humo.
Alitoa rai hiyo kutokana na changamoto zilizoelezwa na wamiliki wa viwanda hivyo mara baada ya kuainisha changamoto zao ikiwemo ukosefu wa wakulima wa kutosha wanaokidhi uhitaji wa soko lililopo ndani na nje ya nchi.
“Tumieni fursa ya zao hili kwa kuzingatia linamatumizi mengi ikiwemo, mafuta ya kula, dawa pamoja na kuchanganya katika vipodozi mbalimbali vinavyotumika kwa matumizi ya binadamu,”alieleza
Aliongezea kuwa, awali zao lilikuwa na mauzo hafifu kutokana na changamoto mbalimbali ambapo hadi mwaka 2015 ilikuwa inasafirishwa takriban tani 3,279 na kufikia zaidi ya tani 9,000 kwa mwaka hadi sasa.
Aidha Waziri aliongezea kuwa zao la parachichi limeendelea kuwa na tija nchini, hivyo wakulima wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo kwa kila hali ili kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo nchini.
“Parachichi ni zao linalokuwa kwa kasi kwa kuangalia hapo nyuma uzalishaji ulikuwa takribani tani 20,000 pekee ingawa kwa kipindi cha miaka minne tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani kumekuwa na ongezeko kubwa ya zaidi ya mara tisa na nusu kufikia tani 190,000 kwa mwaka” alisema Waziri Kairuki
Akitoa taarifa ya kiwanda cha TANZANICE, Meneja viwango Bw. Timothy Msofe alibaini changamoto kadhaa ikiwemo, ukosemu ya elimu ya kilimo sahihi cha maparachichi kwa wakulima walio wengi, ukosefu wa wataalam wa zao hilo, uzalishaji mdogo usioendana na soko pamoja na changamoto za miundombinu unaochangia kuchelewa na uhalibifu wa bidhaa wakati wa usafirishaji.
Aidha alibainisha kuwa, kampuni imefanikiwa kuwafikia wakulima 200 kwa kuwapatia ujuzi wa kilimo bora na sahihi cha zao la parachichi ambapo imeelezwa idadi hiyo kuwa ndogo kulinganana mahitaji yaliyopo.
“Tunalenga kufikia kundi kubwa la wakulima ili kuwa na tija ambapo tunapaswa kuwa na wakulima zaidi ya 600 kwa mkoa wetu ili kulifikia soko ambapo kwa sasa kiwanda kinauwezo wa kusafirisha tani 22 tu ambayo haikidhi soko lililopo,”alisema Msofe.
Naye mmoja wa wafanyakazi wa kampuni inayosafirisha maparachichi nchi za nje Bw. Movick Mteleka alieleza kuwa, uwepo wa fursa kubwa wa masoko nchi za Ulaya  ikiwemo Ufaransa hivyo ni vyema wakulima wa zao hilo wakaiona fursa na kulima maparachichi yanayokidhi hitaji lililopo.
“Maparachichi yanayozalishwa hayana viwango vya kutosha kukidhi soko la nje hivyo ni rai kwa wakulima kujitokeza kwa wingi na kupata mafunzo ili kulima kwa tija,”alisema Movick.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com