Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Chikoko, iliyopo katika Wilaya ya Ruangwa, Mkoani Lindi, wakati alipotembelea shule hiyo, Februari 26, 2021.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa Shule Maalum ya Sekondari ya Wasichana Ruangwa, Mkoani Lindi. Februari 26, 2021.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua nyumba za walimu zilizojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (T.E.A), wakati alipotembelea, Shule ya Sekondari Liuguru, wilayani Lindi. Februari 26, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa mradi wa shule maalumu ya sekondari ya wasichana Ruangwa na amesema kwamba Serikali imeadhamiria kuwekeza katika elimu ya mtoto wa kike kwa lengo la kumuwezesha kutimiza ndoto zake kielimu.
Baada ya kukagua mradi huo, Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na maendeleo yake na amewataka waliokabidhiwa jukumu la kusimamia ujenzi huo waendelee kuwa waaminifu na wahakikishe wanashirikiana vizuri na mjenzi ili akamilishe kwa wakati uliokusudiwa.
Waziri Mkuu amekagua ujenzi wa mradi huo leo (Ijumaa, Februari 26, 2021). Shule hiyo ya mchepuo wa sayansi inayojengwa katika kijiji cha Dodoma kata ya Nachingwea wilayani Ruangwa kupitia fedha za mpango wa lipa kwa matokeo (EP4R), ambapo awamu ya kwanza imegharimu sh. milioni 700.
Amesema kukamilika kwa ujenzi wa shule hiyo kunatarajiwa kuinua kiwango cha ufaulu kwa mtoto wa kike ambaye ndiyo mlengwa. ”Tumedhamiria kuinua kiwango cha elimu kwa watoto wa kike kwa kuwaboreshea mazingira ya kujifunzia. Tunataka watoto wa kike wasome bila usumbufu.”
Waziri Mkuu amesema walianzisha mradi wa ujenzi wa shule ya wasichana katika wilaya hiyo ili kutoa nafasi nzuri kwa mtoto wa kike kupata fursa ya kusoma vizuri akiwa katika mazingira rafiki yatakayo muepusha na changamoto mbalimbali zinazowafanya washindwe kutimiza ndoto zao kielimu.
Kwa upande wake, fundi mkuu wa mradi huo, Michael Fabian amesema mradi wa ujenzi wa shule hiyo unajengwa kwa awamu na ya kwanza inahusisha jengo la utawala, vyumba vinane vya madarasa, nyumba mbili za walimu, matundu 16 ya vyoo, jengo la maabara za fizikia, kemia, baiolojia na jengo la jiografia.
Shule hiyo ambayo inatarajiwa kufunguliwa mara baada ya kukamilika kwa majengo ya awamu ya kwanza na ya pili. Awamu ya pili ujenzi wa mradi huo unaojengwa kwa kupitia mfumo wa force account inahusisha mabweni, bwalo la chakula na kichomea taka.
Baada ya kukagua mradi wa shule maalumu ya sekondari ya wasichana Ruangwa, Waziri Mkuu alitembelea shule ya sekondari ya wasichana ya Liuguru iliyopo kata ya Narungombe ambapo alizungumza na walimu, wazazi na wanafunzi ambao aliwasisitiza wanafunzi kuzingatia masomo.
Waziri Mkuu amesema suala la mtoto wa Kitanzania kwenda shule ni la lazima na si hiayari hivyo wazazi na walezi wametakiwa kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanakwenda shule na watakaoshindwa kuwapeleka watoto wao shule watachukuliwa hatua za kisheria. ”Serikali imeondoa michango yote ya hovyo ili kutoa fursa ya watoto kusoma.”
Awali, Waziri Mkuu alitembelea shule ya msingi Chikoko iliyoko katika kata ya Makanjiro ambapo amewataka wananchi washikamane na wajitokeze kwa wingi katika utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya ujenzi wa madarasa.
Naye, Diwani wa kata hiyo, Simon Machela alimuhakikishia Waziri Mkuu kwamba atashirikiana na uongozi wa wilaya pamoja na wananchi wa kata hiyo katika kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.
0 comments:
Post a Comment